Wadau wachangishana Sh132 kupiga jeki hospitali Rombo
Mbunge wa Rombo, ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda
Muktasari:
Mbunge wa Rombo, ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda pamoja na wafanyabiashara maarufu Mkoani Kilimanjaro wamejitolea na kuchangisha zaidi ya Sh100 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dharura na uzio kuzunguka hospitali ya Huruma iliyopo wilayani Rombo kwa ajili ya usalama wa wagonjwa na watumishi wa hospitali hiyo.
Rombo. Mbunge wa Rombo, ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda pamoja na wafanyabiashara maarufu Mkoani Kilimanjaro wamejitolea na kuchangisha zaidi ya Sh100 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dharura na uzio kuzunguka hospitali ya Huruma iliyopo wilayani Rombo kwa ajili ya usalama wa wagonjwa na watumishi wa hospitali hiyo.
Hospitali hiyo ambayo inamilikiwa na kanisa katoliki ilianzishwa mwaka 1968 na kuzinduliwa rasmi na Hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1970 ambapo mwaka 1972 hospitali hiyo ilipandishwa hadhi na kuwa hospitali teule ya wilaya ya Rombo na baadaye kuwa hospitali ya Wakala wa Hiari.
Akizungumza wakati wa harambee iliyofanyika hospitalini hapo, Daktari kiongozi wa hospitali hiyo, Sr Marrydaria Mushi amesema hospitali hiyo imekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa huo pamoja na nchi jirani husuani nchi ya Kenya kwa zaidi ya miaka 54.
"Ni matamanio yetu kupata jengo la dharura na vifaa muhimu vya tiba na uzio wa kuzunguka hospitali hii, hii itampunguzia mgonjwa maumivu na gharama za kutafuta matibabu mbali," amesema Sr Mushi
Amesema ili hospitali hiyo iweze kutoa huduma zilizokamilika na nzuri zaidi wanahitaji kuboresha jengo la kisasa la kuhifadhi maiti ambali litagharimu zaidi ya Sh183 milioni, jengo la mionzi ambalo litabeba mashine za X-Ray, Ultra Sound, ECG na ECHO ambalo litagharimu zaidi ya Sh242 milioni na X- Ray digital mashine ambayo ni Sh205milioni.
Aidha, amesema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya baada ya waliokuwepo kustaafu, kufariki na baadhi ya watumishi waliokuwa wameajiriwa na Halmashauri kupangiwa vituo vingine vya serikali.
Pamoja na mambo mengine amesema mpaka sasa hospitali hiyo imeweza kutoa msamaha wa gharama za matibabu ya wagonjwa wa makundi ya msamaha zaidi ya Sh.115milioni.
Naye mbunge wa Rombo, ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, amesema licha ya hospitali hiyo kufanya kazi nzuri licha ya kuwepo kwa changamoto hizo imekuwa ikifanya vizuri na kutoa huduma kwa gharama nafuu ikilinganishwa na hospitali nyingine binafsi.
"Menejimenti ya hospitali ya Huruma ni nzuri sana na wanafanya kazi katika mazingira hayo hayo na sisi sote ni mashuhuda, tunao uongozi mzuri sana, ahadi yangu tutazungumza na Wizara tuweze kupata watumishi ili hospitali hii iweze kuongeza kasi ya huduma kwa namna pekee ya kuhakikisha tunatoa huduma nzuri zaidi,"amesema Profesa Mkenda.
"Niwaombe Warombo na wasio wa Rombo na wenye mapenzi mema tushikane mkono tuisaidie hii hospitali iweze kusonga mbele zaidi, tunachofurahi ni ndoto kubwa kwamba sasa hii iwe ndio hospitali ya Rufaa kwa kiwango cha Mkoa,"
"Hata tukiwa na hospitali ya Wilaya tunayohakika kuwa Warombo wanaougua hapa wanaweza kupata huduma hapa hapa Rombo badala ya kuanza kukimbiza na usafiri mpaka KCMC,"amesema Profesa Mkenda
Profesa Mkenda ametoa wito kwa marafiki wote wa hospitali hiyo kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya kuisaidia hospitali hiyo ambapo pia amewashukuru wadau waliojitolea na kuchangisha zaidi ya Sh132milioni kwa ajili ya ujenzi huo.