Vyama vya upinzani vya Tanzania, kiza kilichotawala

Vyama vya upinzani vya Tanzania, kiza kilichotawala

Muktasari:

Siasa ni mchakato endelevu ambao unavitaka vyama vya siasa kuendesha shughuli zao za kisiasa kila siku kwa kufanya mikutano ya hadhara, warsha, makongamano au kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali ya kichama na kitaifa.

Siasa ni mchakato endelevu ambao unavitaka vyama vya siasa kuendesha shughuli zao za kisiasa kila siku kwa kufanya mikutano ya hadhara, warsha, makongamano au kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali ya kichama na kitaifa.

Kwa maneno mengine, mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi mwingine. Vyama vinatakiwa kuanza maandalizi ya uchaguzi mwingine baada ya uchaguzi kukamilika ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata ushindi.

Kwa bahati mbaya, tangu uchaguzi wa Oktoba 28, 2020 ulipokamilika, vuguvugu la siasa lililozoeleka miaka ya nyuma baada ya uchaguzi sasa halipo tena, vyama vya upinzani vimepoa, havifanyi siasa motomoto.

Imekuwa nadra kusikia vyama vya siasa vikifanya jambo fulani mahali fulani. Tanzania ina vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, hata hivyo, hakuna chama cha upinzani ambacho kimesimama imara katika kutekeleza majukumu yake. Miaka ya nyuma, ilizoeleka kila baada ya uchaguzi mkuu kwisha, wagombea mbalimbali walioshindwa kwenye uchaguzi huo walikimbilia mahakamani kupinga matokeo yaliyotangazwa wakiwa na sababu zao.

Hata hivyo, safari hii hakuna wagombea waliojitokeza kupinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 28 hasa Tanzania Bara licha ya kuwapo kwa madai lukuki kwamba uchaguzi huo ulitawaliwa na udanganyifu wa dhahiri katika maeneo mengi kama vile Jimbo la Kawe kulikodaiwa kukamatwa kwa karatasi feki za kura.

Chadema na ACT Wazalendo waliungana kupinga matokeo ya uchaguzi huo uliompa ushindi Rais John Magufuli na kuitisha maandamano nchi nzima.

Hata hivyo, maandamano hayo hayakufanyika na tangu wakati huo, viongozi wa vyama vya upinzani “wamepotea”.

Katika salamu zake za mwaka mpya, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aligusia suala hilo akisema wananchi wamekosa imani na mfumo wa uchaguzi hapa nchini pamoja na mahakama zilizopo.

Mbowe alisema ufa katika Taifa hili ni mpana hasa baada ya uchaguzi akidai kwamba watu wengi wamekosa imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wamepunguza imani kwa Mahakama kama chombo cha kutoa haki.

“Kwa mara ya kwanza hakuna Watanzania waliokwenda Mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi, huo ni ushahidi kwamba wamekosa imani na uchaguzi pamoja na kupunguza imani na mahakama zetu,” alisema Mbowe.

Mwanasiasa huyo alibainisha kwamba mwaka 2021 utakuwa mwaka wa kudai Katiba mpya kwa madai kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kutibu majeraha ambayo Watanzania wanapitia katika nyanja tofauti za maisha.

“Ni rai ya chama chetu kwenu wote tushirikiane bila kujali mipaka ya tofauti zetu… tufikirie kwa pamoja tuitafute Katiba ya wananchi ambayo inatibu majeraha yetu sote,” alisema Mbowe katika hotuba yake.

Hata hivyo, kiongozi huyo hakubainisha ni jinsi gani chama chake kitakavyoidai katiba hiyo na mchakato huo utaanza lini. Itakumbukwa kwamba Rais Magufuli aliwahi kusema katiba mpya siyo kipaumbele katika utawala wake.

Ukimya huo umekuwa na tafsiri tofauti miongoni mwa wadau mbalimbali na baadhi yao wanasema ni utekelezaji wa katazo la Rais John Magufuli la kufanya mikutano ya hadhara isipokuwa kwa wabunge pekee katika majimbo yao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala anasema upinzani unapita katika kipindi kigumu kwa sasa, lakini hauwezi kufa kwa sababu umejengwa kikatiba.

Anasema vyama vya upinzani vinashindwa kufanya siasa kwa sababu havitakiwi kufanya mikutano ya hadhara licha ya kwamba Katiba ya Tanzania inaruhusu vyama vya siasa kuendesha shughuli zao kwa kufuata sheria.

“Vyama vya upinzani vimedhibitiwa na watawala, haviwezi tena kufanya mikutano ya hadhara. Sasa kama havifanyi mikutano vitafanyaje kazi zao? Wananchi hawawezi kuviona tena kwa sababu mikutano ya hadhara ndiyo inawakutanisha,” anasema.

Mwanazuoni huyo anasema wananchi wamepoteza imani na Tume ya Uchaguzi kwa sababu hawaoni haja ya kwenda kupiga kura kwa sababu kura zao hazitaheshimika. Anasema vyama vya siasa na wananchi wamekata tamaa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu anasema wapinzani wameshindwa kukata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi kwa sababu ya mambo matatu makubwa.

Kwanza, anasema mfumo wa kupinga matokeo umejaa vikwazo vingi vya kifedha na kimfumo.

Shaibu anasema ili mgombea aweze kufungua kesi, anatakiwa kuweka dhamana ya fedha kiasi cha Sh5 milioni ili endapo atashindwa kesi, fedha hizo zifidie gharama za kesi.

Jambo la pili, anasema watu wamekata tamaa na mifumo ya utoaji haki hususani Mahakama.

Wanaamini kwamba wakienda mahakamani hawawezi kutendewa haki kwa sababu mchakato mzima wa uchaguzi haukuwa mzuri.

“Jambo la tatu, watu wameona uwepo wa mkakati wa kupora uchaguzi kwa kutumia vyombo vya dola. Sasa unakataje rufaa kwa watu waliokupora ushindi, haki itatendeka kweli?” anahoji Shaibu.

Kiongozi huyo ambaye pia alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Tunduru, anasema maisha lazima yaendelee baada ya uchaguzi na chama chake kinabuni mbinu za kukiwezesha kuishi katika mazingira yaliyopo.

“Hatuwezi kukwepa bila kugusa kiini cha tatizo. Tutalazimika kuwa na vuguvugu la mabadiliko katika Tume za uchaguzi Bara na Zanzibar,” anasema Shaibu wakati akizungumza na Mwananchi.

Akiwa na mtazamo tofauti, Katibu Mkuu wa NLD, Tozi Matwanga anasema vyama vya siasa vyenyewe vina hofu ya kwenda kwa wananchi huku akisisitiza kwamba hakuna aliyezuia vyama kufanya shughuli zao.

“Nakumbuka Rais Magufuli alikataza mikutano ya hadhara kipindi kilichopita, tangu ameanza kipindi hiki, sijamsikia akisema tusifanye mikutano ya hadhara, ni sisi wenyewe tuna hofu,” anasema kiongozi huyo.

Kuhusu wapinzani kutokwenda Mahakamani, Matwanga anasema madai ya wapinzani katika uchaguzi uliopita hayana hoja za kisheria bali ni malalamiko tu kama ambavyo imekuwa ikitokea kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

“Malalamiko yapo lakini hayana hoja za kisheria, ndiyo maana hawajaenda mahakamani,” anasema Matwanga ambaye chama chake hakikusimamisha mgombea urais katika uchaguzi wa Oktoba 28, 2020.