Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau mguu sawa nishati safi ya kupikia

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akimkabidhi mtungi wa gesi ya kupikia mmoja wa mama lishe kutoka Mbagala, Dar es Salaam katika hafla inayohamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Picha na maktaba.

Muktasari:

Mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mei 8 mwaka huu, ukilenga kuepuka athari za matumizi ya kuni na mkaa.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha mkakati wa miaka 10 wa matumizi ya nishati safi ya kupikia unatekelezwa kwa ufanisi, wadau wameeleza namna walivyojipanga kuufanikisha.

Mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mei 8 mwaka huu, ukilenga kuepuka athari za matumizi ya kuni na mkaa.

Baadhi ya wadau wameeleza njia na mbinu watakazozitumia kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya gesi kwa urahisi na bei nafuu ili kuepukana na matumizi ya nishati chafu.

Njia hizo ni kusambaza gesi katika maeneo ya vijijini, kuweka teknolojia itakayowezesha wananchi kununua gesi kama ambavyo wananunua nishati ya umeme kwa mfumo wa luku.

Wameeleza hayo leo Mei 17,2024 Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari katika mkutano wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais- Ikulu, Zuhuru Yunus aliyekuwa akitoa mrejesho kuhusu ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa alikoshiriki mkutano wa nishati safi ya kupikia kwa Afrika.

Katika ziara hiyo, Rais Samia alikuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano huo wenye lengo la kuipa kipaumbele sekta hiyo katika anga za kimataifa na kuwepo na sera katika nchi mbalimbali.

Rais Samia alishiriki mkutano huo kutokana na mchango wake mkubwa katika kuifanya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele chake cha kimataifa.

Katika mkutano huo wanahabari waliuliza maswali yakiwamo kuhusu gharama kwa Watanzania wanaoanza kutumia gesi na upatikanaji wa uhakika wa gesi hasa katika maeneo ya vijijini.

Kutokana na maswali hayo, Zuhura aliwainua wadau hao walioeleza mikakati ya taasisi zao katika suala la zima la nishati safi ya kupikia ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono mpango mkakati wa miaka 10 unaotaka hadi kufikia asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Mkuu wa Maendeleo ya Biashara na Ukuaji wa M-Gas, Abdallah Kijangwa amesema wameandaa teknolojia itakayowezesha Watanzania wa hali ya chini kununua au kutumia nishati safi ya kupikia.

Amesema ili kutumia nishati safi ya kupikia inakulazimu kuwa na mtungi na kununua gesi, hivyo kwa kutumia teknolojia ya mita janja katika mtungi wa gesi watawezesha upatikanaji taarifa za matumizi ya gesi hivyo kulipia kulingana na matumizi.

“Tumeangalia Watanzania wengi hata mkaa hawawezi kununua gunia zima, sasa tunaenda kumgusa hadi yule anayenunua mkaa wa Sh2,000 kwa sababu gesi yetu mtu atakuwa na uwezo wa kununua kuanzia Sh1,000,” amesema.

“Mtungi wa gesi utakaofungwa ‘mita janja’ tutakupa bure na kuuweka nyumbani kwako. Mwananchi atalazimika kununua jiko la gesi au kukopa kwetu kwa miaka miwili na kulipa kidogo kwa kila wiki Sh625,” amesema.

Kijangwa amesema kwa mwananchi atakayehitaji huduma hiyo wataenda kwenye makazi yake kupata taarifa, ikiwemo mazingira na mahali pa kufunga vifaa vyao kwa usalama.

Amesema kwa kuanza atalipa Sh30,000 kwa atakayehitaji jiko, kati ya hizo Sh20,000 itaenda katika jiko na Sh10,000 itawekwa katika gesi. Baada ya hapo atanunua gesi kwa kiwango anachohitaji kuanzia Sh1,000.

“Mita janja itakupa taarifa na sisi pia, kujua kiwango cha gesi kilichobakia ili tuje kukubalishia. Lile suala la kusema mtungi umeisha gesi tutakuwa tunaachana nalo, kwa sababu kuna watu maalumu watakakuwa wanafuatilia mwenendo wa matumizi kupitia mita janja,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria, Uhusiano na Utawala wa Total Energies, Getrude Mpangile amesema katika mkutano wa Paris kiongozi wa kampuni hiyo, aliuhakikishia ulimwengu kuwa wamejizatiti ifikapo 2030 watu milioni 100 wa Bara la Afrika na India wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Total Energies kwa Tanzania tumejizatiti kuhakikisha Watanzania wanapata nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu, tutawekeza katika teknolojia rahisi ya usambazaji wa gesi na elimu ya matumizi.

