Wadau wachambua bima ya afya kwa wote, Waziri ajibu

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

Chama cha ACT-Wazalendo kimesema ili kuwe na bima ya afya inayozingatia usawa, iwe fao kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii mfumo utakaoifanya Serikali na wananchi kuchangia kwa pamoja.


Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema ili kuwe na bima ya afya inayozingatia usawa, iwe fao kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii mfumo utakaoifanya Serikali na wananchi kuchangia kwa pamoja.

Chama hicho kimeeleza lengo la mfumo huo ni kuondoa matabaka katika utoaji wa huduma kwenye sekta ya afya.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Januari 25,2023 na Waziri kivuli wa sekta ya afya ya ACT Wazlendo, Dk Elizabeth Sanga katika mjadala wa Twitter Space ya Mwananchi.

Mjadala huo unaohudhuriwa na wananchi, wataalamu wa afya wa sekta binafsi na Serikali akiwemo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, wenye mada isemayo ‘mambo gani muhimu yazingatiwe katika bima ya afya kwa wote.”

Dk Sanga amesema mfumo huo utamkinga mwananchi kuingia kwenye umasikini kutokana na Serikali inamwekea akiba.

“Muswada wa sheria umeacha mzigo mkubwa wa ugharamiaji kwa wananchi, pia hauna usawa kuna matabaka kwenye matibabu, kuna watu watakuwa wanatibiwa kwenye vituo vya afya na watakaohitaji kwenda hospitali za mikoa kutakuwa na changamoto za kulipia,” amesema

Dk Sanga amesema mfumo wa bima ya afya wa sasa hautoi kinga ya uchumi kwa wananchi.

Amesema muswada unahitaji mapinduzi ili kupatikane kwa mfumo mzuri wa kugharamia matibabu kwenye sekta ya afya.

Akijibu suala la matabaka, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema, bima hiyo ya afya haitakuwa na matabaka yoyote kwani wamefanya utafiti kwa kutumia wataalamu wawili kutoka nje kuwafanyia mahesabu ya gharama.

Amesema lengo la Serikali,”hatutamwacha mtu nyuma katika hili na tutakuwa makini.”

Awali, Herieth Makwette, Mwandishi wa habari za Afya gazeti la Mwananchi amesema hofu kubwa ya wananchi sasa kufika vituo vya afya kupata huduma ni gharama akisisitiza umuhimu wa bima ya afya.

Naye Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema Serikali inapaswa kuangalia ni namna gani itawahusisha wananchi wengi na mfumo wa bima ya afya akisisitiza wagonjwa wengi wasio na uwezo wa kulipia huduma za afya ni mzigo kwenye sekta ya afya.

Maoni hayo ya wadau yanakuja wakati Serikali tayari imeweka bayana kwamba, Februari 2023 itawasilisha bungeni kwa mara muswada huo baada ya mwaka jana kushindwa kuindia bungeni na kujadiliwa kisha kupitishwa.