Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vitendo vya unyanyasaji vimemsababishia Marry ulemavu wa kudumu

Muktasari:

  • Matukio ya ukatili dhidi ya wanawake kwenye jamii ni kama zimwi ambalo limekuwa likiitesa jamii kwa miaka mingi bila kupatiwa mwarobaini, hivyo ndivyo unavyoweza kusema.


Kilimanjaro. Matukio ya ukatili dhidi ya wanawake kwenye jamii ni kama zimwi ambalo limekuwa likiitesa jamii kwa miaka mingi bila kupatiwa mwarobaini, hivyo ndivyo unavyoweza kusema.

Mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya mikoa ambayo jamii yake imeelimika kwa kiasi kikubwa, licha ya kuwepo matukio ya ukatili kwenye jamii, yapo matukio ambayo yamekuwa ni sugu kwenye baadhi ya familia ikiwemo vipigo na mauaji dhidi ya wanawake.

Mwandishi wa makala haya alikutana na mmoja wa wanawake ambao wamefanyiwa ukatili na mumewe hali ambayo imemrudisha nyuma kimaendeleo pamoja na kumsababishia ulemavu wa kudumu ambao unatokana na msongo wa mawazo.

Marry Ushaki Mkazi wa Mkuu, Wilaya ya Rombo mkoani humo anaeleza namna vipigo na manyanyaso kwa mume wake vilivyomsababishia ulemavu baada ya kupata kiharusi mara tatu mwaka 2014.

Anasema muda mchache baada ya kuolewa na kufanikiwa kupata watoto, mumewe alianza ukorofi ambapo kila akirudi nyumbani jioni akiwa amelewa alikuwa akiambulia vipigo hali ambayo ilimtesa kwa muda mrefu kwenye ndoa yake.

Anasema ilikuwa sio jambo jepesi kwake na watoto wake kwani mumewe huyo alifika mahali hatoi matumizi ya nyumbani na kumwachia majukumu peke yake hali ambayo ilimfanya ataabike kwa muda mrefu kwani ni kitu ambacho hakutazamia kutokea katika maisha yake.

Anasema baada ya kupitia changamoto hiyo ya manyanyaso alilazimika kujitenga chumba na mumewe akawa analala chumba chake na yeye cha kwake kutokana na vipigo alivyokuwa akivipata.

“Ilifika mahali nikaondoka kwenye familia ile nikaenda kwa ndugu zangu na baadaye niliamua kujiongeza kujitafutia riziki maana watoto wangu bado walikuwa ni wadogo, nilipambana nikapata mtaji kidogo nikaanza ujasiriamali,”

“Baadaye huyu mwanaume akajua ninapoishi akanifuata kwa sababu alikuwa ni baba watoto wangu na kwa vile niliondoka nilijua tayari ameshajifunza na kujirekesbisha, baada ya muda kidogo mwendo ukawa ni ule ule wa vipigo,”

“Ilifika mahali hata kipato nilichokuwa ninakipata kwenye shughuli zangu za ujasiriamali alikuwa anachukua kwenda kunywa nazo pombe wakati hajui familia ilikuwa inaishi katika mazingira magumu,”

“Niliendelea kuteseka sana huku nikiwa na msongo mkubwa wa mawazo ambapo baadaye ilinipeleka kuwa na tatizo la shinikizo la damu ambapo baadaye nilipata kiharusi ambacho kimeniletea shida mpaka sasa,”

“Nakumbuka mwaka 2019 amani iliondoka kabisa ndani ya nyumba tukawa hatuelewani lakini mateso na manyanyaso nikawa naendelea kuishi nayo kama kawaida na ni uvumilivu ulinifanya niendelee kuishi naye maana nilikuwa nawaza nikiondoka watoto wangu wataishije,”

“Na huyu mwanaume nimeishi naye tangu mwaka 1981 na hakuna hata siku moja niliyoiona ina unafuu katika maisha yangu ya ndoa mimi na yeye maana alikuwa ni mtu mkatili sana, niliendelea kuishi naye hivyo hivyo baadaye nikapata kiharusi kwa mara ya pili na mpaka sasa naishi kwa kutumia dawa na umri umeshasogea,”

“Nakumbuka kuna kipindi mwaka 2016 alinipiga na kuning’atang’ata mgongoni bila sababu na alikuwa akifanya hivyo akishakunywa pombe nilitafuta wasaidizi wa kisheria ambao walinisaidia kwa kiasi kikubwa tukawa tumempeleka dawati la jinsia kila alichokuwa ana ulizwa alikuwa akikana kuwa hajafanya hivyo,”

“Kutokana na mateso yale nilitaka anipe talaka yangu nilienda ustawi wa jamii haikutosha, ikabidi niende kwa kiongozi wa imani akaambiwa aombe msamaha lakini akakataa na akasema hataomba msamaha,”

