Vikwazo vinne wanavyokumbana navyo watetezi, wasaidizi wa sheria
Muktasari:
Watetezi na wasaidizi wa sheria nchini wametaja ukosefu wa elimu kwa baadhi ya watumishi wa Serikali na wananchi, kutembea umbali mrefu, mgongano wa kiutendaji na ukosefu wa raslimali fedha ni miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha utendaji kazi wao.
Mwanza. Watetezi na wasaidizi wa sheria nchini wametaja ukosefu wa elimu kwa baadhi ya watumishi wa Serikali na wananchi, kutembea umbali mrefu, mgongano wa kiutendaji na ukosefu wa raslimali fedha ni miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha utendaji kazi wao.
Wakizungumza Agosti 28, 2023 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo ya siku mbili kwa watetezi na wasaidizi wa sheria Kanda ya Ziwa yanayofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (Saut) Mwanza na kuandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDs), wamesema mgongano wa kiutendaji hutokea baina yao na viongozi wa Serikali.
“Wakati wa kutetea haki za wanawake na watoto kunachangamoto mbalimbali tunakumbana nazo kama umbali wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, mgongano wa utendaji kazi wetu sisi na viongozi wa Serikali…wengine hawajui majukumu yetu sisi tunavyoenda kutetea haki za watu,”amesema Sophia Donald, Mkurugenzi wa Shirika la Sauti ya Wanawake Ukerewe
Naye Mkurugenzi wa Tuwakomboa Paralegal Organization, Bonny Matto ameiomba Serikali kuwajengea uwezo watumishi wake kuhusu masuala ya kisheria na namna watetezi na wasaidizi wa sheria wanavyofanya kazi ili kutatua changamoto ya kuingiliana katika majukumu.
“Wasaidizi wa sheria tumekuwa tukikumbana na changamoto ya baadhi ya watumishi wa serikali kukosa elimu hali ambayo inatukwamisha katika kutekeleza majukumu yetu kwahiyo niwaombe Serikali wawe wanawajengea uwezo pindi wanapoingia kushika nafasi hizo na kuwapatia semina za mara kwa mara zitakazo waelimisha zaidi,”amesema Matto
Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Saut, Balozi Profesa Costa Mahalu ametoa wito kwa watetezi na wasaidizi wa sheria kuzidi kutoe elimu ya sheria kwa wananchi huku akiwataka kuacha kushabikia sheria ambazo haziendani na tamaduni na maadili ya kitanzania.
“Kila wakati kunapokuwa na suala la haki za binadamu tuweze kuzifurahia na kuzilinda japo kuwa sio zote kuna baadhi tunaweza kuziita haki za binadamu kwa wenzetu wa mataifa ya Ulaya, Asia na Amerika lakini kwa mataifa ya bara la Afrika zikawa zinatuumiza…unakuta ni kitu ambacho hakiendani na tamaduni na maadili yetu kwahiyo katika kuangalia tuwe makini sana,”amesema
Akizungumzia malengo ya mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Utetezi wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Paul Kisabo amesema yanalenga kuwajengea uwezo watetezi na wasaidizi wa sheria kuhusu sheria mbalimbali zinazotungwa na kubadilishwa, kuwakumbusha majukumu na wajibu wao, kusikiliza na kupokea maoni na changoto zinazowakabili ili kuzifanyia kazi.
“Changamoto ya watu kutokufahamu sheria na haki zao zimekuwa zikipelekea kupoteza haki zao za msingi ndio maana tumekuja kutoa mafunzo haya ili wakitoka hapa waweze kwenda maeneo mbali zaidi na kuwafikia watu wengi zaidi kwa kuwaelimisha na kuwasaidia kupata haki za msingi,”amesema Kisabo