Wachangishana Sh217 milioni kuboresha hospitali Rombo
Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda akikata utepe katika jengo linalojengwa katika Hospitali ya Huruma iliyopo wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.
Muktasari:
- Wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro wachangishana zaidi ya Sh217 milioni kwa ajili ya kuboresha hospitali ya Huruma iliyopo Rombo.
Rombo. Wakati Serikali ikiendelea kuboresha huduma za afya nchini, wadau kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wamechangishana zaidi ya Sh217 milioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya hospitali ya Huruma ili ipande hadhi na kuwa hospitali ya rufaa ngazi ya mkoa.
Akizungumzia hatua ambayo hospitali hiyo imefikia leo, Januari 28, 2024, daktari kiongozi wa hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, jimbo la Moshi, Dk Daria Mushi amesema mchakato huo ulianza mwaka 2022 na lengo lilikuwa kujengwa jengo la wagonjwa wa dharura katika hospitali hiyo.
Amesema hadi sasa zimeshatolewa Sh101 milioni kati ya Sh217 milioni zilizoahidiwa na wadau katika harambee iliyofanyika hospitalini hapo mwaka 2022.
“Jumla ya ahadi na fedha taslimu tulizopata ni Sh217 milioni na mpaka sasa tumepokea zaidi ya Sh101 milioni na tumepokea vifaa vyenye thamani ya Sh50 milioni na bado tuna ahadi ya Sh66 milioni ambazo hazijakamilishwa.
“Napenda kumpongeza kwa namna ya pekee Profesa Adolf Mkenda, mbunge wetu na kamati ya uratibu kwa kutuongozea harambee ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa kwetu,” amesema Dk Saria.
Naye mbunge wa Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewashukuru wadau waliojitokeza na kuchangia kiasi hicho cha fedha na kwamba kinachotolewa ni sadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine.
“Tunachochangia hapa ni sadaka ambayo inaweza kwenda kuokoa uhai wa mtu, tunawashukuru wale wanaoishika mkono hospitali hii, wapo ambao wanatoka ndani na nje ya Rombo tumeona namna wanavyotukimbilia.
“Sisi sio wanyonge, ujasiri mliouanza wa kuigeuza hospitali hii kuwa hospitali ya ngazi ya mkoa utafanikiwa, sio mzigo kwetu, ni baraka, kupata fursa ya kuchangia kitu ambacho kitaokoa maisha ya watu,” amesema mbunge huyo.
Hospitali hiyo ilianza mwaka 1968 katika Kijiji cha Ibukoni, wilayani humo, ikiwa umbali wa kilomita 80 kutoka Manispaa ya Moshi na mita 100 kutoka Makao Makuu ya Halmashauri ya Rombo.