“Ikabidi tutenganishwe kwa muda ili aweze kujirekebisha ilichukua miaka miwili na miezi miwili ndipo alinirudisha mwaka 2019 tukaishi hivyo hivyo kwa shida niliporudi nyumbani nilikuwa naumwa nikaendelea kujihudumia mwenyewe,”

“Kwa hiyo maisha yangu niliishi kwa kutukanwa na pigwa ,kufungiwa nje na wakati mwingine kufukuzwa na kupata kashafa za kila aina. Kuna wakati nikiwa nafanya biashara zangu nikipata fedha kidogo anazichukua kwa nguvu kwa hiyo nabaki sina fedha hata ya kuwanunulia wanangu chakula, kwa kweli maisha yaliendelea kuwa magumu mno,”

Hatua

“Nililalamika na kumpeleka kwenye vyombo vya sheria lakini tabia ile haikukoma niliendelea kuishi naye kwa mateso makubwa huku nikiumia moyoni namna ninavyopata mateso na watoto wangu wakati yeye hana habari yoyote, hawazi watoto wake wanakula nini na wanaishije na wala wanasomaje kwa hiyo nikawa napamabana nao wenyewe,”

“Mpaka watoto wangu wanakuwa wakubwa hajawahi kujua kwamba wanaishije wanasomaje, changamoto zilikuwa ni nyingi hata hapa nilipofika ni kwa neema tuu maana nilikuwa nikiishi kama ndege mkiwa juu ya mti ,nilikuwa sina msaada wowote nilikuwa nikipambana tu mwenyewe ilhali niko na mzazi mwenzangu,”

“Mpaka sasa nina mtoto ambaye ameacha chuo kwa sababu sina uwezo wowote ule wa kumsomesha na hata sijui nafanyaje, mwanangu wa mwisho amesoma chuo mwaka mmoja miaka mingine akashindwa kuendelea kutokana sina namana ya kumsaidia kutokana na ulemavu nilioupata kutokana na manyanyaso,”

Wasemavyo wadau

Akizungumzia matukio ya ukatili wa kijinsia, Mkurugenzi wa shirika lisislokuwa la kiserikali linalohusika na kutoa msaada wa kisheria wilaya ya Rombo, Mwanaidi Mkumbwa, anasema kuwa wilaya hiyo imekuwa na matukio mengi ya ukatili ikiwemo mauaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Anasema chanzo cha matukio hayo ni ulevi wa kupindukia unaosababishwa na umaskini kwa baadhi ya familia na ikitiliwa maanani kwamba wilaya hiyo ina aina nyingi za pombe za kienyeji ambapo inapelekea baadhi yao wanajikuta wanafanya ukatili bila kukusudia.

“Asilimia kubwa ya mauaji yanatokana na ulevi uliopindukia ambao unapelekea migogoro mbalimbali kwenye familia wakati mwingine ugomvi ambao husababisha watu kuuana na kujeruhiana, yapo matukio mengi ya namna hii kwenye jamii zetu,”anasema.

Anasema kuhusu suala la unyanyasaji wa kijinsia kuanzia Januari 2021 hadi Machi 2022 unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake ikiwemo vipigo walipokea jumla ya matukio 59 ambapo wanaume ni 13 na wanawake ni 46 na yote hayo alisema walifuatilia kuchunguza yanasababishwa na nini ambapo walkibaini chanzo cha matukio hayo ni ulevi uliokithiri ndani ya jamii watu kutumia madawa ya kulevya pamoja na ushirikiana.

Alisema zipo jitihada ambazo wanataka kuzianzisha ili kuangalia namna ya kukabiliana na mtukio hayo ambayo yamekuwa hayaishi katika wilaya hiyo ambapo alisema ni matukio ya kufedhehesha na kuchukiza.

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu tawala msaidizi mipango na uratibu katika mkoa wa Kilimanjaro, Melchior Temu, inaonyesha kwa kipindi cha Julai 2021 mpaka kufikia Machi 2022 zipo taarifa mbalimbali kutoka madawati ya polisi, madawati ya jinsia na ustawi wa jamii ,vituo vya kutolea huduma za tiba na mashirika ya kutetea hazi za usawa wa kijinsia ambapo jumla ya matukio 3056 yameripotiwa.

Anasema katika matukio hayo yapo ya ukatili wa kimwili (ikiwemo vipigo) ni matukio 1026 ambapo wanawake ni 662 na wanaume ni 364, ukatili wa kihisia ni 1630 ambapo wanawake ni 1237 na wanaume ni 393 huku ukatili wa kingono ukiwa ni 400 ambapo wanawake ni 316 na wanaume ni 84.

Anasema sababu kubwa za ukatili katika mkoa huo ni mila kandamizi za masuala ya kijinsia, upotovu wa maadili katika jamii, umaskini, imani za kishirikina pamoja na kulipiza visasi.