Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau waliomba Bunge kupitisha Muswada wa Haki za Kidigitali

Muktasari:

Wadau kutoka asasi za kiraia, wasomi, wanasheria na waandishi wa habari wameliomba Bunge kupitisha Muswada wa Haki za Kidigitali unaolenga kuwalinda watumiaji wa mitandao wakiwemo watoto pindi utakapofika bungeni.

Wadau kutoka asasi za kiraia, wasomi, wanasheria na waandishi wa habari wameliomba Bunge kupitisha Muswada wa Haki za Kidigitali unaolenga kuwalinda watumiaji wa mitandao wakiwemo watoto pindi utakapofika bungeni.

Maombi hayo yametolewa na wadau hao jana jijini Dar es Salaam katika mkutano uliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Paradigm Initiative uliyowakutanisha kwa lengo la kujadili muswada huu.

Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, Wakili Salma Kassim kutoka Kampuni ya Infinity Excellence Ltd alisema Muswada huo ukijadiliwa na ukapita kuwa Sheria utasaidia ulinzi wa haki za mtumaji wa mtandao na kutengeneza wajibu kwa mtumiaji kulinda na kuheshimu usiri wa mtu mwingine.

“Tunaamini muswada huu pindi utakapokamilika na kupelekwa bungeni, wabunge wataupitia na kuupitisha kwa kuwa una lengo la kumlinda kila mtumiaji wa mitandao ya kijamii akiwemo mtoto mdogo,” alisema

Aidha alisema bado kumekuwapo na changamoto kwa vijana wengi kushindwa kutumia mitandao kama sehemu ya kujiingizia kipato na kujikwamua kiuchumi badala yake uitumia kwa kufanya mambo yasiyofanya katika jamii.

Akizungumza kutoka nchini Kenya kwa njia mtandao, Mratibu Mkuu wa Mradi Afrika Mashariki wa Paradigm Initiative Ekai Nabenyo alisema wana amini kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan utaupokea muswada huo na kuujadili na hatimaye utakuwa sheria yenye kulinda haki za kidigitali zikiwemo masuala ya faragha na uhuru wa mtumiaji.

“Tunatambua kuwa Tanzania kuna majadiliano kuhusu sheria ya faragha hivyo tunawasihi Watendaji na Bunge kuharakisha michakato ya sheria kama hizo ili kuhakikisha usalama wa data na haki za dijiti kwa watanzania wote unakuwepo.

“Kama Shirika la haki za digitali za Pan-Afrika, tumekuwa mstari wa mbele kukuza ushirikiano kati ya Serikali na asasi za kiraia barani Afrika. Ushirikiano kama huo ulisababisha kuanzishwa kwa Muswada wa Haki za Digitali na Uhuru nchini Nigeria.” alisema

Alisema mambo hayo yatawezeka endapo tu kila raia, asasi za kiraia, na serikali inafanya kazi pamoja katika kuunda siku zijazo, kupitia hatua za sera zinazounga mkono uvumbuzi na kulinda watu kama vile Muswada wa Haki za Digitali na Uhuru wa Tanzania 2021.

Awali Mwezeshaji wakati wa mkutano huo, Peter Mmbando alisema Muswada huo ni muhimu na umekuja wakati muafaka hasa kwa kuzingatia kumekuwepo na matumizi makubwa   ya mtandao katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Alisema ni muhimu kuwepo na miongozo ambayo itawafanya watumiaji mbali ya haki zao kulindwa wajue ni aina gani za maudhui ambazo wanaweza kuweka mtandaoni bila kuvunja sheria.