Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yajibu Bunge la Ulaya kupinga msaada wa Sh480 bilioni

Muktasari:

  • Bunge la Ulaya limeitaka Tume ya Ulaya kuondoa mpango wa kutoa euro 156 milioni (sawa na Sh480 bilioni) kwa Tanzania mwaka 2026, likieleza kuwa masuala ya haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria bado hayajapatiwa ufumbuzi.



Dar es Salaam. Bunge la Ulaya limepitisha azimio la kupinga Tume ya Ulaya kutoa euro 156 milioni (takribani Sh480 bilioni) kwa Tanzania kwa mwaka 2026.

Hatua hiyo inayofungua sura mpya ya mvutano kati ya taasisi za Umoja wa Ulaya na Tanzania kutokana kinachoelezwa ni ukiukaji wa haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria nchini kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata.

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imejibu kwa kueleza, baadhi ya hoja zilizomo katika azimio hilo haziakisi uhalisia wa hali halisi ya Tanzania na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali baada ya matukio ya Oktoba 2025.

“Serikali ilitoa ufafanuzi wa kina kuhusu hatua hizo kwa Bunge la Ulaya na kwa wabunge wote wa Bunge hilo kabla ya upigaji wa kura. Hivyo, Serikali inasikitishwa kwamba pamoja na ukweli huo kujulishwa, hoja zilizo katika azimio hilo hazijazingatia ukweli huo,” imesema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Alhamisi June 18, 2026, Bunge hilo la Ulaya, limesema wabunge wake wanaamini Tume ya Ulaya imepuuza wasiwasi waliouibua miezi kadhaa iliyopita kuhusu mwenendo wa kisiasa nchini Tanzania.

"Wasiwasi wa wabunge wa Bunge la Ulaya haujashughulikiwa na Tume ya Ulaya," imesema sehemu ya taarifa hiyo katika kueleza msimamo wa Bunge hilo.

Baada ya hatua hiyo, suala hilo sasa linarudi kwa Tume ya Ulaya, ambayo ndiyo chombo chenye mamlaka ya utekelezaji ndani ya Umoja wa Ulaya.

Katika hatua hiyo, Tume italazimika kuamua ama kuondoa au kusitisha pendekezo la ufadhili au kuwasilisha kwenye Bunge hilo rasimu mpya yenye masharti yatakayohakikisha fedha zozote za EU zinatolewa kwa hakikisho la namna zitakavyotumika.

Hivyo, Bunge hilo pia limeitaka Tume hiyo kuondoa rasimu yake ya utekelezaji wa mpango wa ufadhili kwa Tanzania na kuwasilisha rasimu mpya itakayohakikisha kuwa hatua zozote zitakazochukuliwa hazitaathiri utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi, ulinzi wa haki za binadamu, demokrasia na ushiriki wa asasi za kiraia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wabunge wa Ulaya wanaona kuwa rasimu ilivyo sasa 'haiendani na sheria za Umoja wa Ulaya.'

Bunge hilo, limeeleza kuwa wasiwasi wake unatokana na matukio yaliyojitokeza baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, likidai kuwa Tanzania ilishuhudia ukandamizaji wa maandamano ya umma na changamoto za uwajibikaji kuhusu vifo na majeruhi vilivyotokea katika kipindi hicho.

Katika taarifa yake, Bunge hilo limesema idadi ya vifo vya watu katika vurugu za Oktoba ni zaidi ya 400 huku mamia wakikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini mahakamani.

Hata hivyo, idadi ya vifo vya matukio hayo ilitolewa na Tume ya Taifa ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025, iliyotolewa Aprili 23, 2026, ni kuwa watu wasiopungua 518 walifariki dunia katika matukio yaliyohusishwa na uchaguzi huo.

 Aidha, Bunge la Ulaya limeeleza wasiwasi wake kuhusu kuahirishwa mara kadhaa kwa ziara ya Kamati ndogo ya Haki za Binadamu ya Bunge hilo, iliyokuwa imepangwa kutembelea Tanzania kwa ajili ya kujadili masuala ya haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria.


