Viongozi wa dini nchini wahubiri amani
Wanakwaya ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Azania Front, wakimba wakati wa Ibada ya mkesha wa Krismas juzi. Picha na Salim Shao
Muktasari:
- Waitaka Serikali kuwasaka watu wanaowashambulia viongozi hao kwa kuwamwagia tindikali
Viongozi wa dini katika makanisa mbalimbali nchini, wametumia Sikukuu ya Krismasi kuhubiri amani, kulaani ubinafsi huku wakiitaka Serikali kuhakikisha inawang’oa viongozi mizigo ambao ndio chanzo cha umaskini nchini.
Pia walielezea kushangazwa kwao na kuhusu kukithiri kwa uhalifu na kusababisha watu kuwa katika hofu.
Walisema hata hivyo, Serikali haichukui hatua mwafaka za kuzuia hali hiyo. Viongozi hao, wakiwemo maaskofu, mapadri na wachungaji, walitoa mahubiri hayo kwenye ibada zilizofanyika jana asubuhi na mkesha wa Krismasi.
Zanzibar wailalamikia Serikali
Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar limesema bado kuna safu ndefu ya viongozi wasiowajibika wanaohitajika kuondolewa kwenye nyadhifa zao.
Viongozi wa kanisa hilo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, walisema bila kuondolewa lengo la kupambana na umaskini nchini haliwezi kufikiwa.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Dk Augustino Shao, alisema Tanzania inashindwa kupambana na umaskini licha ya kubarikiwa kuwa na rasilimali nyingi yakiwemo madini, hifadhi za wanyama, mito na ardhi yenye rutuba.
Dk Shao alisema pamoja na Bunge la Muungano kuonyesha mfano wa kuwawajibisha mawaziri wanne kwa kushindwa kusimamia dhamana zao kiutendaji, alisisitiza kuwa safari bado ni ndefu kwa sababu kuna safu ndefu ya viongozi wasiowajibika ipasavyo.
“Nachelea kusema kuwa hali itaendelea kuwa hivyo kama wale tuliowakabidhi uongozi wa nchi si wazalendo halisi. Kiongozi makini lazima aondoe ubinafsi na kuweka masilahi ya wengi katika utendaji wake,” alisema Dk Shao.
Alisema tatizo la kutokuwajibika limejengwa na misingi ya rushwa katika ngazi mbalimbali za Serikali na haki inapokuwa bidhaa ya kununuliwa, uhai wa wanyonge uko hatarini. Alisema viongozi wa madhehebu ya dini na waumini wao wanaendelea kuishi kwa woga kutokana na matukio ya mashamabulizi ya kumwagiwa tindikali, kupigwa risasi na nyumba za ibada kuchomwa moto.
“Woga na hofu ya maisha vinaendelea kuchukua sehemu pale tunapoona vyombo vyetu vya usalama haviwajibiki ipasavyo, inawezekanaje nchi inayolindwa katika utawala wa sheria kila kukicha ishindwe kudhibiti matukio hayo,” alihoji Askofu Shao.
Huku waumini wakiwa kimya ndani ya kanisa, Askofu Shao alisema haiwezekani kwa nchi iliojizatiti kijeshi na kiusalama kama Tanzania matukio ya kutumia silaha, mauaji, uharibifu wa mali za raia na matumizi ya tindikali yakatendeka mchana wa jua kali na wakose kujulikana.
“Maovu yaliofanyika yangekuwa yametokea kwa wanajeshi, polisi au mtu wa cheo fulani cha kisiasa, kwa hakika wote wangekamatwa na vithibitisho vyote kupatikana,” alieleza Dk Shao.
Alisema utawala wa sheria Zanzibar unafanya kazi kwa kubagua watu kwa itikadi za kisiasa, imani, mahali alipotoka mtu kwa kujuana ndiyo maana si rahisi haki kupatikana katika vyombo vya sheria.
Kwa upnde wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Hafidh Michael, alisema wakati umefika kwa Watanzania kuwa na Bunge lenye matumaini linalojengwa na watu wenye uwezo wa kujenga hoja zenye masilahi kwa Watanzania.
Askofu Hafidh alisema maendeleo hayawezi kupatikana bila ya kuwa na Bunge na Baraza la Wawakilishi lenye uwezo wa kuisimamia Serikali na kujadili matatizo ya wananchi wake.
Alisema vitendo vya viongozi wa dini kuhujumiwa kwa tindikakali na kupigwa risasi ni uhalifu na uvunjaji wa haki za msingi za binadamu. Askofu wa Kanisa la TAG, Dickson Kaganga aliwataka Wakristo visiwani humo kusherehekea Sikukuu ya Krismasi kwa kujiepusha na vitendo vya ulevi na uasherati.
Askofu Kaganga alisema Serikali ya Zanzibar lazima iendelee kuwasaka na kuwachukulia hatua wale wote waliofanya matendo ya kuwamwagia tindikali viongozi wa dini.
Malasusa ahimiza upendo
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa, amewataka Watanzania kutumia Sikukuu ya Krismasi kudumisha amani.
Akizungumza katika ibada ya kuadhimisha Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Azania Front, Askofu Malasusa alisema waumini wengi wanaishi maisha yasiyompendeza Mungu na matokeo yake ni kutumbukia katika migororo na kuvuruga amani ya nchi.
