Viongozi wa nchi 17 wamuaga Magufuli

New Content Item (1)
Viongozi wa nchi 17 wamuaga Magufuli

Muktasari:

  • Viongozi kutoka nchi 17 duniani wamehudhuria ibada ya kitaifa ya kumuaga wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli inayofanyika jijini Dodoma leo Jumatatu Machi 22, 2021 katika uwanja wa Uhuru.

Dar es Salaam. Viongozi kutoka nchi 17 duniani wamehudhuria ibada ya kitaifa ya kumuaga wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli inayofanyika jijini Dodoma leo Jumatatu Machi 22, 2021 katika uwanja wa Uhuru.

Akizungumza leo uwanjani hapo waziri mkuu, Kassim Majaliwa amesema ujio wa viongozi hao umelifariji Taifa na kuonyesha ni jinsi gani Magufuli alipendwa.

“Orodha kubwa ya viongozi kutoka nchi 17 wamekuja kutufariji, kwa kukimbiliwa na majirani zetu tunashukuru sana Tanzania ni nchi rafiki na jirani, tunawapenda na kupata marais tisa, makamu wa marais wawili kutoka nchi zao si jambo dogo, wawakilishi wa marais na wa nchi karibu zote zinazowakilishwa Tanzania tunashukuru sana,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kuishi katika ujasiri wake uliojaa maono na mapenzi katika kipindi chote cha uongozi wake.

“Wote tulitamani kuwa naye lakini kifo ni jambo lisilozoeleka, hivyo hatuna budi kukubali na jina lake lihimidiwe kwani yote ni mapenzi yake Mungu, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, tuungane na tuendelee kushirikiana, kustamihilia na kuzidisha upenzi na umoja na mshikamano kati yetu tuendelee kumuombea Mungu ampumzishe kwa amani,” amesema Majaliwa.