Viongozi wa dini watakiwa kuhimiza wapiga kura
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza leo Alhamisi Septemba 28, 2023 katika Baraza la Maulid kitaifa alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Muktasari:
- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Maulid, huku akiwaomba viongozi wa dini kusaidia kuhamasisha wapiga kura wengi kujitokeza kwenye chaguzi.
Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao kujitokeza kwa wingi kupiga kura wakati wa chaguzi nchini ili kutimiza haki yao ya kuchagua viongozi.
Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 28, 2023 katika Baraza la Maulid kitaifa alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye baraza hilo.
Amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inayo utaratibu wa kuendesha shughuli ya uchaguzi na wakati utakapofika itaanza kwa kutoa matangazo ili taasisi zote zikiwemo za kidini zile ambazo zina sifa ziweze kuomba na kupata kibali cha kutoa elimu kwa mpiga kura.
Amewataka viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kuendelea kuwa watulivu na kujitokeza kwa wingi katika michakato yote inayoendelea ya uchaguzi ili watimize haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wao.
“Lakini tutakuwa na mazoezi ya awali ambayo tutawaomba sana viongozi wa dini wawahamishe watu wetu kabla hata ya uchaguzi wa mwaka ujao wa kuchagua wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutakuwa na zoezi la maboresho la daftari la mpiga kura,” amesema.
Amesema Serikali inawategemea viongozi kuhamasisha waumini wote kwenda kuhakiki uwepo wa majina yao katika daftari la mpiga kura lakini baada ya hapo watashiri katika kutoa elimu kwa watanzania waweze kujitokeza kupiga kura.
“Kauli yenu ina nguvu sana, kauli yenu inasikilizwa sana kauli yenu inajenga matumaini kwa walio wengi. Tunaendelea kuwashukuru na kuwasihi sana waumini waendelee kusikiliza viongozi wa dini na wananchi waendelee kushiriki katika hatua zote za kabla ya uchaguzi ujao,”amesema.
Amesema hayo wakiyatimiza kwa pamoja watapata mafanikio nchini.
Kuhusu rushwa na matumizi mabaya ya watu waliopata mamlaka, Majaliwa amesema kuwa wataendelea kuchukua hatua kwa wala rushwa na wenye kutumia mamlaka yao vibaya na kwamba hilo ndilo litakalofanya litawafanya watanzania waweze kushiriki kikamilifu.
Kuhusu ombi la Bakwata la msamaha wa ada ya visima vinavyochimbwa katika misikiti, Majaliwa amesema wamelipokea na kumtaka Katibu Mkuu wa baraza hilo kuiandikia Serikali barua ili kuona ni maeneo gani yanayoombwa.