Ubunge Mbarali moto, Zitto ampa Kilufi

Wananchi Kata ya Ubaruku wilayani Mbarali mkoani Mbeya wakiwa katika mkutano wa kampeni za mgombea ubunge wa chama cha ACT Wazalendo, Modestus Kilufi

What you need to know:

  • Uchaguzi mdogo jimbo la Mbarali unatarajia kufanyika Jumanne, Septemba 19 kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Francis Mtega aliyefariki kwa ajali.

Mbeya. Zikiwa zimebaki siku mbili kufanyika uchaguzi mdogo jimbo la Mbarali, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewaomba wananchi wilayani Mbarali kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi huo na kumpigia kura mgombea, Modestus Kilufi.

ACT Wazalendo inaendelea na kampeni zake katika maeneo mbalimbali kuomba kura, uchaguzi ambao unatarajia kufanyika Septemba 19 kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Francis Mtega kufariki dunia kwa ajali ya kugongwa na trekta, Julai Mosi.

Akizungumza kwa simu wakati wa mkutano wa kampeni za chama hicho katika Kata ya Ubaruku, Zitto amesema Mbarali haijapata mtu sahihi wa kuitetea hivyo, Kilufi ndiye mtu pekee mwenye maono na huruma ya kutetea maslahi ya wananchi.

Amesema mgombea huyo aliwahi kufanya naye kazi katika moja ya kamati akiwa bungeni, ambapo aliridhishwa na uwajibikaji wake akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi huo na kumpigia kura.

“Mbarali kwanza, vyama baadae, nawapongeza kwa muitikio mkubwa kumuunga mkono mgombea wetu Kilufi, huyu ndiye mtu sahihi kutusemea na kutatua changamoto zetu, namfahamu vizuri ni mtu makini, muadilifu na mchapa kazi,”

“Kwa muda mrefu hatujapa mtu sahihi hapa Mbarali, niwaombe siku ya uchaguzi mjitokeze kwa wingi na kumpigia kura za kishindo ili aweze kutetea maslahi yenu na Taifa kwa ujumla,” amesema Zitto huku akishangiliwa na wananchi.

Kwa upande wake mgombea ubunge, Kilufi amesema Mbarali inazo changamoto nyingi ikiwamo migogoro ya ardhi, ukosefu huduma za kijamii ikiwamo maji, umeme, elimu na afya.

Amesema anaamini kwa uzoefu alionao kwenye uongozi, ameamua kurejesha tena jina lake kuhakikisha anawatumikia wananchi ambao wamemuomba kuwania kinyang’anyiro hicho.

“Niwashukuru wananchi kwa kuniamini kuniomba nigombee nafasi hii, binafsi nimejipanga na sitawaangusha mtakaponichagua kuwaongoza, kero ni nyingi na wa kuzimaliza kwa uwezo wa Mungu ni mimi,”

“Migogoro ya ardhi, umeme, elimu na afya ndio vipaumbele vyangu kuhakikisha wananchi mnaondokana na changamoto hizi, CCM kwa muda mrefu wameshindwa sasa acha tuingie kazini kuwanusuru,” amesema mgombea huyo aliyewahi kuwa mbunge mwaka 2010 hadi 2015.