Waandishi wa habari wageukia mazingira, wapanda miti Sao Hill
Mhifadhi Mkuu wa shamba la Miti Sao Hill PCO Tebby Yoram akielezea namna ya shughuli za kuendelea kuhifadhi na kutunza miti ya asili ambayo mingine husaidia katika kulinda vyanzo vya maji. Picha na mwandishi wetu
Muktasari:
- Mwenyekiti mstaafu wa Misa-Tan ambaye pia ni wakili, James Malenga amesema lengo la kutembelea shamba hilo ni kujifunza kwa vitendo kuhusu aina mbalimbali za miti, ikiwemo ya asili na ya kupandwa, pamoja na michakato ya uzalishaji na uvunaji wa mazao ya misitu.
Mufindi. Waandishi na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini ambao ni wanachama wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-TAN), wamepanda miti 140 katika shamba la miti la Sao Hill wilayani Mufindi, mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani inayoadhimishwa Machi 21 kila mwaka.
Kazi hiyo imefanyika kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ikilenga kuhamasisha uhifadhi wa misitu na uendelezaji wa miti ya asili ambayo ina mchango mkubwa katika kulinda vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.
Akizungumza leo Jumatano, Machi 19, 2026, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, Tebby Yoram amesema lengo la upandaji huo ni kuendelea kuhifadhi na kutunza miti ya asili, sambamba na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mbegu za miti hiyo.
Amesema wanachama hao wa Misa - Tan wamepata fursa ya kutembelea shamba hilo kwa ajili ya kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa, ikiwamo uzalishaji wa miche, upandaji na uvunaji wa mazao ya misitu.
Aidha, Yoram amesema miti iliyopandwa ni ya aina ya Mkangazi na Mkongo, ambayo hutumika kwa mbao katika shughuli za ujenzi na utengenezaji wa samani, lakini imekuwa ikipungua kwa kasi kutokana na matumizi makubwa.
“Zoezi hili limekwenda vizuri na tumefurahishwa na ujio wao. Tunaamini waandishi wa habari ni mabalozi muhimu wa kuifikia jamii kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu uhifadhi wa misitu na mchango wake katika maendeleo ya taifa,” amesema Yoram.
Ameongeza kuwa upandaji huo wa miti ya asili utasaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu, hatua itakayochangia kulinda spishi hizo zisipotee nchini.
Kwa upande wake, mmoja wa wanachama wa Misa-Tan, Teresia Method amesema wamefika mkoani Iringa kwa ajili ya mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi hiyo, lakini pia wanatumia fursa hiyo kutembelea vivutio mbalimbali, ikiwemo shamba la miti la Sao Hill.
Amesema ziara hiyo imewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa misitu katika maisha ya binadamu na mazingira, hasa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
“Tumejifunza kwamba misitu ina mchango mkubwa katika uchumi na ustawi wa jamii. Ikiwa tutaiwekeza na kuitunza ipasavyo, tunaweza kunufaika na mazao yake pamoja na kulinda vyanzo vya maji,” amesema Teresia.
Awali, akizungumzia ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Misa-Tan ambaye pia ni wakili, James Malenga amesema lengo la kutembelea shamba hilo ni kujifunza kwa vitendo kuhusu aina mbalimbali za miti, ikiwemo ya asili na ya kupandwa, pamoja na michakato ya uzalishaji na uvunaji wa mazao ya misitu.
Amesema kupitia maelezo waliyopatiwa, wamebaini kuwa shamba hilo lina mchango mkubwa kiuchumi, likikusanya zaidi ya Sh30 bilioni kwa mwaka kutokana na mazao ya misitu.
Hata hivyo, Malenga amesema wanachama wa Misa-Tan wataitumia ziara hiyo kama jukwaa la kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa misitu na mchango wa shamba la Sao Hill katika kukuza uchumi wa taifa pamoja na kuhifadhi mazingira.