“Tutashirikiana na wadau watakaokuwa tayari, tutawezesha wajasiriamali na wabunifu wadogo wanaojihusisha na nishati safi ya kupikia. Katika kufanikisha mkakati wa Serikali wa miaka 10, uongozi umejizatiti kuwekeza Sh17 bilioni kwa mwaka ili kusambaza gesi katika maeneo yote nchini,” amesema.

Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Davis Deogtatius amesema mkakati wa Serikali wa matumizi ya nishati safi ya kupikia una nia njema katika Taifa kwa sababu unagusa afya na mazingira.

“Ili kuepukana na suala la gharama, Taifa Gas tumewekeza miundombinu katika maghala ili kuleta unafuu. Miundombinu ndiyo changamoto kuu inayosababisha gharama ya gesi iwe juu,” amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Seleman Jafo amesema mkutano wa nishati safi ya kupikia kwa Afrika hamasa yake ilitoka kwa Watanzania na Rais Samia ndiye alikuwa kinara.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema katika mkutano huo, Tanzania imeieleza dunia kuwa 2024 ndiyo mwaka wa kuleta mabadiliko mapya katika kupigania ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Kwa mujibu wa Zuhura, miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika mkutano huo ni ahadi za wadau wa maendeleo na mashirika binafsi yaliyoahidi kukusanya Dola za Marekani Sh2.2 bilioni, huku Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ikiahidi kutoa Dola za Marekani 2 bilioni kwa ajili ya nishati safi ya kupikia ndani ya miaka 10.

Wakati huohuo, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesaini mkataba wa makubaliano ya uwezeshaji wa kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi na uendelezaji wa mradi mdogo wa gesi kimiminika (Mini LNG), itakayosambazwa mbali na maeneo yaliyopita mabomba ya gesi.

Makubaliano ya ubia yaliyofikiwa jana kati ya TPDC, Rosetta na Africa 50 kwa uwekezaji katika mradi wa Mini LNG utaleta suluhu ya ufikishaji gesi asili katika maeneo ambayo bomba la nishati hiyo bado halijafika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana baada ya kuingia mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame amesema kumekuwa na changamoto ya kufikisha gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) na gesi asilia inayopita kwenye mabomba katika maeneo ya mbali, kwa sababu ya kukosekana kwa uwekezaji mkubwa ambao ungesambaza gesi nchi nzima.

"CNG unapoipeleka mbali zaidi ya kilomita 400 au 500 kiuchumi bei ambayo unakwenda kuuza inakaribia gharama ya kueneza, ili kuitatua changamoto ya kutoeneza mabomba nchi nzima tumeamua kuingia makubaliano na wenzetu," amesema.

Katika utekelezaji wa mradi huo amesema utakuwa wa mafanikio kwamba, hautahakikisha tu upatikanaji wa mapema wa gesi asilia kwa viwanda, kaya na magari bali utatangaza enzi mpya ya ufanisi wa nishati na uendelevu wa matumaini makubwa kwa sekta ya nishati nchini.

Huo ni mkataba wa pili kusainiwa kati ya TPDC na wawekezaji binafsi kwa ajili ya uwekezaji katika mradi wa Mini LNG baada ya uliotiwa saini Januari 2024 na KS Energy.

Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TPDC, Paul Makanza amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu kwani inaendana na mipango yao ya kuongeza usambazaji wa gesi asilia kufikia mikoa mingi nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rosetta Ernegy Solution, Karim Shaaban amesema kuingia mkataba huo ni katika kuunga mkono dira ya nchi katika kuwezesha usalama wa nishati kwa Taifa kwa bei nafuu na shindani.

Amesema uwekezaji huo utagharimu zaidi ya Dola milioni 100, na unalenga kuhamisha maarifa na ustawi wao kwenye soko la kutengeneza msururu wa ajira nchini, na kuwa wachangiaji wakubwa wa pato la ndani la Taifa.

Walichoteta Rais Samia na Macron

Katika hatua nyingine, Zuhura ameeleza walichozungumza na kukubaliana Rais Samia na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron walipokutana Mei 14 katika Ikulu ya Elysee jijini Paris.

Amesema masuala waliyozungumzia viongozi hao ni umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya nishati safi ya kupikia, maji, uwezeshaji wa wanawake, kilimo, biashara na uwekezaji.

“Uendelezaji wa miundombinu na masuala yanayohusu amani na usalama, Kaskazini mwa Msumbiji na Mashariki mwa Congo DR. Viongozi hawa wamekubaliana kutoa tamko linalobainisha azma ya Tanzania na Ufaransa kuimarisha ushirikiano katika sekta hizo,” amesema.