Viongozi wa dini wadai watu wamepoteza imani
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa viongozi wa dini wanapaswa kutoa mafundisho mema yenye kujenga kuhusu misingi ya maadili na umuhimu wa kuyafuata kwa faida ya vizazi vijavyo.
Mwanza. Baadhi ya viongozi wa dini wametahadharisha kupoteza nguvu na ushawishi wa imani katika jamii, kwa kile walichodai watu wanaongozwa na misimamo ya vyama, makabila, masilahi binafsi, makundi na mitandao yao.
Hayo yamesemwa jana Jumamosi Juni 22, 2024, kwenye kongamano la kujadili umuhimu wa dini katika kusimamia maadili na amani ya jamii nchini, lililofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) jijini Mwanza.
Viongozi hao wamependekeza kuundwe baraza la dini la kitaifa litakaloshughulikia na kuhoji dini zinazopotosha waumini badala ya kuwajaza maarifa sahihi.
Akimuwakilisha Sheikh wa Mkoa wa Mwanza wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Hassan Kabeke, Sheikh Fadhili Salum amesema watu wengi wanaishi kwa hofu duniani kwa sababu wamekiuka maagizo ya Mwenyezi Mungu. Amesema ili kuwa na amani duniani, ni lazima kurejea katika maandiko matakatifu ya Quran na Biblia.
“Kama tunataka tuwe na amani katika dunia yetu ni kurudi katika mfumo ambao ni kitabu kitakatifu ambacho ni Quran… kwenye maandiko matakatifu kinasema atakayepuuza maandiko matakatifu ataishi maisha ya hofu, huzuni na dhiki,” amesema Sheikh Fadhili.
Amesema mambo aliyokataza Mungu ndiyo yanayofanywa katika jamii hivi sasa huku yale aliyoelekeza kufanywa, yakipuuzwa.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema dini ambayo ni chanzo cha maadili, imepoteza ushawishi miongoni mwa watu na haitegemewi sana na wafanya uamuzi katika jamii.
Amesema watu wengi wanazungumza kuhusu ushawishi mkubwa wa viongozi wa dini, lakini ukweli ni kwamba, dini imepoteza ushawishi wake.
“Dini imepoteza nguvu na ushawishi katika jamii japo ukiwasikiliza watu wanatuzungumza sana viongozi wa dini kwamba tunaushawishi mkubwa sana, wengine wanasema watu wengi wanawasikiliza, hapana wanatudanganya kwa sababu dini imepoteza ushawishi katika jamii,” amesema Bagonza.
Amesema siasa ndiyo kiini cha uamuzi unaotuongoza kila siku na watu wengi wanaongozwa na misimamo ya vyama, makabila, masilahi binafsi, makundi na mitandao kuliko dini zao.
Askofu Bagonza amesema imekuwa kawaida kwa viongozi wa dini kuhojiwa wanapozungumzia mambo ya Serikali na siasa nchini, wakidaiwa kuchanganya dini na siasa.
Hata hivyo, amesema viongozi wa Serikali na siasa wanapozungumzia dini au kujihusisha na mambo ya dini hawahojiwi.
Amesema anakubaliana na Serikali kutokuwa na dini na anakubaliana na viongozi wa dini kutokuwa na itikadi za vyama vya kisiasa, ingawa kila raia ana haki ya kutoa maoni ya kisiasa.
Dk Bagonza amesema viongozi wengi wa umma wamejichanganya, wanakuwa waumini wakiwa kwenye nyumba za ibada lakini wakiwa mitaani wanakuwa watu tofauti.
Hivyo, amewataka kuiga mfano wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyependa na kujitahidi kuwa mtu mmoja hadharani na kwenye faragha.
“Uaminifu kwa Mwalimu ilikuwa ni dhambi ya kutoiba wakati huna cha kuiba. Kuna watu hapa ni waaminifu kwa sababu hawana cha kuiba, wakipata cha kuiba utawashangaa,” amesema.
Amesema hali ilivyo hivi sasa, hata viongozi wa dini wanashikwa kigugumizi cha kukemea rushwa na hata serikalini hakuna wakusimama na kukemea rushwa.
