Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nishati safi njia sahihi kukabili mabadiliko ya tabianchi, jitihada zinahitajika

Dar es Salaam.   Takwimu za Shirika la Nishati la Kimataifa (IEA) zinasema takriban asilimia 75 ya utoaji wa gesi chafu duniani hutoka kwenye sekta ya nishati. Hili linafanya sekta hiyo kuwa changamoto zaidi kwenye jitihada za mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kutokana na ukweli huu dunia iliweka malengo ya kupunguza matumizi ya nishati zinazozalisha hewa chafu ambazo kwa kiasi kikibwa ni nishati kisukuku (makaa ya mawe, mafuta na gesi) ili kupunguza ongezeko la  joto la dunia lisizidi nyuzi joto 1.5 °C ifikapo mwaka 2030 ambapo tayari hadi 2023 joto la dunia lilifika 1.1 °C .

Kwenye matumizi ya nishati safi nchini tumepiga hatua tangu kuanza kufanya kazi kwa bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP). Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zilionyesha Desemba 2023 asilimia 71 ya umeme ilizalishwa kutokana na gesi na asilimia 32 ilikua maji.

Lakini hadi Machi 2024 umeme wa maji uliongezeka hadi asilimia 38 na kupunguza utegemezi kwenye gesi iliyopungua hadi asilimia 59 wakati vyanzo vingine vikichangia asilimia tatu. Huu ni mwelekeo mzuri.

Mbali na nishati, shughuli nyingine za binadamu zinazochangia ongezeko la hewajoto ni udhibiti mbovu wa taka, kilimo hasa matumizi ya baadhi ya mbolea za viwandani lakini jingine ni ukataji wa miti kwa ajili ya makazi au nishati ya kupikia.

Kwenye uharibifu wa mazingira hasa ukataji miti bado kuna changamoto. Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) asilimia 90 ya matumizi ya jumla ya nishati nchini hutegemea miti (kuni, mkaa) huku takriban asilimia 2 ikitoka kwa umeme na asilimia 8 kutoka kwa bidhaa za mafuta.

Pia licha ya kwamba, Utafiti wa Kitaifa wa ufuatiliaji wa kaya wa 2020/21 (NPS) uliozinduliwa Januari 2023 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ulionyesha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yaliongezeka kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014/15 hadi asilimia 10.2 mwaka 2020/21, hado kuna kazi kubwa sana.

Kwa sababu hii inamaanisha kwamba hadi mwaka 2020/21, Watanzania tisa kati ya kumi wanatumia nishati isiyo safi kwa kupikia, huku ikitaja kuni na mkaa kama vyanzo vikuu vya nishati.

Pia, Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) uliozinduliwa hivi karibuni ulinukuu takwimu za Benki ya Dunia za Mwaka 2023, idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia imekua ikiongezeka kwa kiwango kidogo kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 6.9 mwaka 2021.

‘Kiwango hiki ni chini ya kiwango cha wastani cha dunia cha asilimia 71 kwa mwaka 2021” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo pia ilitaja nishati safi ni “teknolojia au nishati safi kwa matumizi kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha sumu ni pamoja na umeme, bayogesi, gesi asilia, LPG, bayoethano, nishati ya jua, majiko banifu na mkaa mbadala wenye viwango vilivyothibitishwa na mamlaka ya kudhibiti viwango.” 

Itakumbukwa kuwa kuzinduliwa mkakati huu ni mwendelezo wa mikakati ya nchi iliyoanza muda mrefu na Desemba 2023 kwenye mkutano mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi (COP28) uliofanyika huko Dubai Rais Samia Suluhu Hassan alihadi kuja na mpango huo ili uwe mwongozo kwa nchi za Afrika.

Mpango wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Wanawake Afrika (AWCCSP) unahimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kushughulikia changamoto za kiafya, kimazingira, kiuchumi na kijamii ambazo mara nyingi zinaathiri wanawake na watoto.

"Tunazindua mradi huu kwenye COP28 kuonyesha uwajibikaji wetu licha ya kuwa na utoaji mdogo wa hewa joto, suala la nishati safi ni sehemu ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na usalama wa wanawake," alisema Rais Samia kwenye mkutano huo.

Rais aliyasema hayo kutokana na ukweli kwamba nchi za Afrika zinachangia chini ya asilimia nne ya uzalisaji hewa joto duniani.

Kwenye mkakati huu lengo kuu ni, “Kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034”.

