Vijana wamzawadia Rais Samia ng’ombe wawili

Rais Samia akizungumza katika mkutano na vijana uliofanyika jijini Mwanza leo Jumanne Juni 15, 2021.
Muktasari:
- Vijana wa mikoa ya Kanda na Ziwa imempa zawadi mbalimbali Rais Samia Suluhu Hassan wakiwemo ng’ombe wawili.
Mwanza. Vijana wa mikoa ya Kanda na Ziwa imempa zawadi mbalimbali Rais Samia Suluhu Hassan wakiwemo ng’ombe wawili
Kanda ya Ziwa inaundwa na mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Simiyu, Kagera na Shinyanga.
Akizungumza kwa niaba ya vijana wa kanda hiyo wakati wa mkutano wa Rais Samia na vijana unaofanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza leo Jumatatu Juni 15, 2021 Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobas Katambi ametaja zawadi nyingine kuwa ni kutoka sekta ya kilimo ikiwemo zao la pamba, uvuvi na biashara.
“Vijana wa kanda ya ziwa pia wameandaa zawadi ya michoro na picha mbalimbali zenye taswira ya sura ya Rais Samia zilizochorwa na vijana kuonyesha vipawa na vipaji vyao katika sanaa,” amesema Katambi ambaye pia ni mbunge wa Shinyanga Mjini
Kutokana na ng'ombe hao kutoweza kufikishwa jukwaani, vijana hao wamemkabidhi Rais Samia kamba mbili kama ishara ya kupokea mifugo hiyo kulingana na mila na desturi za jamii ya wafugaji.
Mkutano huo wa Rais na vijana wa kanda ya ziwa kwa niaba ya wenzao wa nchi nzima umehudhuriwa na mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, wabunge vijana na wa majimbo, mameya na wakurugenzi kutoka halmashauri za mikoa ya kanda ya ziwa.