Wimbi la dini zisizofaa
Askofu huyo ameitahadharisha jamii kuhusu kuibuka kwa dini zinazonyonya waumini na kuhamasisha vitendo viovu, ikiwamo ushirikina na kupata utajiri bila kufanya kazi.
“Eti kidole cha albino kikufanye wewe kuwa tajiri bila kufanya kazi? Kidole cha albino kiwafanye watu wote wakupigie kura hata kama kichwani hapana kitu?” amehoji Dk Bagonza. Amesema dini za aina hiyo zinatengeneza wafuasi wa viongozi badala ya wafuasi wa Mungu.
Amesema kisiasa na kijamii, dini zisizowajibika hazina tofauti na bangi ya kuwalewesha watu ili wakabidhi hatma yao mikononi mwa viongozi wa kidini na kisiasa.
Mkuu wa Chuo cha Biblia cha Kilutheri Nyakato jijini Mwanza, Mimii Mziray amesema chuo hicho kimefanya utafiti wa awali kuona ni kwa nini mafundisho potofu yanavuma na yana mvuto mkubwa kwa watu wengi.
Amesema umebaini sababu za kisaikolojia na kiuchumi kuwa miongoni mwa visababishi.
“Jambo la kwanza ni sababu za kisaikolojia na kijamii, sababu za kiuchumi kutokana na hali duni ya maisha inasababisha watu kuvutiwa na mafundisho potofu. Sababu nyingine ni ya kidini na kiimani na sababu ya mwisho ni ya kichungaji,” amesema.
Amesema tayari wameanzisha programu ya kutafuta suluhu ya janga hilo yenye lengo la kuwa na ithibati ya maadili ya uenezaji wa injili kwa kushirikiana na chuo cha Saut.
Mfalme kutoka imani ya Rastafarihai, Bagaile Valerian amesema maisha siyo magumu kama watu wanavyosema.
“Kila binadamu amezaliwa na utu, mtu na mtu, utu na roho. Muumbaji alivyokuumba aliweka hazina sita; maisha, amani, imani, subira, hekima na akili,” amesema.
Ameitaka jamii kuacha kudharauliana, kula rushwa, wala kufanyiana mabaya. Alidai kuwa endapo watafanya hivyo, hakutakuwa na magereza na yaliyopo yatageuka kuwa vyuo vikuu.
Viongozi serikalini wakubali kukosolewa
Askofu Bagonza amesema uvumilivu wa maoni tofauti kwa viongozi wa umma unaonekana kuwa mdogo huku akiwataka kukubali kukosolewa bila kuchagua maneno na namna wakosoaji watakavyowakosoa.
Amedai hata kiwango cha kusikiliza kipo chini kwa kuwa hakuna maadili ya kujenga jukwaa imara la maridhiano katika jamii kwa kuamini yanaletwa na fedha na madaraka.
“Tunaamini mno fedha na madaraka katika kuleta maridhiano. Kiwango chetu cha kusikilizana kipo chini mno. Hatuchelewi kuchomoa sime pale mjadala unapokuwa na joto kali, kwa hiyo tunahitaji kufanyia kazi eneo hili,” amesema Bagonza.
Amesema maridhiano ni jadi ya Watanzania ndiyo maana hata uhuru ulipatikana bila kumwaga damu.
Awali, akifungua kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Saut, Profesa Costa Mahalu amesema jukumu la dini katika kudumisha maadili na amani ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote.
Amesema hivi sasa watu wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya migogoro, umasikini na ukosefu wa usawa.
“Dini inaweza kuhamasisha umoja na maelewano katikati ya makabila mbalimbali. Viongozi wa dini wanaweza kutumika kuhamasisha amani na kutatua migogoro katika jamii. Dini inatoa huduma za kijamii kama elimu, afya na msaada kwa masikini na wanyonge. Dini inaweza kuhamasisha maendeleo katika jamii kupitia ujasiriamali, na katika hilo niseme dini inatoa huduma kwa watu wote bila kubagua mtu,” amesema Profesa Mahalu.