Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viporo miradi ya maji vyawaibua wabunge

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza bungeni Jumanne Mei 5, 2026 wakati akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake.

Muktasari:

  • Ni baada ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso kuwasilisha bajeti ya wizara hiyo ya Sh1.12 trilioni, akisema miradi 993 inatekelezwa.


Dodoma. Wabunge wameibua hoja ya miradi viporo katika Wizara ya Maji wakitaja kutopeleka fedha kumewakimbiza wakandarasi.

Wabunge hao wameibua hoja ya miradi isiyokamilika leo Jumatano, Mei 6, 2026 wakati wakichangia hotuba ya Wizara ya Maji 2026/27, mmoja wao akitaka Waziri Jumaa Aweso pamoja na bajeti yake wafanyiwe maombi.

Jana Jumanne, Waziri Aweso aliwasilisha bajeti ya wizara hiyo ya Sh1.12 trilioni, akitaja vipaumbele sana.

Katika bajeti hiyo, asilimia 93 ni fedha zinazokwenda kwenye miradi ya maendeleo ambapo asilimia 7 kwenye matumizi ya kawaida.

Mbunge wa Monduli (CCM), Isack Joseph amesema dhana ya kumtua ndoo mwanamke kichwani haiwezi kutimia ikiwa miradi viporo haitakamilika.

Joseph amesema katika Jimbo la Monduli hali ni mbaya kwa kuwa wapo katika ukanda wa ukame lakini akasema miradi iliyoanzishwa kama ingekamilika, itaongeza kiwango cha maji katika jimbo hilo.

“Waziri Aweso, mimi naomba kwangu ulete fedha kukamilisha miradi viporo, vipaumbele vyako viwe kukamilisha miradi ya zamani, siyo kwenda na mipango na miradi mipya wakati ya zamani haitakamilika,” amesema Joseph.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, fedha zinapotengwa ni lazima kutazama wapi hapajakaa sawa kuliko kuanzisha mambo mapya ambayo hayafiki mwisho.

Mbunge wa Msalala (CCM), Johnson Magangila amesema kumtua mwanamke ndoo kichwani ni kuhakikisha miradi ya maji viporo inakamilishwa nchi nzima, hoja ambayo imeungwa mkono na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Adonis Bitegeko ambaye ameomba wizara hiyo kupanua wigo wa miradi kwa kuishirikisha sekta binafsi.

Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Mwantumu Zodo ametaja sababu za kutokamilika kwa miradi mingi kwamba inatokana na Serikali kutopeleka fedha za miradi.

Zodo ameitaka Serikali kuwalipa makandarasi wanaojenga miradi ya maji ili warudi saiti kunusuru miradi kwa kuwa imekwama kwa kuwa wameondoka.

Hoja ya Wakandarasi kukimbia miradi imeibuliwa pia na Mbunge wa Itwangi (CCM), Azza Hillali akieleza kuwa miradi iliyokwama ni lazima ipelekewe fedha ili wakandarasi waendelee na kazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola amesema kwa hali ilivyo, inabidi Waziri wa Maji na bajeti yake waombewe.

"Mheshimiwa mwenyekiti, sijui kama kanuni zinaruhusu, nilitaka nije hapo mbele ili waziri asimame na hotuba yake nimuombee, naamini Mungu anaweza kujibu," amesema Lugola.

Sababu za kuombea hotuba hiyo amesema inatokana na hali ilivyo ndani ya wizara kwani anaona vipo vijiji katika jimbo lake vinapakana karibu na Ziwa Victoria kwa umbali wa kilomita mbili lakini havina maji.

Lugola ameshauri uwepo utaratibu wa kutafuta fedha kwa namna yoyote ili kumalizia miradi ya zamani ikiendana na mahitaji halisi.

Mbunge wa Busega, Simon Lusengekile amesema, fedha zilizoidhinishwa na Bunge zinapaswa kupelekwa kwa wingi na wakati kwa ajili ya kutekeleza miradi na wizara iweke mipango ya muda mrefu ya miaka 20 au 30 kwa ajili ya kuwa na uhakika wa maji nchini.

Naye Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde amependekeza wakati wa kujenga miradi ya maji, Serikali itumie matokeo ya sensa na kutazama ukuaji miji, vijiji na ongezeko la watu.

Lusinde amesema vitabu vya Sensa vikiwaongoza wataalamu itakuwa na maana nzuri, kuliko wanavyojenga miradi lakini katika kipindi kifupi maji yanakuwa hayatoshelezi.