Chanzo cha tatizo

Mvutano kuhusu ufadhili wa Tanzania ulianza Novemba 2025, Bunge la Ulaya lilipoitaka Tume ya Ulaya kusimamisha mchakato wa kuidhinisha msaada huo kufuatia wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa kisiasa nchini.

Licha ya kusitishwa kwa muda, Tume ya Ulaya baadaye iliwasilisha rasimu mpya ya utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa mwaka 2026, lakini ikibakiza kiwango kilekile cha Sh480 bilioni, hatua iliyozua pingamizi jipya kutoka kwa wabunge wa Ulaya.

Hatimaye, katika kikao chake cha Juni 18, 2026 Bunge hilo limepitisha azimio la kuitaka Tume hiyo kuondoa kabisa mpango huo na kuandaa mapendekezo mapya yatakayozingatia hoja zilizotolewa na wabunge.


Kauli ya Serikali ya Tanzania

Kutokana na uamuzi huo wa Bunge la Ulaya, Serikali ya Tanzania katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Ijumaa Juni 19, 2026 imesema imefuatilia na kubaini baadhi ya vyombo vya habari vinatoa habari zenye tafsiri isiyo sahihi kuhusu maana ya kura hiyo.

Katika ufafanuzi wake, Serikali imesema kura iliyopigwa si uamuzi wa mwisho wa Umoja wa Ulaya kuhusu Programu ya Ubia na Tanzania kwa mwaka 2026.

“Kura hiyo ni sehemu ya mchakato wa ndani wa taasisi za Umoja wa Ulaya ambapo Bunge hilo limetoa maoni na mapendekezo yake kwa mamlaka nyingine zinazohusika na maamuzi ya mwisho,” imesema.

Pia, imesema kinyume na baadhi ya taarifa zinazosambazwa, mapendekezo yaliyotolewa na Bunge la Ulaya si kusimamishwa kwa fedha hizo zinazotekelezwa au kutarajiwa kutekelezwa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kilichopendekezwa na Bunge hilo, Serikali imesema ni kufanyiwa mapitio programu hiyo na kuwasilishwa tena.

Aidha, kwa mujibu wa taratibu zilizopo mapitio yoyote ya programu ya ubia hufanyika kwa mashauriano na makubaliano ya pande mbili na hatimaye kuridhiwa kupitia Mkataba wa Pamoja wa Fedha kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya.

“Hivyo, maamuzi hayo si ya upande mmoja na hayatakuwa hivyo. Aidha, ni muhimu kwa umma kufahamu kuwa katika jumla ya Euro milioni 156 zinazozungumziwa, kiasi kilichokuwa kimepangwa kuelekezwa moja kwa moja serikalini kupitia mifumo rasmi ya Serikali ni Euro 17 milioni pekee,” imenukuliwa taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kiasi kilichobaki cha takribani Euro 139 milioni kilikuwa kimepangwa tangu awali kutekelezwa kupitia taasisi teule za Umoja wa Ulaya, taasisi za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na asasi za kiraia.

“Sehemu kubwa ya fedha za programu hiyo haikuwa imepangwa kuingia moja kwa moja katika mifumo ya Serikali,” imenukuliwa taarifa hiyo.

Aidha, Serikali imesema baadhi ya hoja zilizomo katika azimio lililopitishwa haziakisi kikamilifu ukweli na uhalisia wa hali halisi ya Tanzania na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali baada ya matukio ya Oktoba 2025.

“Serikali ilitoa ufafanuzi wa kina kuhusu hatua hizo kwa Bunge la Ulaya na kwa wabunge wote wa Bunge hilo kabla ya upigaji wa kura. Hivyo, Serikali inasikitishwa kwamba pamoja na ukweli huo kuwasilishwa, hoja zilizo katika azimio hilo hazijazingatia ukweli huo,” imenukuliwa taarifa hiyo.

Serikali imewahakikishia wananchi kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ni imara, wa kirafiki na wa kimkakati na unaendelea kuimarika katika maeneo mbalimbali yenye manufaa kwa pande zote mbili.

“Aidha, imesema pande hizo mbili zina mifumo rasmi ya kushauriana na kuwasiliana kwenye masuala yote yanayogusa mahusiano yao kila kunapokuwa na hitaji hilo.