Viongozi, wanachama Chadema waachiwa kwa dhamana

Tuesday October 05 2021
chademapicc
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Makada wanane wa Chadema waliokuwa washikiliwa na polisi kwa tuhuma za kupanga njama za kufanya mkusanyiko isiyo halali  wameachiliwa kwa dhamana na jeshi hilo.

Kati yao wapo viongozi wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha)  Kanda ya Pwani ya chama hicho. Walikamatwa Oktoba 2, 2021  katika viwanja vya Tanganyika Packers.

Hata hivyo, jana Jumatatu Oktoba 4,2021 ofisa habari wa chama hicho Kanda ya Pwani, Gervas Lyenda amesema viongozi hao walikamatwa wakiwa katika utaratibu wa kufanya mazoezi ‘joging’.

Soma zaidi: Chadema yadai kada wake anashikiliwa na Polisi Zanzibar

Leo Jumanne,  Lyenda ameieleza Mwananchi Digital  kuwa viongozi wao pamoja na mwandishi wa habari wa mtandao wa Mgawe TV, Harold Shemsanga wameachiwa kwa dhamana.

“Wameachiwa jana jioni wote waliokamatwa, leo wameambiwa wakachukua simu zao,” amesema Lyenda.

Advertisement

Waliokuwa wamekamatwa ambao sasa wameachiwa kwa dhamana ni Lilian Kimei ambaye ni  katibu uenezi wa Chadema  Kanda ya Pwani, Rose Moshi (Katibu wa Chadema Kinondoni), Hadija Mbaga, Rosi Masiyanga, Levina Lufyagila, Vaileti Seka wote Bawacha.Wengine ni Mwenyekiti wa Chadema Kawe, Leonard Manyama na Ernest Mgawe.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro wafauasi hao walikamatwa kwa kupanga njama za kufanya mkusanyiko usio halali kwa malengo ya kujenga taharuki na uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Advertisement