Viongozi elimu ya juu watwishwa zigo la ajira kwa wahitimu

Muktasari:
- Viongozi wa taasisi hizo wanapaswa kujitathmini na kuchukua hatua za kimaendeleo kuhakikisha vyuo vikuu vinakuwa kinara katika kutengeneza wanataaluma bora.
Dar es Salaam. Viongozi wa taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania wamehimizwa kuzingatia maadili, weledi na uzalendo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Pia, wametakiwa kutumia maarifa waliyonayo na ubunifu kuleta suluhu ya changamoto zinazozikabili taasisi hizo ikiwamo ile ya ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu, Juni 2, 2025 na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa viongozi wa idara mbalimbali wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Daudi amesema miongoni mwa sababu inayochangia changamoto hiyo ni kuporomoka kwa ubora wa elimu nchini.
"Changamoto hiyo imesababisha hata baadhi ya vyuo hapa nchini kutotambuana au kutilia shaka sifa za wahitimu katika chuo kingine iwe katika ajira au maombi ya kujiunga na chuo, hii haiko sawa," ameeleza Daudi.
Amewaeleza kama viongozi wa taasisi hizo wanapaswa kujitathmini na kuchukua hatua za kimaendeleo kuhakikisha vyuo vikuu vinakuwa kinara katika kutengeneza wanataaluma bora.
Pia, amewasisitiza kuendelea kufanyika kwa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi hao akisema ni sehemu muhimu ya kukuza uongozi bora katika taasisi za elimu ya juu.
"Warsha hii ni ushahidi wa uelewa wa kina wa kwamba uongozi bora hauishii tu katika vyeo au mamlaka, bali unajengwa kupitia mafunzo endelevu, tafakari ya kina, ubunifu wa mikakati na uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi mipango ya maendeleo.”
Awali, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amewasisitiza viongozi hao kuongoza kwa misingi ya ushirikiano na kuepuka mashindano yasiyo na tija katika ufanyaji wa kazi zao.
Amewahimiza wawajibikaji huku akiwataka kutambua kiongozi wa kitengo sio mmoja wa wafanyakazi katika kitengo chake, bali ana nafasi ya kipekee katika uamuzi.
"Kwa mfano, kiongozi wa kitengo ndiye mtu mkuu mwenye wajibu kwa kila kinachotokea ndani ya kitengo," ameeleza.
Pia, amesisitiza umuhimu wa mafunzo kwa viongozi wa taasisi kwani ni fursa kwa baadhi ya viongozi wapya kupata uelewa wa misingi ya uongozi katika taasisi.
"Ni muhimu kuhakikisha kila kiongozi na msimamizi mwandamizi ana uelewa wa kutosha wa misingi na taratibu muhimu za kushughulikia majukumu ya uongozi katika taasisi ili kazi ziweze kufanyika kwa ufanisi," amesema.