Wabunge kujadili mwongozo wa likizo kwa wanaopata watoto njiti

Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati akijibu maswali bungeni leo Jumanne, Februari 13, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Baada ya wadau wa afya ya uzazi kuiomba Serikali kuongeza ya likizo kwa wanaopata watoto njiti, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupeleka mwongozo bungeni.

Dodoma. Serikali itapeleka bungeni mwongozo wa ujumuishaji wa jinsia wa mwaka 2023 utakaojumuisha likizo kwa wanaume wanaopata watoto njiti, ili ujadiliwa na wabunge.

Hatua hiyo imeelezwa leo Jumanne Februari 13, 2024 na Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Santiel Kirumba.

Mbunge huyo amehoji iwapo Serikali haioni umuhimu wa kuwaongezea likizo ya uzazi kwa wanaume wanaopata watoto njiti kwa ajili ya kuendelea kuwatunza na kuwaangalia kwa ukaribu wake zao.

Akijibu swali hilo, Ridhiwani amesema Serikali imeandaa mwongozo wa ujumuishaji wa jinsia wa mwaka 2023 ambao pamoja na masuala mengine unazungumzia suala la likizo kwa wazazi wanaopata watoto njiti.

Amesema mwongozo huo unahusu pia kuingiza wanaume katika sehemu ya watu watakaochukua likizo katika kipindi hicho cha kusaidia kulea watoto njiti.

“Serikali italeta mwongozo huo ndani ya Bunge, tutajadili kwa pamoja na tukubaliane kimsingi ni njia gani ya kuwawekea wazazi hawa, ili tuweze kufikia ulezi bora usiochosha kwa mzazi mmoja,”amesema.

Katika swali la msingi, Santiel amehoji iwapo Serikali haioni haja ya kuwapa likizo ya uzazi ya zaidi ya siku 120 wanaojifungua watoto njiti, ili kuwa na muda wa kutosha kuwatunza watoto hao.

Akijibu, Ridhiwani amesema katika utumishi wa umma, likizo ni miongoni mwa haki za watumishi wa umma ambazo wanastahili kupewa na waajiri wao.

Amesema hiyo ni kwa mujibu wa kanuni H.12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma (2009), ikisomwa pamoja na Kanuni ya 97 ya Kanuni za Utumishi wa Umma (2022).

“Suala la likizo kwa mtumishi aliyejifungua mtoto njiti halijaelezwa bayana kwenye Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma,”amesema Ridhiwani.

Hata hivyo, amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 135 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022, linapotokea suala ambalo halikuelezwa bayana katika Kanuni za Utumishi wa Umma, mtumishi atamtaarifu mwajiri kuhusu suala husika.

Ridhiwani amesema mwajiri anaweza kutumia busara kulitatua na pale inapobidi, anaweza kutumia sheria zingine au kushauriana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi) kwa ufafanuzi wa suala husika ikiwemo nyongeza za siku katika likizo.


Takwimu njiti

Kwa muda mrefu sasa wadau wa afya ya uzazi na maendeleo ya jamii wamekuwa wakipaza sauti juu ya umuhimu wa Serikali kuwaongezea likizo wazazi wanaojifungua watoto njiti.

Wadau hao wanasema wanaojifungua wanalazimika kukaa muda mrefu wa hadi miezi mitatu hospitali, na wataalamu kuhitaji kufuatilia maendeleo ya watoto kila wiki.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha watoto njiti 210,000 huzaliwa kila mwaka nchini, huku 13,900 kati yao wakifariki dunia kwa kukosa huduma, huku Tanzania ikiwa ni nchi ya 12 kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto njiti duniani.

Taasisi ya Doris Mollel (DMF) ni miongoni mwa wadau wanaopigania suala la likizo ya uzazi kuongezwa kutoka miezi mitatu hadi sita kwa wanaojifungua watoto njiti tangu mwaka 2017.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Doris Mollel akifanya mahojiano na Mwananchi Agosti 19, 2023 alisema mwaka 2021 waliamua kuifanya ajenda ya mtoto njiti ikiwa na mambo makuu matano ambayo ni Serikali itenge bajeti, bima za afya na elimu juu ya mtoto njiti iingizwe katika somo la baiolojia.

Jambo lingine ni kuruhusiwa kwa waliojifungua kuwahudumia wakiwa hospitali na likizo ya uzazi, ili kuwezesha mama kumlea mtoto kwa utaratibu wa kangaroo kwa sababu tafiti na Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha ni njia nzuri ya kumtunza mtoto.

Hata hivyo, Doris anasema wamefanikiwa mambo matatu isipokuwa bima ya afya na kuongezwa kwa likizo ya uzazi ambayo liko kwenye mchakato mzuri wa kuwezesha marekebisho ya sheria.

Anasema kwa kushirikiana na wizara nyingine wamefanya uchambuzi wa sheria zinazoathirika kutokana na marekebisho hayo na kubaini kuwa zipo 13.

Doris anasema kinachosubiriwa sasa ni Serikali kutoa uamuzi kuhusu suala hilo kwa sababu uchambuzi na utafiti umeshafanyika na kwamba anatamani matokeo chanya ya harakati hizo angalau yaonekane mapema.