Waathirika mafuriko Morogoro wahifadhiwa, mmoja awalilia kuku wake

Muktasari:

  • Kaimu Kamanda Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Mkaguzi Emmanuel Ochieng amesema wameweza kuokoa watu 48 katika ajali ya mafuriko na wamepelekwa katika ofisi ya Kata ya Kihonda ili kupatiwa msaada na serikali

Morogoro. Kaimu Kamanda Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Mkaguzi Emmanuel Ochieng amesema wameweza kuokoa watu 48 katika ajali ya mafuriko na wamepelekwa katika ofisi ya Kata ya Kihonda ili kupatiwa msaada na serikali.

 Amesema hayo leo Ijumaa Januari 13, 2023 eneo la Kihonda wakati akizungumza na Mwananchi Digital baada ya kufanya uokozi wa watu na mali zao waliokubwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia Januari 13 mwaka huu.
Ocheing amesema walipata taarifa kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa kuwa kuna matukio mbalimbali hasa kwa kata ya Kihonda na askari kuanza kwenda kufanya uokoaji na kwamba wamefanikiwa kufanya uokoaji na hakuna kifo wala majeruhi.

“Askari wako kwenye maeneo yote ambayo yalitolewa taarifa na kwamba kwa sasa hali ya hewa imebadilika hivyo tahadhari inatakiwa kuchukuliwa, na wale waliopo kwenye maeneo hatarishi kwenye mikondo inayopitisha maji watafute utaratibu zaidi kwa ajili ya usalama wao.
Aidha alitoa wito kwa wale waliochimba mashimo ya taka na karo kuwa ni hatari kwa wanafunzi, wazee na watoto na kuwataka kuhakikisha wanayafukia mara moja kwa ajili ya usalama wa watu wote.

Mmoja wa waliopata athari ya mafuriko hayo Simon Mkude mkazi wa Mtaa wa Magunila Kihonda, Manispaa ya Morogoro amesema, “Adha tuliyoipata hapa ni maji tangu saa nane na hatujalala. Nyumba zimejaa matope tuna kazi ya kuyaondoa, hakuna chombo chochote kilichobaki kwa sababu vyote vimesombwa na maji. Maeneo ya Mbuyuni, Majengo Mapya yote tumeathirika.”

Ameeleza baada ya mvua kunyesha imesababisha madhara ikiwemo maji kuingia majumbani, kusomba vitu mbalimbali kama vyombo vya ndani, nyumba kujaa tope.

Mkude amesema alisikia mvua ikinyesha kuanzia saa nane akafikiri kuwa ni zile mvua za kawaida, kisha akaendelea kulala. Hata hivyo baadaye alisikia maji yakiingia ndani na alipoamka alikuta tayari yamesambaa. Baada ya muda mfupi aliwaamsha watoto na mkewe na kuangalia namna ya kutoka nje.
Alisema kazi walioifanya ni kuanza kutoa maji na tope. Ameiomba serikali kuangalia taratibu ya kusaidia wananchi wake, huku akilalamikia ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR) kuleta athari zote kwenye makazi ya wananchi.

Mgaya Ramadhani mkazi wa Mtaa wa Tuelewane alisema miaka ya nyuma mvua zilipokuwa zikinyesha bila kuleta madhara makubwa na kwamba kila mkondo ulikuwa na njia yake lakini baada ya kujengwa kwa barabara hiyo ya reli mambo yamekuwa tofauti.

“Vitu vingi vimepotea watu wamepoteza mali zao, nyumba zimebomoka upande mmoja. Mimi mwenyewe nika kuku zangu broila sitini ambazo nimezifuga ili nipate kipato lakini zote zimepotea. Naomba serikali ituangalie kwa jicho la pili miundombinu ya mvua inatuharibia maisha watu wengi hawana pa kukaa wala pakulala,”alisema.

Mkuu wa Milaya ya Morogoro, Albert Msando akizungumzia tukio hilo la mafuriko alisema kwa sasa ameita kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kwa ajilli ya kufanya tathmini ya athari iliyotokea na kwamba hajapata taarifa yoyote ya watu kujeruhiwa ama vifo.

Msando akawataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na mvua hizi zinazoendelea kunyesha wilayani Morogoro ambapo alieleza kuwa wanapaswa kutoa taarifa pindi watakapoona tatizo lolote limejitokeza.

Kutokana na kutokea kwa mafuriko hayo jana barabara ya Morogoro Dodoma ilifungwa kwa zaidi ya saa sita baada ya maji kukatisha barabara hiyo eneo la Kihonda Mbuyuni huku kukiwepo na msululu wa magari yakiwemo ya abiria na mizigo.