Mkakati huo unaeleza utatekeleza haya kwa kuteleza malengo kumi ikiwemo Kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika na kupunguza gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia.

Mengine ni kuandaa, kuhuisha na kuoanisha sera, sheria, kanuni na miongozo wezeshi itakayofanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Kuhamasisha Uwekezaji, Kujenga uwezo wa watekelezaji wa miradi, kujumuisha masuala ya VVU na Ukimwi katika shughuli za nishati safi ya kupika.

Kujumuisha masuala ya usawa wa kijinsia katika masuala ya nishati safi ya kupikia na kuimarisha utawala bora katika masuala yanayohusu nishati safi ya kupikia.

Malengo haya yote yamewekewa mikakati, shabaha na upimaji wa matokea katika muda husika uliopangwa wa utekelezaji na wahusika wa kutekeleza hayo.

Mpango kazi wa utekelezaji wa hili unalenga kutekeleza mikakati midogo midogo 20 kwa gharama ya Sh4.554 trilioni.

Mjadala wangu utakuwa kwenye kupunguza gharama za nishati safi na kupata hizo trilioni za shilingi kutekeleza mkakati huu.

Hapa nitanukuu mambo kadhaa niliyoyasoma kwenye makala iliyoandikwa na mdau wa mazingira kwenye gazeti hili, Clay Mwaifwani. Ameandika mambo mengi kwenye makala iliyokuwa na kichwa cha “Nishati Safi ya Kupikia: Wanaoongea ni wengi lakini bosi ni hela”.

Mwaifwani alitukumbusha uhalisia kuwa kabla ya kubeba ajenda hii tukumbuke kuwa misitu mingi ipo vijijini na wanavijiji wanatumia zaidi kuni, hasa zile zinazodondoka zenyewe bila kukatwa na mti wakati watu wa mjini wanatumia zaidi mkaa.

Alisema kuwa licha ya maeneo mengi ya mijini kama Dar es Salaam kuunganishwa na umeme zaidi ikilinganishwa na maeneo ya vijijini bado watu wa mkoa huu wanatumia zaidi mkaa kuliko wa vijijini.

Hapa jambo la haraka la kujiuliza ni kwanini matumizi ya mkaa ni makubwa hata mijini ambapo kuna umeme? Je mtu wa kijijini anayeishi kwa kuokota kuni au kukata mti shambani kwake na kutumia kama nishati ataweza kutumia nishati za gesi au umeme ambazo atalazimika kununua?

Hoja inayokuaja hapa ni gharama ndio kikwazo. Mtungi wa gesi wa kilo sita unabadilishwa kwa wastani wa Sh20,000, Je, Watanzania wangapi wanaweza kumudu gharama hizi kila wiki au kila mwezi?

Mwaifwani anasema watu wasio na uhakika wa kula, wakipata chakula watakipika kwa nishati ya bei ya chini zaidi. Ni rahisi kwa mchumi wa chuo kikuu kusema nishati nafuu ni gesi, akakupa na namba kwa kusema unahitaji mkaa wa Sh1,000 kupika ugali.

Baada ya ugali kuiva ule moto unaoteketea bila matumizi ni hasara na zile Sh1,000 za kila siku ukizijumlisha ni gharama kubwa kuliko mtungi wa gesi wa Sh52,000 unaoweza kuuzima baada ya kupika; kudhibiti upotevu wa nishati. Ni rahisi kusema hivi.

Hata hivyo, nani anayo Sh52,000 mara moja gesi iishapo? Lakini wengi wanamudu mkaa wa Sh1,000, kesho itajisumbukia yenyewe, siyo kwamba hawaijali kesho, wanajali ila hawana hela. Ni suala la maisha halisi, siyo uwingi wa maneno ya motisha. Kama ni maneno, wanaoongea ni wengi, lakini bosi ni hela.

Turudi kwenye umeme. Wakazi wa Dar es Salaam ni mfano kuwa Mtanzania anaogopa kupika maharage kwenye umeme; anatumia umeme wake kuwasha taa, kuangalia runinga na kuchaji simu. Siyo kupika makande.

Tuna malengo mazuri ila kuna kazi kubwa kwenye kuyafikia kutokana na uhalisia wa hali za Watanzania.

Hata hivyo hakuna lisilowezekana na muda ni mwamuzi mzuri wa kama tutafika ama hatutofika kwenye nishati safi ya kupikia.