Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi wanane Chadema Mwanza, wengine 15 wapandishwa kizimbani

Washtakiwa 23 wanaoshtakiwa katika kesi mbili tofauti zenye kosa moja la kujihusisha na mikutano au mazungumzo yanayoweza kupelekea ugaidi wakifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obadi, kati ya watuhumiwa hao 23, wanane ni viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia matawi na kata, ambapo Nyamagana ina viongozi wanne na Ilemela wanne.

Mwanza. Washtakiwa 23 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza wakishtakiwa katika kesi mbili tofauti zenye kosa moja la kujihusisha na mikutano au mazungumzo yanayoweza kupelekea ugaidi.

Baadhi ya washtakiwa hao ni viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo kesi hizo mbili zimesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza na Naibu Msajili, Erick Marley.

Katika kesi ya kwanza namba 16379/2026, washtakiwa 13 kutoka Wilaya ya Ilemela wanatuhumiwa kufanya kosa hilo kati ya Juni 25 na Julai 7, 2026.

Washtakiwa hao ni Alphaxadi Nyamwaga, Fantson Mpango, Abely Mwesa, Hassan Said, Emanuel Wambura, Adam Idd, Damas Sadock, Petro Mabula, Abdul Kagwidi, Devid Mashaka, Philipo Masatu, Edward Mikindo na Emmanuel Doto.

Kesi ya pili namba 16375/2026 imewahusisha washtakiwa 10 kutoka Wilaya ya Nyamagana ambao pia wanatuhumiwa kufanya mikutano hiyo kati ya Julai 4 na Julai 7, 2026, katika eneo la Igoma.

Washtakiwa hao ni Deus Masalago, Mohamed Tosha, Fabian Nguvumali, Samweli Mtani, Samweli Kobell, Julius Makonga, Fanuel Lutana, Philipp Kulwa, Philipp Shipuluko na Hamis Mnyimvua.

Washtakiwa hao 23 wanatuhumiwa kufanya vikao hivyo kwa lengo la kupanga vitendo vya ugaidi, ikiwemo kuchoma majengo ya Serikali na ya watu binafsi.

Hata hivyo, watuhumiwa wamerudishwa rumande baada ya Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, ambayo imepangwa kutajwa tena Agosti 6, 2026.

Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa upande wa utetezi, Erick Mutta amesema watuhumiwa hao walishikiliwa kwa takribani mwezi mmoja kabla ya kufikishwa mahakamani.

"Jumla ya washtakiwa 23, wakiwemo viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamefikishwa mahakamani na kushtakiwa katika kesi mbili tofauti, lakini kwa ujumla wakikabiliwa na kosa moja la kujihusisha na mikutano, vikao au mazungumzo yanayoweza kupelekea ugaidi.

"Wakiwa na lengo, katikati ya mashtaka imeelezwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Juni 25 na Julai 6, 2026, watu hao 23 walifanya vikao vya kupanga kufanya vitendo vya kigaidi, ikiwemo kuchoma au kulipua majengo ya Serikali na ya watu binafsi," amesema Mutta.

Aliongeza, "Washtakiwa hao hawakuweza kudhaminiwa kutokana na mashtaka hayo kusikilizwa na Mahakama Kuu, na Mahakama hii haina mamlaka ya kuyasikiliza, hivyo wamerudishwa rumande."

Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obadi, kati ya watuhumiwa hao 23, wanane ni viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia matawi na kata, ambapo Nyamagana ina viongozi wanne na Ilemela wanne.