Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Udzungwa wataka gesi ya kupikia kukabiliana na ukataji miti

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Theodora Batiho akizungumza na ujumbe wa chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira ofisini kwake, Kilombero mkoani Morogoro. Picha na Mpigapicha Maalumu

Muktasari:

  • Nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia majumbani inatajwa kuwa mwarobaini wa ukataji miti ndani ya hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na pia kuhifadhi ikolojia ndani ya hifadhi hiyo iliyopo mkoani Morogoro.

Morogoro. Ili kukabiliana na ukataji wa miti kwenye hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa kwa ajili ya kuni, mkuu wa hifadhi hiyo, Theodora Batiho amewaomba wadau kujitokeza kuwapatia wananchi nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia majumbani.

Amesema hiyo itakuwa njia mbadala ya kuwasaidia wananchi hao kuepukana na madhara ya matumizi ya kuni lakini pia itasaidia kupunguza ukataji wa kuni kwenye hifadhi hiyo, jambo ambalo ni hatari kwa ikojojia ya hifadhi hiyo.

Bahito amebainisha hayo hivi karibuni katika Kijiji cha Mang’ula kilichopo Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wakati alipotembelewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

JET inatekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kwa lengo la kuhamasisha shughuli za uhifadhi kwa wananchi na kupitia mradi huo, imekuwa ikitembelea shoroba za wanyamapori na kuhamasisha uhifadhi wake.

Akizungumza na JET, Batiho amesema wananchi katika vijiji vinavyoishi jirani na hifadhi ya milima ya Udzungwa wanakabiliwa na changamoto ya nishati ya kupikia, hivyo wanalazimika kuingia msituni kukata kuni, jambo ambalo haliruhusu kisheria.

“Tunaomba wadau wa maendeleo wajitokeze kuwasaidia wananchi hawa kupata majiko ya gesi lakini pia elimu ya matumizi ya majiko hayo. Hii itatusaidia sana hasa kwenye masuala ya uhifadhi ili tuondokane na changamoto hiyo,” amesema.

Amebainisha kwamba walitoa ruhusa kwa wananchi kuingia ndani ya hifadhi kuokota kuni, lakini sasa wamezuia baada ya watu waovu kutumia mwanya huo kufanya ujangili ndani ya hifadhi hiyo.

Batiho amesisitiza kwamba hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ni ya kimkakati na moja ya mkakati huo ni kuhifadhi maji kwa ajili ya wananchi wa Morogoro. Amesema hifadhi hiyo ina vyanzo 11 vya maji ambavyo vinahifadhiwa.

Katika kupunguza tatizo la ukataji miti, Shirika la Associazione Mazingira linahamasisha na kuzalisha majiko banifu ambayo yanawawezesha wananchi kutumia mkaa mbadala badala ya kuchoma mkaa au kukata kuni.

Mratibu wa Programu ya Jamii katika shirika hilo, Felister Mwalongo amesema wanahamaisha matumizi ya majiko banifu kwa wananchi na taasisi mbalimbali na wameunda vikundi vya wazalishaji wa mkaa mbadala.

“Tumejenga majiko banifu kwenye shule 10 kati ya 18 zilizopo hapa, pia tumejenga majiko haya kwenye kaya 52. Tunaendelea kuhamasisha wananchi watumie majiko haya na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa,” amesema.

Mwalongo amesema kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, wanashirikiana na Reforest Afrika katika urejeshaji kwenye ushoroba wa Nyerere Selous – Udzungwa na jukumu lao ni kuhamasisha wananchi kati jambo hilo ambapo sasa wamewafikia wanafunzi 300 na walimu 45 katika shule tatu kuanzia Januari – Mei, mwaka huu.

Kwa upande wao, wanawake wanaozalisha mkaa mbadala wamebainisha kwamba wanazalisha mkaa mbadala kwa kutumia mabaki ya mimea kama vile majani, mabaki ya miti, pamba na Maranda ya mbao.

“Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni upatikanaji wa malighafi hasa msimu wa mvua. Tuna mashine yenye uwezo wa kuzalisha kilo 300 kwa saa lakini hatufikii kiwango hicho kwa sababu hatupati malighafi za kutosha,” amesema Restuta Ruwanga, katibu wa kikundi cha Mazingira Group.

Kwa upande wao, watumiaji wa mkaa huo wameeleza kwamba wanapata unafuu mkubwa wanapotumia mkaa huo kwa kuwa gharama zake ni ndogo na unadumu kwa muda mrefu, jambo ambalo linawapunguzia mzigo wa nishati.

“Mkaa wa kawaida ni mwepesi, huu mbadala ni mzito na unachelewa kwisha. Mkaa huu wa Sh2,000 tu unaweza kutumia siku mbili wakati ule wa kawaida unatumia Sh10,000,” amesema Halima Rashid, mkazi wa Kijiji cha Mang’ula anayefanya kazi ya mama lishe.