Wabakaji wa ‘teleza’ wawagonganisha Zitto, Lugola bungeni

Mbunge wa Kigoma mjini (ACT), Zitto Kabwe akiomba mwongozo bungeni jijini Dodoma leo, kuhusu uwepo wa wanaume wanaowafanyia vitendo vya kinyama wanawake mkoani Kigoma ikiwemo ubakaji. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Wanaume wanaodaiwa kujipaka mafuta machafu aina ya oil maarufu ‘Wanaule teleza’ kisha kuwabaka wanawake mkoani Kigoma, wamesababisha mvutano kati ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe wamevutana bungeni kuhusu wanaume wanaojipaka oil chafu maarufu ‘wanaume teleza’ kisha kuwabaka wanawake mkoani Kigoma.

Mvutano huo umeibuka leo Jumanne bungeni Mei 21, 2019 mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika.

Baada ya kipindi hicho kumalizika, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga alimpa nafasi Zitto kutoa maelezo akitumia kanuni ya 47 (1) akisema jimbo la Kigoma kwa miaka mitatu kumeibuka tabia ya vijana kujipaka oil chafu, kuwavamia na kuwabaka wanawake.

“Usiku wa kuamkia jana, siwezi kumtaja jina kwani yuko hospitali, amejeruhiwa kwa kupigwa nondo, mwingine amepigwa kisu,” amesema Zitto.

Amesema shirika lisilo la kiserikali la Tamasha, wamekusanya matukio ya wanaume teleza na kubaini matukio kama 43.

Zitto ambaye ni kiongozi wa ACT-Wazalendo amesema mashirika hayo yamemwandikia barua yeye, waziri wa mambo ya ndani na mashirika mengine lakini mpaka sasa hatujaona ufuatiliaji wa Serikali.

“Nimelileta hapa bungeni na tukio hili linasononesha kama mbunge wa Kigoma Mjini, tunashindwa kulinda dada zetu, mama zetu, watoto zetu,” amesema Zitto wakati Bunge zima likiwa kimya kumsikiliza.

“Ninaomba kiti, kielekeze Serikali ilete ndani ya Bunge, taarifa ya hatua gani wamechukua mpaka sasa kukomesha vitendo hivi na kuchukua hatua kali kwa wote wanaodhalilisha wanawake.”

Baada ya kumaliza kutoa maelezo hayo, Mwenyekiti wa Bunge, Giga akasema Serikali imesikia kwa upeo unaostahiki, Serikali kama wataweza kutupa taarifa sasa au baadaye sawa.

Hata hivyo, Waziri Lugola alisimama kuzungumzia maelezo hayo ya Zitto akisema ubakaji ni kosa la jinai na linaadhibiwa kisheria na kwamba vitendo hivi vya makosa ya aina hii vimekuwa vikitokea si Kigoma tu hata maeneo mengine na vimekuwa vikidhibitiwa.

“Kwa mkoa wa Kigoma, matukio aliyosema Zitto ni kweli vinadhalilisha na walikuwa wanajikuta mtu ambaye haonekani kwa macho na mwanamama anajikuta sehemu zake za siri amelowa,” amesema Lugola na kuongeza kuwa mwanamke akitaka kumshika mtu huyo analeteza.

“Vitendo hivi vimeendelea kudhibitiwa na nilipopata taarifa kutoka kwa Zitto na mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze. Lakini jambo hilo si kubwa kwa kiasi hicho, kama anavyosema Zitto, tukiangalia taarifa katika vitabu vyetu pale Kigoma, hakuna taarifa zilizoripotiwa mpaka leo,” amesema waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Mwibara (CCM)

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, hakuna tukio lolote lililohusisha mwanamke kubakwa isipokuwa yapo matukio matatu ya kubakwa yanayohusisha wanawake kujeruhiwa katika nyumba zao

Waziri Lugola amesema yawezekana katika kujeruhiwa hawakufikia kiwango cha kutenda kosa.

“Kwenye maeneo mbalimbali katika nchi yetu, kuna baadhi ya taasisi au mtu mmoja mmoja, wanakuza mambo na kujenga hofu, niseme bayana, taasisi ambazo zinakwenda kufanya tafiti na kukuza mambo, tumeanza kuziorodhesha na hatua zitaanza kuchukuliwa,” amesema Lugola.

Wakati wote huo, Zitto alikuwa akisimama mara kwa mara kutaka kuzungumza lakini Mwenyekiti Giga anamzuia akimtaka kusubiri waziri amalize kisha atampa nafasi ya kuzungumza.

“Kama Zitto una taarifa hizo, niko tayari kwenda Kigoma na nitachukua hatua,” amesema Waziri Lugola.

Baada ya kumaliza, Giga alimpa nafasi Zitto ambaye alisema, “Ni kwa bahati mbaya sana, waziri mwenye dhamana kwenye usalama wa wananchi wetu wakiwemo wanawake kuzungumza kama alivyozungumza sasa.”

“Mwanzoni mwa mwaka 2016, akina mama hawa waliripoti polisi na kamanda aliyekuwepo alidhibiti na baadaye alihamishwa. Ma RPC waliofuata walianza kuwadhihaki na kuwaita wanawake wa teleza,” amesema Zitto.

Kauli hiyo imemfanya Waziri Lugola kusimama kutaka kuzungumza lakini Giga amemzuia akimtaka kutulia amwache Zitto azungumze.

“Ni akina mama gani watakwenda polisi kutoa taarifa na kukejeliwa,” amehoji Zitto

‘Mimi kama mbunge wa Kigoma Mjini, ninawaomba wanawake wa ndani ya Bunge hili, wafumbe macho, kuvuta hisia za kuingiliwa waone ilivyoshida katika mambo hayo mabaya,” amesema.

Waziri Lugola alisimama tena bila kuruhusiwa akisema, “Niko tayari kwenda Kigoma hata leo.”

Baada ya Zitto kumaliza, Giga amehitimisha suala hilo akisema waziri amejibu alivyoelewa, Zitto ameeleza anavyolielewa suala hilo.

“Waziri kama huna taarifa, hili jambo hata liwe dogo, litaleta shida, suala la ubakaji liwe kwa watoto au wakubwa sio la kuvumiliwa,” amesema Giga huku akishangiliwa.

“Mheshimiwa Kangi kama huelewi, nakuelekeza nenda Kigoma kashughulikie hilo,” amesema Giga.