Wadau waeleza matamanio muda uliosalia wa Rais Samia

Muktasari:

  • Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imeendesha mjadala wa X-Space na kuwakutanisha wadau mbalimbali kuzungumzia muda uliobaki wa utawala wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Wamegusia matamanio yao wanayotaka kuona yakifanyika.

Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya siasa na uchumi nchini wametaja mambo saba wanayoyatarajia katika muda uliobaki wa uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ikiwemo suala la kushuka kwa gharama za maisha, uwajibikaji na kukamilika kwa miradi ya kimkakati inayoendelea nchini.

Mambo mengine kuimarika kwa diplomasia ya uchumi, uchaguzi huru na haki, ujenzi wa taasisi imara za Serikali na kupunguza ziara za nje ya nchi.

Kupanda kwa gharama za maisha kunatajwa kuongeza pengo baina ya wenye nacho na wasio nacho huku wananchi wakipitia changamoto ya kupanda kwa bei ya vyakula, mafuta, sukari na bidhaa nyinginezo, vitu ambavyo wadau wameweka mategemeo ya kuwepo kwa utulivu ndani ya muda wa miaka miwili iliyobaki.

Hata hivyo, matumaini yaliyopo kwenye uwajibikaji ni hatua kali dhidi ya viongozi wanaobainika kupora mali za umma na mara kadhaa Rais Samia alitarajiwa kuwawajibisha wahusika, lakini hawaoni hatua anazochukua licha ya kuahidi kufanya hivyo.

Vilevile, eneo miradi ya mikakati ambayo wadau hao wameweka shauku ya kumuona Rais Samia akikamilisha ndani ya muda uliobaki, ni ile iliyoanzishwa na mtangulizi wake hayati Rais John Magufuli hasa mradi wa umeme wa Bwawa la Nyerere na Mradi wa Reli ya kisasa (SGR).

Mategemeo hayo ya wadau wameyaelezwa leo Jumatano, Machi 20,2024 kwenye mjadala wa Mwananchi X space ukiwa na mada isemayo “Nini matarajio yako kipindi kilichobaki cha uongozi wa Rais Samia?

Akichokoza mada kwenye mjadala huo, Mhariri wa Jarida la Saiasa wa gazeti la Mwananchi, Peter Elias amesema matarajio aliyoanayo kwa kiongozi huyo mkuu wa nchini kuimarisha zaidi Amani.

“Natamani kwa miaka miwili iliyobaki adumishe suala la amani, tunataka amani ya mtu mmoja mmoja, mtu akikaa awe huru kutoa maoni yake kusiwe na kitu kibaya cha kumtokea,” amesema.

Elias anaongeza jambo la pili analotarajia ni kushuka kwa gharama za maisha kwani ni vigumu kuachanisha uchumi wa wananchi na siasa, akisistiza siasa ziendelee lakini wananchi wawe na maisha bora.

“Kwa muda uliobaki, tunataraji kuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, natamani tuwe na uchaguzi huru na haki na huu ni mtihani uliopo mbele ya Rais Samia kuhakikisha haturudi tulipotoka miaka mitano hadi sita iliyopita,” amesema

Kwa upande wake, Msomi wa Siasa za Maridhiano Afrika, Ezekiel Kamwaga amesema ni Rais Samia anapaswa kujikita kutengeneza uhusiano mzuri na wananchi.

 “Matarajio yangu kwa muda uliobakia Rais anafanya zaidi ziara za ndani ya nchi kwa kutembelea mikoa ambayo hakufika na itasaidia kutengeneza mahusiano mazuri na wananchi na inawezekana iwapo atapunguza safari za nje ya nchi,” amesema.

Hoja nyingine imeibuliwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunga ambaye amesema kwa kipindi kilichobaki anatamani kuona kiongozi huyo anaweka uwazi na uwajibikaji serikalini kwa kuwa alifanya kazi sekta binafsi inayoamini kwenye dhana hiyo.

“Tunaona takwimu zinapeperushwa lakini haziakisi ukweli, mfano tumezungumza masuala ya vyakula, mafuta kuuzwa bei ya juu na tunajua mafuta yanaathiri mfumuko wa bei lakini ukifuatilia takwimu unazikuta zipo chini sana, sasa unajiuliza kuna uhalisia gani kwenye hili,” amesema.

Jambo lingine analotaja Mbunda amesema hivi karibuni Rais Samia alitoka hadharani na kutangaza uwepo wa mtandao unaochepusha fedha za Serikali akisema jambo alilopaswa kufanya ni kuchukua hatua na kuzitangaza na si kulalamika.

Katika ujenzi wa taasisi imara, alitolea mfano Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo inapaswa kuwa mlezi wa vyama vyote nchini akidai imekuwa ikilalamikiwa hasa kuviminya baadhi ya vyama.

“Katika ujenzi wa taasisi, mfano Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa inapaswa kuwa ya ulezi lakini inavyofanya kazi inaonekana kama ofisi ya nyapara na vyama vingi vya siasa, vingi vimekuwa vikiilalamikia,” amesema.

Kwa upande wa uimarishaji wa diplomasia, Mchambuzi na Mtafiti wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Abbas Mwalimu amesema lazima Serikali itumie Tehama katika nchi ambazo hazina balozi.

“Ubalozi wetu wa Abuja nchini Nigeria unahudumia nchi 12 kitaalamu naona unampa mzigo mkubwa yule anayetekeleza majukumu yake, hii ni changamoto ambayo inapaswa sasa tujikite kwenye teknolojia.

“Mfano kuvunjika kwa uhusiano baina ya Marekani na Iran mwaka 1979 ilipofika 2011 Marekani walizindua ubalozi wa kuwasiliana na wananchi wa kule pasipo kufungua ubalozi kule, nafikiri kama Tanznaia tunaweza kujielekeza huko ili kuondoa changamoto hizo na hatimaye tuwe na diplomasia ya uchumi itakayofanikiwa kwa kiasi kikubwa,”amesema.

Pia Mwalimu amesisitiza juu ya kuwepo kwa taasisi moja inayofuatilia mikataba inayosainiwa na nchi kimataifa, akitolea mfano sasa mambo yanayohusu nchi nje ya nchi inashughulikiwa na Wizara ya Mmabo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu.