VITA VYA KAGERA: Nyerere, Samora wakubaliana kumpiga Idi Amin-5

Muktasari:

Jana tuliona jinsi majeshi ya Tanzania yalivyoanza safari ya kwenda mpakani kukabiliana na majeshi ya Idi Amin wa Uganda, uhamasishaji wa taasisi na watu wengine kutoa magari yao ili yasaidie kusomba wanajeshi na kitendo cha Rais Julius Nyerere kulitangazia taifa kuhusu uvamizi na uamuzi wa kupambana nao na baadaye kuchukua ndege kwenda Beira, Msumbiji.

Muda mfupi baada ya Rais Julius Nyerere kulitangazia Taifa jijini Dar es Salaam kuhusu uvamizi wa Idi Amin na uamuzi wa Tanzania kumpiga, Alhamisi ya Novemba 2, 1978, alipanda ndege kwenda Beira, Msumbiji kwenye mkutano na mwenyeji wake, Rais Samora Machel.

Ilikuwa aahirishe safari hiyo lakini alilazimika kwenda kwa sababu alikuwa mwenyekiti wa Nchi za Mstari wa Mbele (FLS) katika ukombozi. Nchi nyingine ni Angola, Botswana, Msumbiji, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Wakati huo pia kulikuwa na mgogoro wa mpaka kati ya Zambia na Zimbabwe (zamani Rhodesia) uliosababishwa na Rais Kenneth Kaunda wa Zambia. Nyerere ndiye aliyekuwa ameitisha mkutano wa kushughulikia mgogoro huo.

Kaunda alikuwa amefungua mpaka wake na Zimbabwe, jambo lililomkera sana Nyerere na Samora.

Nchini Rhodesia, mwanasiasa aliyeitwa Ndabaningi Sithole, ambaye ni mwanzilishi wa chama cha Zimbabwe African National Union (Zanu) kabla ya kuangushwa na Robert Mugabe, alikuwa mshirika wa karibu sana wa Idi Amin.

Kwa hiyo kufunguliwa kwa mpaka huo kulimfadhaisha Mwalimu Nyerere, hasa wakati huo ambao tayari alikuwa na mgogoro na Uganda. Kwa namna fulani Rhodesia ilikuwa na uhusiano wa kijeshi na utawala wa Idi Amin wa Uganda.

Katika ukurasa wa 114 wa kitabu chake cha For the Sake of Argument: Essays and Minority Reports, mwandishi Christopher Hitchens anasema wakati fulani “akiwa ofisini, (Sithole) aliomba msaada wa Idi Amin wa kuunda jeshi lake binafsi”.

Jumatatu ya Julai 17, 1978, ikiwa ni miezi minne kabla ya kuzuka kwa Vita vya Uganda, jarida la Facts and Reports (volume 8), katika habari iliyoandikwa na David Martin iliyokuwa na kichwa kilichosomeka “Sithole Guerrillas Fly to Amin for Training”, kulikuwa na tuhuma za uhusiano huo wa kijeshi.

“Dikteta Idi Amin ameshutumiwa vikali kwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa maelfu ya vijana wa washirika wa Ian Smith (wa Rhodesia) kwa madhumuni ya kuwatumia kuvuruga harakati za ukombozi nchini Zimbabwe,” aliandika mwandishi huyo.

Jarida jingine la International Bulletin (volume 4) la Julai 1978, lilizungumzia suala hilo.

“Mshirika mweusi wa Ian Smith, Mchungaji Ndabaningi Sithole anafundisha jeshi lake binafsi nchini Uganda,” liliandika jarida hilo. Pia, jarida la Africa Research Bulletin’ likaripoti kuwa “Mchungaji Ndabaningi Sithole amepokea idadi kubwa ya wapiganaji kutoka Uganda kwa Idi Amin pamoja na vifaa vya mafunzo”.

Zilikuwapo pia habari kwamba ndege za Rhodesia zilikuwa zikitua katika viwanja vya ndege vya Uganda—Entebbe na Nakosongola.

Habari hizo na nyinginezo za ushirika wa Idi Amin na Sithole, zikijumlishwa na ile ya Zambia kufungua mpaka wake na Rhodesia, zilimfanya Mwalimu Nyerere kwenda Beira, Msumbiji, kujadili jambo hilo haraka kadri ilivyowezekana.

Nyerere na Samora walikutana jioni ya Novemba 2, 1978 kujadili jambo hilo na kuridhika kuwa Idi Amin alitumiwa na mataifa mengine kuivamia Tanzania kwa lengo la kumuondoa Nyerere katika harakati zake za ukombozi wa Zimbabwe dhidi ya akina Ian Smith na mshirika wake, Mchungaji Ndabaningi Sithole, na kwamba huenda Uingereza ilikuwa nyuma ya mpango huo.

Baadhi ya wanazuoni wanaamini kuwa halikuwa jambo la bahati mbaya kwamba vita vya Kagera kuzuka wakati huo muhimu wa mazungumzo kati ya vikosi vya ukombozi na serikali ya wachache ya Ian Smith nchini Zimbabwe.

Walisema wapinzani wa ukombozi walitaka kudhoofisha jitihada za Mwalimu Nyerere “kwa gharama zozote”.

Baada ya kutafakari yote hayo, Nyerere alimhakikishia Samora kwamba Tanzania ingeweza kupambana na Idi Amin bila kupoteza lengo lake la harakati za ukombozi wa Zimbabwe.

Walikubaliana kuwa kikosi cha jeshi la Tanzania kilichokuwa katika mpaka wa Msumbiji na Rhodesia kirejee Tanzania na, zaidi ya hilo, Samora naye akaahidi kutoa kikosi chake kuja kusaidiana na Tanzania.

Ndani ya siku chache, wanajeshi wa Msumbiji wakawa wamewasili Kagera tayari kwa mapigano. Hakuna chombo chochote cha habari cha Tanzania kilichoandika taarifa zozote za wapiganaji wa Msumbiji kuwasili Kagera.

Hata hivyo, kitabu cha War in Uganda cha Tony Avirgan na ‎Martha Honey kinasema “ushahidi mdogo sana kwamba wapiganaji wa Msumbiji walikuwa Tanzania ni nakala ya gazeti Noticias iliyoachwa kwenye ukumbi wa mapumziko wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza.”

Waandishi wa kitabu hicho, ambao walikuwa uwanja wa vita, wamesema mbali na wapiganaji hao 800 kutoka Msumbiji, hakukuwa na wapiganaji wengine kutoka taifa jingine lolote duniani waliokuwa wakipigana bega kwa bega na wapiganaji wa Tanzania dhidi ya majeshi ya Idi Amin.

Katika lile juma la pili la Novemba 1978, pamoja na magumu yote waliyokumbana nayo kama mvua, Tanzania iliweza kuwaandaa vyema wapiganaji wake.

Juma hilo ndipo alipowasili Meja Jenerali Tumainieli Kiwelu kuongoza mapambano. Pamoja na kwamba Tanzania ilisikitishwa sana na kuvunjwa kwa daraja la Mto Kagera, ilipata nafasi ya kufanya maandalizi ya kutosha bila hofu ya kuvamiwa na majeshi ya Idi Amin ambayo yangeweza kulitumia daraja hilo kushambulia upande wa pili.

Itaendelea kesho