Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge wang’aka maadili ya wakusanyaji, waeleza chanzo upotevu wa mapato

Mbunge wa Viti Maalumu (CHAUMA), Devotha Minja, akizungumza wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Katika malalamiko hayo, wamesema sehemu ya fedha zinazokusanywa haziwanufaishi wananchi kutokana na vitendo vya ubadhirifu na kile walichokiita uporaji wa rasilimali za umma.

Dodoma. Baadhi ya wabunge wametaja mmomonyoko wa maadili kuwa miongoni mwa changamoto zinazochangia kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa mapato nchini, wakidai kuwa hali hiyo imechochea vitendo vya ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Kwa mujibu wa wabunge hao, sehemu ya fedha zinazokusanywa haziwanufaishi wananchi ipasavyo kutokana na vitendo vya ubadhirifu na kile walichokiita uporaji wa rasilimali za umma.

Wabunge hao walitoa hoja hizo wakati wakichangia mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27, unaotarajiwa kuhitimishwa mapema wiki ijayo.

Katika michango yao, baadhi ya wabunge walieleza kuwa pamoja na Serikali kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, bado changamoto za maadili kwa baadhi ya watumishi zinakwamisha juhudi za kuongeza mapato ya ndani.

Katika mchango wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja amesema Serikali inakabiliwa na changamoto katika ukusanyaji wa kodi kutokana na kile alichodai baadhi ya watendaji hutumia mabavu na makadirio yasiyozingatia uhalisia badala ya weledi wa kikazi.

Minja amesema licha ya Serikali kuendelea kutoa maelekezo ya kudhibiti vitendo hivyo, bado wafanyabiashara wengi wanaendelea kulalamikia makadirio makubwa ya kodi, kufungiwa biashara na hatua nyingine wanazodai si rafiki kwa mazingira ya biashara.

Alimtaka waziri mwenye dhamana kutazama kwa karibu malalamiko hayo, akieleza kuwa wananchi wengi wamekuwa wakitoa kilio kuhusu namna baadhi ya taratibu za ukusanyaji kodi zinavyotekelezwa.

Akitoa mfano wa uzoefu wake binafsi, Minja amesema aliwahi kukadiriwa kodi kwa kiwango alichodai hakikuakisi hali halisi ya biashara zake, hali iliyosababisha akaunti zake za benki kufungwa na fedha kuchukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Tunapaswa kujenga mfumo wa ukusanyaji wa kodi unaozingatia haki, uwazi na weledi ili kuongeza utii wa hiari wa walipakodi na kuimarisha mazingira ya biashara nchini,” alisema Minja.

Maelezo kama hayo hayo yalitolewa na Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas kuwa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu mfumo wa ukusanyaji kodi yamekuwa yakiongezeka, hali inayoashiria kuwa bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho.

Tarimba amesema changamoto kubwa inaanzia katika makadirio ya kodi, ambapo baadhi ya wafanyabiashara hudai kukadiriwa kiwango kisichoendana na hali halisi ya biashara zao.

Amesema mazingira hayo yamechangia baadhi ya wafanyabiashara kuamua kutotoa risiti za mauzo kwa lengo la kukwepa kodi.

Mbunge huyo alieleza kuwa wafanyabiashara wengi wanajikuta wakikabiliwa na shinikizo kutoka pande mbalimbali, jambo ambalo linaendelea kuzalisha malalamiko ndani ya sekta ya biashara.

“Wafanyabiashara wanapigwa kulia, wanapigwa kushoto na wanapigwa juu. Mwanzo mwisho watu wanalia. Hakuna urafiki wala undugu kwenye kodi, hii nchi tunaipeleka wapi?” alihoji Tarimba.

Ameitaka Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na mfumo wa ukusanyaji kodi ili kuongeza utii wa hiari wa walipakodi na kuondoa malalamiko yanayoweza kudhoofisha shughuli za kiuchumi nchini.

Si hao tu, hata Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe alipita humohumo, akisema wengi wa watumishi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawana weledi na mambo wanayoyafanya hayaendani na kile kinachohubiriwa.

Mafuwe amesema kuna maeneo watu wanalia ukubwa wa kodi wanazokadiriwa na hata namna wanavyodaiwa kodi hizo, bado mahusiano ya pande mbili yanaonekana kuwa madogo, bila kujua kwamba bila mfanyabiashara hakuna mapato.

“Lazima tuwaambie watumishi wetu kuwa, ubabe na kufunga biashara hautatusaidia, ni vema tutakaa chini na kuzungumza namna gani tunavyoweza kulisaidia Taifa hili na kila mmoja ajue kulipa kodi ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yake,” alisema Mafuwe.

