Vyama sita vyalamba ruzuku ya Sh1.4 bilioni

What you need to know:

  • Miezi miwili baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, vyama sita vyenye sifa ya kupata ruzuku vimeanza kuneemeka baada ya kuingiziwa mgawo wa fedha na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
  • Vyama ambavyo vimevuna fedha hizo za mgao wa ruzuku hiyo unaotokana na idadi ya wabunge, madiwani na kura za urais ni pamoja na CCM, Chadema, ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi na kile cha Democratic Party.

Dar es Salaam. Miezi miwili baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, vyama sita vyenye sifa ya kupata ruzuku vimeanza kuneemeka baada ya kuingiziwa mgawo wa fedha na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Vyama ambavyo vimevuna fedha hizo za mgao wa ruzuku hiyo unaotokana na idadi ya wabunge, madiwani na kura za urais ni pamoja na CCM, Chadema, ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi na kile cha Democratic Party.

Kwa mujibu taarifa ambazo gazeti hili linazo, chama kinachoongoza kwa kuzoa ruzuku hiyo ni CCM yenye wabunge 354 ambacho kimepata zaidi ya Sh1.33 bilioni, Chadema ‘inayohesabiwa’ kuwa na wabunge 20 imepata Sh109.68 milioni, ACT Wazalendo yenye wanne kimepata Sh14 milioni na CUF yenye mbunge mmoja ikipata Sh5.7 milioni.

Vyama vingine vinavyopata ruzuku kwa idadi ya kura za madiwani ni pamoja na NCCR Mageuzi kilichoambulia Sh316,937, huku DP ikiambulia Sh63,387.

Hata hivyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikuthibitisha juu ya kutolewa kwa fedha hizo, lakini vyama vitatu vimethibitisha kupata fedha hizo za ruzuku na mchanganuo wake.

Vyama vilivyothibitisha ni pamoja CCM, ACT-Wazalendo na CUF iliyoeleza imepata mchanganuo wa mgawo huo.

Alipoulizwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama kuhusu mgawo huo wa ruzuku kwa vyama, alielekeza suala hilo aulizwe msajili.

“Ni kweli jambo hilo liko katika ofisi yangu, lakini mtu anayeweza kulitolea maelezo ni msajili. Naomba muulize Jaji Mutungi atawapeni ukweli halisi bila shaka kila kitu atakueleza kwa mapana yake,” alisema.

Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema halifahamu suala hilo.


Vyama vyakiri kupata mgawo

Viongozi wa vyama vitatu vya CCM, ACT-Wazalendo na CUF waliithibitishia Mwananchi kuwa walikuwa wamepata mgawo huo wa ruzuku.

Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Catherine Peter alisema ruzuku waliyoipata ni ya mwezi Novemba, mwaka jana.

“Ruzuku tuliopwa ni ile ya Novemba mwaka jana, lakini kwa mwezi Desemba haijapatikana,” aliongeza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alikiri chama hicho kupokea ruzuku hiyo alipozungumza na Mwananchi kwa simu.

Ado alisema fedha hizo zimeingizwa moja kwa moja bila kuwa na kikao na Ofisi ya Msajili.

“Ni kweli tumepata... kwa mujibu wa sheria, ruzuku mpya inayotokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 kwa ratiba ya Msajili inalipwa Novemba.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa ruzuku huchelewa mwezi mzima, ruzuku mpya imeingia mwanzoni mwa Desemba.

Naye Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya, alisema kuwa chama hicho kilikuwa hakijapata fedha lakini kimetumiwa mchanganuo na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Mpaka sasa hatujapata ruzuku, ila jana tumepata mchanganuo, lakini naona haueleweki. Kwa sababu tunajua mbunge mmoja wa kuchaguliwa au viti maalum analipwa Sh4 milioni, sasa hicho kiasi kinachoonyeshwa hakieleweki,” alisema Sakaya.

Katibu Mkuu wa chama cha DP Abdul Mluya alisema bado hajapata uhakika kama ruzuku hiyo imeingia.

Vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na DP kwa upande wao havikuthibitisha juu ya taarifa za kupata ruzuku hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alipoulizwa suala hilo kwa simu hakuweka wazi akisema alikuwa likizo na hakumbuki kuona ruzuku mpya.

“Pesa iliyoingia mara ya mwisho nakumbuka ilikuwa ni ruzuku ya Oktoba ambayo ni zao la ruzuku ya 2015,” alisema Mwalimu akifafanua kuwa ruzuku hiyo huchelewa kwa mwezi mmoja.

“Kwa mfano ruzuku ya Januari inaingia Februari, ya Februari inaingia Machi. Kwa hiyo Novemba ruzuku iliingia lakini ni ya Oktoba ambayo ni zao ya ruzuku ya uchaguzi wa 2015 siyo ya uchaguzi wa 2020.”


Sintofahamu ruzuku ya Chadema

Hata hivyo, suala la Chadema kupelekewa ruzuku hiyo huenda likazua maswali kutokana na kuwapo kwa mgogoro na waliokuwa makada wake, ambao wamechukua nafasi 19 za viti maalum bungeni.

Tangu Novemba 2020 Chadema ilishatangaza kutoyatambua matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka jana ikidai kuwa uchaguzi huo hakuendeshwa kwa haki na pia haitajihusisha na kitu chochote kinachohusu uchaguzi huo.

Novemba 27, 2020 Kamati Kuu ya Chadema iliwafukuza wabunge 19 wa viti maalum kwa kosa la kwenda kuapishwa bungeni jijini Dodoma Novemba 24, 2020 bila idhini ya chama hicho.

Hata hivyo, wabunge hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho, (Bawacha), Halima Mdee waliandika barua za kukata rufaa Baraza kuu wakipinga hatua ya kuvuliwa uanachama.

Licha ya kususia matokeo hayo, Chadema yenye mbunge mmoja aliyechaguliwa katika jimbo la Nkasi Kaskazini, Aida Khenani pia ilipewa nafasi 19 za wabunge wa viti maalum na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambazo pia ilitangaza kuzisusia.

Juhudi za kuupata uongozi wa NCCR Mageuzi pia hazikufanikiwa baada ya simu ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Elizabeth Mhagama kuita bila kupokelewa kwa muda mrefu.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.