Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau haki za binadamu wajitosa sakata la kukamatwa kina Slaa

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga

Muktasari:

  • Siku chache baada ya sakata la kukamatwa kwa Wakili Boniface Mwabukusi pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu Dk Wilbroad Slaa na Mdude Nyagali, watetezi wa haki za binadamu nchini wameungana kwa pamoja wakilaani kitendo hicho huku wakipinga kosa la uhaini wanalotuhumiwa nalo wanaharakati hao.

Dar es Salaam. Wadau wa haki za binadamu leo Jumanne Agosti 15, 2023 wamelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia watu wote wanaodaiwa kukamatwa na jeshi hilo kwa kuhusianishwa na ukosoaji wao katika mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA).

Akisoma taarifa hiyo ya pamoja ya wadau hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga amedai kuwa kati ya waliokamatwa wakihusishwa na ukosoaji wao ni pamoja na; Dk Willbroad Slaa, Peter Madeleke, Boniphace Mwabukusi na Mdude Nyagali.

Wadau hao walioungana kwa pamoja ni Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

"Kama ilivyofanyika kwa Wakili Boniface Mwabukusi na Nyagali, Dk Slaa alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi lakini baadae tuhuma zikabadilishwa na kuhojiwa tena kwa tuhuma za uhaini," amesema Henga.

Amesema kitendo hicho ni kinyume na kanuni za kimataifa za upelelezi wa makosa ya jinai.

Akisoma tamko hilo, Henga ametoa wito kumtaka Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati suala hilo ili watuhumiwa waachiwe bila masharti kwani ni dhahiri kwamba hawajatenda kosa la uhaini hata kidogo kulingana na masharti ya kosa hilo.

Pia wamelitaka Jeshi la Polisi kuheshimu haki na uhuru wa kutoa maoni huku wakisisitiza mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande kuhusu mfumo wa haki jinai nchini yaheshimiwe.

"Tunatoa wito kwa wanasiasa kuachana na kutoa matamko ambayo wakati mwingine hupelekea uvunjifu wa haki za binadamu kupitia Jeshi la Polisi," amesema Henga.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) Ananilea Nkya amesisitiza kuwa kosa la uhaini halijafanywa nchini kwa miaka mingi huku akiwataka Jeshi la Polisi kuwa makini na matamko yanayoweza kuchafua taswira ya nchi.