Viongozi wa Amcos, makarani watakiwa kuzingatia weledi

Viongozi wa Amcos wakiwa wamekutana kwenye Jukwaa la Ushiriki lililofanyika wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
- Inadaiwa wapo baadhi ya viongozi wa Amcos na makarani wao wanashindwa kusimamia mazao ya wakulima na kusababisha kuibiwa
Ruangwa. Serikali imesema haitasita kumchukulia hatua kali kiongozi yeyote wa chama cha ushirika (Amcos) atakayekwenda kinyume na maadili ya ushirika.
Imesema wapo baadhi ambao tayari wamebainika wanashindwa kusimamia mazao ya wakulima na kusababisha kuibiwa hasa kwenye msimu wa ufuta.
Akizungumza leo Alhamisi Juni 6, 2024 kwenye Jukwaa la pili la ushirika linalofanyika mjini Ruangwa, Mrajisi anayesimamia vyama visivyo vya kifedha, kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Richard Zengo amesema kutokana na hilo, Serikali haitamfumbia macho kiongozi yeyote atakayekiuka msingi wa kazi yake hasa akibainia kuwaibia wakulima mazao yao.
Zengo amesema makarani wana wajibu wa kusimamia mazao ya wakulima, huku akiwataka kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
"Nitoe wito kwa makarani pia, hakikisheni mnasimamia mazao ya wakulima, nasema tena, Serikali haitasita kumchukulia hatua kiongozi yeyote atakayekengeuka, mkulima anapoleta mazao yake ghalani anatakiwa apate haki yake ileile aliyoileta, lakini kuna baadhi yenu mnawaibia, tukikubaini sheria itachukua mkondo wake,” amesema Zengo.
Akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa chama kikuu cha Runali kinachojumuisha wakulima wa Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale, Jahida Hassan amesema wanapoelekea msimu wa ufuta wa 2024, magunia 800,000 yameshapelekwa kwa wakulima kwa ajili ya kuhifadhia zao hilo.
“Runali tumejipanga kupokea ufuta ulio bora katika msimu huu, tayari tumepewa mizani ya kidijitali tutahakikisha ufuta unaoingia sokoni unakuwa bora ili tupate bei nzuri zaidi,” amesema Jahida.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kujitahidi kuvijenga vingi vitakavyosaidia kuuza bidhaa zilizobanguliwa badala ya ghafi kama ilivyo sasa kwenye maeneo mengi.
Mwananchi imezungumza na mkulima wa ufuta Elly Singano kutoka wilayani Liwale, amesema kutokana na elimu waliyopatiwa na maofisa ugani juu ya zao hilo, ana imani wakulima wengi wataenda kuuza ufuta ulio bora katika msimu huu.