Wabunge ahoji mkakati wa Serikali matumizi ya gesi asilia majumbani, kwenye magari

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha 46 cha mkutano wa bunge la bajeti jijini Dodoma leo, Juni 12, 2024. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Wakati wabunge wakihoji mikakati ya Serikali katika kupunguza matumizi ya mafuta kwenye magari, yenyewe imesema hadi kufikia Desemba 2025 watakuwa wamefungua vituo 16 vya kujazia gesi asilia kwenye magari.
Dodoma. Wabunge wameibua mjadala wa kupunguza matumizi ya petroli na dizeli katika magari huku Serikali ikisema vituo 16 vya kujazia gesi asilia kwenye magari, vikijumuisha vinavyohamishika, vinatarajiwa kufunguliwa ifikapo Desemba 2025.
Mjadala huo umeibuka leo Juni 12,2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu baada Mbunge wa Kawe, (CCM), Askofu Josephat Gwajima kuhoji ni lini Serikali itakuja na mkakati wa kutumia gesi asilia kuendesha magari nchini, ili kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali ilishaanza programu mbalimbali za matumizi ya gesi iliyogandamizwa yaani CNG kwenye magari.
“Mpaka sasa, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kufungua vituo vitano na inatarajia kufungua vituo vingine tatu ifikapo Desemba, 2024,”amesema.
Aidha, amesema jumla ya vituo 16 (vituo mama 2 na 14 vidogo) vikijumuisha vinavyohamishika vinatarajiwa kufunguliwa ifikapo Desemba, 2025.
“Ili kuongeza upatikanaji wa gesi asilia, mwaka 2022 Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ilifunga set 3 za compressor zilizoweza kuongeza pressure ya futi za ujazo milioni 20,”amesema.
Amesema kwa sasa TPDC imeanza utaratibu wa kumpata mzabuni kwa ajili ya kufunga mitambo ya kuongeza mgandamizo wa gesi yenye futi za ujazo milioni 20 kwenye kitalu cha uzalishaji Songosongo na kazi inatarajia kukamilika Machi, 2026.
Amesema kwa upande mwingine, ili kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumia gesi asilia, Serikali inaendelea kutoa msamaha wa kodi kwenye mitungi ya kuhifadhi gesi iliyoshindiliwa kwenye magari na kupunguza ushuru wa magari yanayotumia gesi asilia.
Amesema wanaamini mikakati yote hii itachangia kuongeza idadi ya magari yanayotumia gesi nchini ili kupunguza uagizaji wa mafuta nje ya nchi na mwisho kuokoa fedha za kigeni.
Katika swali la nyongeza, Askofu Gwajima amehoji Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kufungua vituo njiani ili mtu anapokuwa anasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kuwe na vituo maalumu vya gesi asilia ili iwe rahisi kujaza inapopungua au kuisha.
Akijibu swali hilo, Kapinga amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wameanza mkakati wa kuona namna ya kuwa na vituo kwa magari binafsi kuanzia Dar es Salaam mpaka Dodoma.
Amesema kwa awamu ya kwanza wameshaanza mkakati huo na tayari wadau wa sekta binafsi wamejitokeza kwa ajili ya kuwekeza kwenye nyanja hiyo kwa kufungua vituo barabarani kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Amesema hata kwa upande wa magari ya Serikali tayari TPDC imeanza mazungumzo na Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) ili kuongeza vituo vya CNG kutoka Dar es Salaam Kwenda Dodoma ili nayo yaweze kujazwa.
“Kwa hiyo nimuhakikishie mheshimiwa mbunge kwa pande zote mbili za sekta za magari binafsi na magari ya Serikali tumeshaanza kulifanyia kazi ili kuongeza magari yanayotumia CNG,”amesema.
Mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Mohamed Said Issa ametaka kujua mpango wa Serikali kupunguza gharama ya kubadili mfumo wa magari kutoka kwenye mafuta kwenda kwenye gesi ambao kwa sasa ni Sh2.5 milioni.
Akijibu swali hilo, Kapinga amesema gharama ziko juu kidogo na ndio maana Serikali wameendelea kuhamasisha watu wengi na kampuni nyingi zaidi ziwekeze karakana.
“Tunakubali mwanzo huwa ni mgumu sana lakini tunakoelekea ni kuzuri kuliko tulikotoka.”
Amesema wastani magari yaliyokuwa yakibadilishwa mfumo wa gesi yalikuwa 1,159 mwaka 2021 lakini leo magari 5,100 yamebadilishwa mfumo kwa sababu karakana zimeongezeka kutoka moja ile ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) mpaka karakana nane.
“Kwa hiyo wawekezaji wengi wanavyokuja ndivyo gharama inaendelea kushuka kutokana na ushindani. Nimuhakikishie mheshimiwa mbunge tunaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza na kuja na teknolojia bora zaidi. Tukiwa na karakana nyingi zenye teknolojia bora basi gharama zitapungua,”amesema.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba amehoji nini mkakati wa Serikali wa kuhamasisha watu kuleta magari ya umeme nchini ili kuendelea kupunguza matumizi ya mafuta na gesi.
Akijibu swali hilo, Kapinga amesema kama wanavyowekeza matumizi wa gesi asilia na ndivyo ambavyo wameshaanza mikakati ya kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuleta magari yanayotumia umeme.
Naye Mbunge wa Ulyankulu (CCM), Rehema Magila amesema magari mengi yanayotumia gesi ni magari ya petroli tu.
“Sasa je ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha na magari yanayotumia dizeli na yenyewe yanaanza kutumia gesi. Kwa nini tunaona Kampuni ya Dangote magari yake yanatumia dizeli lakini wamefungwa gesi?”amesema.
Akijibu swali hilo, Kapinga amesema wameanza mazungumzo na wawekezaji kwenye sekta binafsi ili kuhakikisha wanaona namna ya kuwa na mifumo yote miwili yaani petroli na dizeli.
Naye, Mbunge wa Viti Maalumu, (CCM) Munira Mustafa Khatib amesema mpango wa Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi na salama. Hivyo ni upi mkakati wa kusambaza mabomba ya gesi asilia ili wananchi watumie nishati safi.
Akijibu swali hilo, Kapinga amesema awamu ya kwanza ya gesi majumbani wamesambaza katika maeneo ya Mikocheni na Mbezi jijini Dar es Salaam.
Amesema lengo ni kuweka miundombinu kwenye maeneo mengi kwa Mkoa wa Dar es Salaam ili wananchi wengi watumie gesi majumbani ambayo ni nafuu kuliko ya mitungi ili kufikia azima ya Serikali ya asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034.