Vikao kamati za Bunge kuanza Machi 8, haya kufanyika

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Muktasari:

Vikao vya kamati za Bunge la 12 vinatarajia kuanza Machi 8 hadi 26, 2021 kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge Machi 30, 2021.

Dar es Salaam. Vikao vya kamati za Bunge la 12 vinatarajia kuanza Machi 8 hadi 26, 2021 kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge Machi 30, 2021.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Machi 4, 2021 na ofisi ya Bunge jijini Dodoma imeeleza kuwa shughuli za kamati katika kipindi hicho ni kupokea mapendekezo ya Serikali kuhusu mpango, kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali mwaka wa fedha 2021/22.

Shughuli nyingine ni wajumbe wa kamati za kisekta kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

“Ziara ya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma kwenye mamlaka za Serikali za mitaa, Serikali kuu na taasisi za umma ili kuzingatia masharti ya sehemu ya nne ya nyongeza  ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Juni 2020,” inaeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shughuli nyingine ni uchambuzi wa taarifa za uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia mashirika, taasisi na kampuni ambazo Serikali ina hisa pamoja na kukagua shughuli za uwekezaji zilizofanywa na Serikali.

“Wajumbe wa kamati za kisekta, kamati ya Bunge na kamati ya masuala ya Ukimwi watafanya uchambuzi wa taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/21 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22,” inaeleza.

Shughuli nyingine ni uchambuzi wa sheria ndogo zilizowasilishwa katika mkutano wa pili wa Bunge ili kutekeleza masharti ya kifungu cha 11cha nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge.


 “Kwa mujibu wa kanuni ya 117(5) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Juni 2020 kutakufanyika mashauriano kati ya kamati ya uongozi na kamati ya bajeti kuhusu masuala muhimu yatakayokuwa yamejitokeza,” imeeleza taarifa hiyo.