Alisema wakati vitabu vitakatifu vinafundisha imani ya kweli kwa kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, jambo la kushangaza waumini hao wanakwenda kinyume na misingi ya imani yao.
“Sikukuu ya Krisimas ambayo inasherehekewa duniani kote ina lengo la kuwaunganisha watu na kudumisha amani. Sasa nasihi kuishi maisha yanayompendeza Mungu na kuhakikisha kwamba matendo yetu yanadumisha amani kwenye familia zetu, nchi yetu na dunia kwa jumla,” alishauri Askofu Malasusa.
Alisema pia, binadamu wengi wamepoteza mfumo halisi wa maisha na kujikuta wakipoteza amani ya dunia kutokana na kujiingiza katika utengenezaji wa silaha za kivita.
“Dunia sasa inatumia sehemu kubwa ya bajeti yake kununua silaha za kivita. Hali hii ingeweza kuepukika kama watu wangejikita kwenye misingi ya ujenzi wa amani na kuikataa roho kama ya Herod,” alionya.
Alisema Herod alikuwa mwanasiasa hatari aliyejitahidi kuwekeza rasilimali zake zote ili kufanikisha utawala wake dhidi ya Wayahudi.
Mapema akizungumza katika ibada ya mkesha wa Sikukuu ya Krismasi, Msaidizi wa Askofu wa Dayosis ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji George Fupe, aliwataka wananchi kudumisha amani na kutumia Sikukuu ya Krismasi kuwasamehe waliowakosea.
Askofu Fupe pia alitumia muda huo kuwataka wananchi kuwasaidia wale wasio na uwezo kadri wanavyoweza kama ambavyo mafundisho ya dini yanavyosema kuwa kusaidiana ni jambo la msingi. Katika Kanisa la Anglikanian, Matakatifu Albano Shemas Joseph Kalulu, aliwataka Watanzania kuishi kwa amani na upendo.
“Ni vyema watu tukaishi kwa amani na upendo, kwani hilo ndiyo jambo la msingi katika maisha ya binadamu,” alisema.
Paroko wa Kanisa la Kristo Mfalme, Tabata wilayani Ilala, Cyprian Kabaga alisema siku za karibuni kumezuka tabia ya watu kusubiri wenzao wakosee ndio waseme. Alisema tabia kama hiyo siyo nzuri na kwamba inaonyesha kuwa kuna kutafutana.
“Tuambiane kabla na wakati tunaona makosa yanafanyika na siyo kusubiri hadi mtu akosee,” alisema.
Alisema watu wa namna hiyo wakati mwingine hukataa kutoa msaada wa namna hiyo kwa ndugu na jamaa zao na kusahau kuwa bila ustawi maisha hakuna amani.
Chimeledya ataka uwajibikaji
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya, ameitaka Serikali kushuka chini na kuwashughulikia watendaji wote ambao ni wazembe kama ilivyofanya kwa mawaziri.
Askofu huyo, amesema iko haja pia kwa Serikali kuona ni umuhimu katika kuwahudumia watu kwa usawa hasa katika elimu kwa kuwa wote ni watoto wa Mungu.
Akiwa katika Kanisa Kuu la Dayosisi ya Mpwapwa, alisema: “Kwanza nawapongeza mawaziri wote wanne kwa kukubali kuwajibika kwa kiasi hicho, nampongeza pia Rais kwa kuridhia wawajibike lakini hawa wa ngazi ya chini inakuwaje?”
“Kusema kweli kama tutaendelea kuishia huko ngazi za juu haitasaidia, naitaka Serikali ipime kwa mapana na ijishushe chini kuwawajibisha viongozi wazembe wote kuanzia ngazi ya chini kabisa,” alisema.
Chimeledya alisema kipindi hiki ni kigumu kuliko vipindi vingine vyote, hivyo ni wakati pia ambao kila mmoja anatakiwa kuangalia familia yake kwa ukaribu kama ilivyo kwa Serikali ambayo lazima iangalie wananchi wake kwa ukaribu.
Kingine alichosisitiza ni suala la utunzaji wa mazingira ili kuiokoa Tanzania isigeuke kuwa jangwa kwani vizazi vijavyo vitawalaumu waliotangulia.
Kutoka Moshi, habari zilisema Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Martin Shao, amewataka waumini wa kanisa hilo kuyaombea mataifa yaliyopo kwenye mahangaiko ya vita.
Dk Shao alitoa kauli hiyo jana katika Kanisa Kuu la Usharika wa Moshi Mjini wakati wa ibada ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
“Wakati tukisherehea Krisimasi, wako watu wana mahangaiko makubwa… wana mfadhaiko kutokana na vita,” alisema Askofu Shao.
Askofu Shao alisema wanadamu wanapokuwa katika mahangaiko na majaribu kama ya vita, njia pekee ni kumfuata Yesu Kristo.
Padri wa Kanisa Katoliki la Kristo Mfalme, John Rowse aliwataka Wakristo nchini kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kwa furaha na kuepuka maovu.
Habari hii imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Fariji Msonsa, Ibrahim Yamola, Idan Mhando, Fariji Msonsa, Habel Chidawali na Joseph Zablon.