Wabunge waja na mbinu mpya kuzuia upigaji serikalini

Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga akizungumza wakati akichangia maoni kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 pamoja na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 bungeni jijini Dodoma jana. Picha na Merciful Munuo.

Dodoma. Wabunge wameibua sababu mbili za kutofikiwa malengo katika Mpango wa Maendeleo, kubwa ikiwa kutosomana mifumo ya makusanyo ya fedha na ufujaji wa mapato ya Serikali kwa baadhi ya watumishi.

Sababu hizo zilitolewa jana jijini hapa, Bunge lilipokaa kama Kamati kujadili Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2024/25.

Baadhi ya wabunge walieleza hayo yangedhibitiwa, Serikali ingekusanya mapato mengi na kuyatumia katika miradi ya maendeleo, huku wakishangazwa kuona mifumo haijawahi kuyumba wakati wa mishahara.

Mbunge wa Makete (CCM), Frank Sanga alisema kuna ombwe la kutokusomana mifumo ya makusanyo linalosababishwa na baadhi ya watumishi kutumia kivuli hicho kufuja fedha. Sanga alisema fedha zinazokusanywa kwa mtindo wa zamani zinakuwa kidogo zaidi ukilinganisha na mifumo ya kisasa.

Alitoa mfano wa ushuru unaotozwa Daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam, akisema awali zilikusanywa kati ya Sh150 milioni na Sh200 milioni kwa mwezi kabla ya kufunga mfumo, lakini sasa makusanyo yamefikia takribani Sh1.3 bilioni kwa mwezi, jambo linaloonyesha kulikuwa na upigaji.

“Mfano mwingine ni Hospitali ya Tumbi-Kibaha ambako makusanyo hayakuzidi Sh13 milioni au Sh12 milioni kwa mwezi, lakini tangu walipofunga mifumo wanakusanya hadi Sh350 milioni, ndiyo maana tunasema bado kuna tatizo. Tusipodhibiti hayo basi tutakuwa tumechagua kufeli,” alisema Sanga.

Kwa mujibu wa Sanga, hali ya kutosomana mifumo iko vivyo hivyo hata kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi na Ofisi ya Mapato (TRA), lakini kitendo cha baadhi ya halmashauri kuzima mashine za Posi kwa zaidi ya siku 1,000 kinathibitisha hilo.

“Hii itushtue kuwa mifumo haina changamoto, bali changamoto ni wale wanaoitumia. Mapendekezo yangu Serikali ihakikishe mifumo inasomana na inafanya kazi, kwa kuwa tunaweza kuifunga ila isifanye kazi,” alisema.

Naye Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu alisema Hospitali ya Taifa ya Bugando kabla ya kufungwa mifumo ilikuwa inakusanya Sh800 milioni, lakini sasa wanakusanya Sh3.5 bilioni, Hospitali ya KCMC walikuwa wanakusanya Sh300 milioni hadi Sh400 milioni, sasa wanakusanya Sh1.5 bilioni.

“Hii mifumo imefungwa na kampuni za Kitanzania, nakubaliana na Sanga, watu wanakataa mifumo kwa sababu ya rushwa na wizi,” alisema Kingu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ng’wasi Kamani alitilia shaka utekelezaji wa mpango wa maendeleo iwapo Serikali haitakuja na mbinu na mkakati kwa ajili ya kudhibiti wezi wa fedha za umma.

“Hatuwezi kufanikiwa, huwezi kuwa na maendeleo ikiwa unaingiza fedha katika mfuko uliotoboka, ni kweli bado kuna ombwe la matumizi ya fedha za umma, baadhi ya watumishi wamekuwa wakizitafuna fedha hizo bila huruma kwa hiyo hazitakaa kwenye maendeleo. Ni lazima tuwe makini kuziba mianya ya ufujaji huo ili tuweze kusaidia Taifa,” alisema Kamani.

Alisema haoni kama kuna dalili za fedha za mikopo ya asilimia 10 kutoka halmashauri kwa ajili ya kundi la vijana, wanawake na wenye ulemavu ambayo ilisitishwa ili Serikali ijipange upya kwa ajili ya kuboresha ukopeshaji.

Alisema Serikali iliahidi kuwa fedha hizo zingeanza kutolewa baada ya kufanya mageuzi na kuzitoa kupitia benki, lakini hakuna dalili kuwa mwaka wa 2023/24 zitatolewa.

“…hata humu kwenye mpango tunaona namna ambavyo kundi la vijana limesahaulika.

“Napata shaka kama vijana watapa mkopo katika mwaka huu wa fedha wa 2023/24 maana sioni dalili, lazima tujipange hata kwa haya wakati tunaendelea kuziba mianya hiyo,” alisema.

Mbunge wa Madaba (CCM), Dk Joseph Mhagama alisema Mpango wa 2023/24 utakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Dola unaosababisha wafanyabiashara kushindwa kuagiza bidhaa nje ya nchi.

Dk Mhagama alisema katika kipindi cha mwaka 2021/22 nakisi ya urari wa biashara imepanda hadi kufikia asilimia 54.8, akisema tatizo ni uagizaji mkubwa wa bidhaa kutoka nje ya nchi hata kwa zile ambazo hazikutakiwa kuagizwa huko.

Aliitaka Serikali kuwa makini kumaliza uhaba wa Dola kwa kuongeza bidhaa za kuuza nje ya nchi, zikiwamo madini, mazao ya misitu na utalii.

Alishauri Serikali iongeze kuuza nyama kwa ajili ya kushindana na nchi ya Brazil ambayo inauza zaidi ya tani 2.9 milioni wakati Tanzania inauza tani 10,000 pekee, licha ya wingi wa mifugo.