Viongozi Njombe wapiga magoti kushukuru mradi wa maji
Muktasari:
- Kutokana na mahitaji mkubwa ya maji katika miji ya Mkoa wa Njombe, Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo amewaongoza viongozi wenzake kupiga magoti wakishukuru mradi mkubwa utakaoanza kutekelezwa.
Njombe. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga amewaongoza wabunge na wenyeviti wa halmashauri za wilaya za mkoa huo kupiga magoti mbele ya wanachama wa CCM kushukuru ujio wa mradi wa maji.
Lakini pia viongozi hao walikuwa wakishukuru utekekezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo huku wakimuomba Rais Samia Hassan Suluhu kumuacha Njombe, mkuu wa Mkoa huo Antony Mtaka.
Kwa muda mrefu baadhi ya miji ya mkoa huo imekuwa ikihaha kupata maji ya uhakika kwa mwaka mzima.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga amesema zaidi ya Sh1.073 trilioni zitatumika kutekeleza miradi ya maji kwenye miji 28 ya Tanzania, Njombe ikipata ndani ya miji mitatu.
"Bilioni 120 zitatumika kwenye miradi ya Njombe, mkandarasi tayari yupo kazini na miji itakayo pata mradi huu kwa mkoa huo ni Wanging'ombe, Makambako na Njombe," amesema Injinia Sanga.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, Sanga amesema kwa namna miradi ya maendeleo inavyo tekelezwa hawana budi kupiga magoti.
"Njooni njooni hapa wabunge wote na wenyeviti wa halmashauri za Wilaya, Sasa tupige magoto kushukuru mabilioni na mabilioni yanayoletwa," amesema.