Hata hivyo, Mbunge huyo alilalamikia alichokiita usumbufu wa kiwango cha karne kwa watu wanaoingiza bidhaa zao kwenye makontena katika bandari ya Dar es Salaam, ambayo alisema watu wanashikilia mioyo yao kabla ya kuchukua mizigo yao.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu, Neema Mwandabila yeye ameibua madai ya kuwepo kwa mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali inayochangiwa na baadhi ya watumishi wasio waadilifu, akitaka hatua kali zichukuliwe ili kulinda fedha za umma na kuhakikisha malengo ya Bajeti ya Serikali yanafikiwa.

Mwandabila amesema viongozi wa kisiasa na watumishi wa umma wana wajibu wa pamoja wa kulijenga taifa, lakini baadhi ya watumishi wamekuwa wakitanguliza masilahi binafsi badala ya masilahi ya nchi.

“Serikali inakusanya fedha nyingi na uwezo wa taasisi zetu za ukusanyaji mapato si wa kuhojiwa, lakini bado kuna mianya ya upotevu wa fedha katika ukusanyaji na matumizi yake. Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa, lakini baadhi ya watendaji hawamuungi mkono,” amesema Mwandabila.

Mbunge huyo ametoa mfano wa vitendo vya baadhi ya watendaji wa Jiji la Dodoma wanaodaiwa kuwataka wananchi kutoa fedha nje ya utaratibu rasmi baada ya magari yao kufungwa kwa madai ya makosa mbalimbali, jambo alilosema linapunguza mapato halali ya Serikali.

Amesema vitendo kama hivyo haviko Dodoma pekee bali hata katika maeneo mengine ya ukusanyaji mapato, ikiwamo Tunduma (Mbeya), na kwamba ni muhimu kwa Wizara ya Fedha kuweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji ili kuondoa mianya ya ubadhirifu.

Malalamiko kuhusu namna ukusanyaji kodi unavyofanyika si mapya, yamekuwepo tangu Serikali ya awamu ya tano, hadi ya sita, licha ya hatua mbalimbali ambazo Serikali imekuwa ikichukua.

Alipoingia madarakani mwaka 2021, Rais Samia alisisitiza mfumo wa kodi unaozingatia haki, uwazi na urahisi wa utekelezaji, huku ikitoa maelekezo kwa mamlaka za ukusanyaji mapato kuboresha mahusiano na walipa kodi na kuondoa vitendo vinavyoweza kukwamisha shughuli za kiuchumi.

Katika kipindi hicho, Serikali ilifanya maboresho mbalimbali ya kisheria kupitia Sheria za Fedha za kila mwaka, ikipanua matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa kodi, ikiwamo maboresho ya mfumo wa kielektroniki wa VAT na matumizi ya teknolojia katika kufuatilia miamala ya biashara.

Aidha, utawala wa Samia uliweka mkazo katika kupanua wigo wa walipa kodi ili sekta nyingi zaidi ziingizwe katika mfumo rasmi wa uchumi.

Serikali ilieleza kuwa sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi ilikuwa bado nje ya mfumo wa kodi, jambo lililosababisha mzigo mkubwa kubebwa na kundi dogo la walipa kodi.

Hatua nyingine ilikuwa kuanzishwa kwa Tume ya Rais ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi mwaka 2024, iliyopewa jukumu la kuchunguza changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa na wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla na mara kadhaa Serikali ilikutana na wafanyabiashara, wakiwemo wa Kariakoo kusikiliza malalamiko yao na kuahidi kuyafanyia kazi.


Uzalishaji zaidi

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge aliishauri Serikali kuelekeza nguvu katika sekta za uzalishaji, hususan kilimo na viwanda ili kuongeza ajira, mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Alitaka Serikali kuweka mkazo katika uzalishaji wa mafuta ya kula kwa kuhimiza kilimo cha alizeti, mawese, soya na karanga badala ya kuendelea kutegemea uagizaji wa mafuta kutoka nje, akipendekeza viwanda vinavyozalisha mafuta vipewe masharti ya kutumia malighafi zinazozalishwa nchini.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Catherine Joackim, amesema sekta ya umwagiliaji ina mchango mkubwa katika mageuzi ya kilimo na kuongeza pato la Taifa, hivyo akaitaka Serikali kuhakikisha fedha za miradi hiyo zinatolewa kwa wakati.

Mbunge wa Bukoba Mjini, Johnson Mutasingwa alisema ushirikishwaji wa walipa kodi katika utungaji wa sheria na utoaji wa elimu ya kodi ni muhimu kwa kuongeza mapato ya Serikali bila kuathiri mazingira ya biashara.

Mbunge huyo amesisitiza baadhi ya sheria hasa zinazokwamisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) zitazamwe upya, akisema baadhi ya mambo yanakidhana ndiyo panatokea mwanya wa upigaji kwa watu wasiokuwa na uaminifu.