Wadau watofautiana ujuzi wa kufanyakazi wahitimu wa vyuo vikuu
Muktasari:
Wakati tukijiandaa kwa tukio hilo la kihistoria, tunakuletea mfululizo wa makala zinazohusu changamoto na fursa zilizopo. Leo tunakuletea maoni ya wadau kuhusu ujuzi wa wahitimu kufanikisha dhamira hiyo. Endelea...
Takwimu zinazoonyesha zaidi ya wahitimu 800,000 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka lakini ni takriban asilimia 10 pekee ndio hufanikiwa kuajiriwa ni miongoni mwa changamoto inayoumiza vichwa vya wadau wa ajira na kazi nchini.
Miongoni mwa sababu zinazoelezwa kuchangia tatizo hilo ni kukosekana kwa ujuzi miongoni mwa wahitimu wengi jambo linalowapa wakati mgumu waajiri ambao hulazimika ama kutafuta wajuzi kutoka nje ya nchi au kuwapa mafunzo kazini suala linaloongeza gharama.
Kutooana kwa taaluma za wahitimu na mahitaji ya waajiri ni suala linaloendelea kujadiliwa huku mapendekezo kadhaa ya kupata suluhu ya kudumu yakitolewa.
Utafiti wa kamisheni ya mipango ya Ofisi ya Rais wa mwaka 2014 unaonyesha asilimia 80 ya nafasi mpya za ajira zinahusu sayansi na hisabati masomo ambayo wahitimu wengi ama hawayapendi au walifanya vibaya kwenye mitihani yao kidato cha nne au cha sita.
Ripoti hiyo ilibainisha tofauti iliyopo kati ya mahitaji na maandalizi yanayofanywa kwenye vyuo vinavyowapika wahitimu wanaotarajiwa kuingia kwenye soko la ajira linalohitaji zaidi watalaamu wa masuala ya sayansi lakini wanaoletwa wengi hawakusoma kozi hizo.
Utafiti huo pia ulibainisha asilimia 79 ya wahitimu wote wanatarajiwa kuajiriwa na asilimia 17 wakisema wanataka kujiajiri. Wahitimu wengi hutumia zaidi ya mwaka mmoja kutafuta kazi.
Kukabiliana na changamoto iliyopo, zipo mbinu zinazotumika kuwapata wataalamu wanaohitajika. Miongoni mwa mbinu hizo ni kuajiri watu wenye ujuzi unaohitajika waliopo kwenye sekta husika, kuwafundisha wafanyakazi walipo, kuajiri kutoka nje ya nchi au kupata ushauri wa wataalamu.
Kampuni kadhaa nchini zinazo program za kuwaongezea ujuzi wahitimu wanaowaajiri. Coca-Cola Kwanza ni miongoni mwa kampuni hizo.
Meneja rasilimali watu wa kampuni hiyo, Neema Kingson anasema hutafuta wahitimu kutoka vyuo vikuu tofauti nchini na wale wanaokidhi vigezo huwapa mafunzo kwa mwaka mzima kabla ya kuwaajiri.
Kwenye mafunzo hayo, licha ya ujuzi unaohitajika, anasema mtazamo wa mfanyakazi kuhusu masuala tofauti yanayopewa kipaumbele na kampuni ni sual ajingine muhimu wanalolipa kipaumbele.
“Lazima uajiri ili kutekeleza sheria zilizopo,” anasema.
Miaka minane iliyopita, kampuni ya Acacia ilikuwa inakabiliwa na uhaba wa watalaamu wa maeneo tofauti ya operesheni zake kuanzia mafunzi mpaka wahandisi, wajiolojia hata watabiri wa hali ya hewa.
Meneja mkuu anayeshughulikia ufanisi, Janet Reuben anasema: “Kulikuwa na changamoto kubwa hasa upatikanaji wa mafundi. Ilikuwa unaweza kumpata mtu mwenye vyeti, amefaulu vizuri lakini hawezi kufanya kazi.”
Kukabili changamoto hiyo, mwaka 2010 Acacia iliingia ubia wa Dola 2 milioni za Marekani Mamlaka ya Elimu na Ufundi (Veta) Moshi kufanikisha mafunzo ya mafundi wa madini.
Mpaka sasa, mafundi 708 wamenufaika na mpango huo huku 402 kati yao wakiajiriwa na kampuni hiyo inayoongoza kwa uchimbaji wa dhahabu.
“Septemba mwaka jana jukumu hilo lilikadhibiwa Veta lakini Acacia itaendelea kutoa fedha kufanikisha mafunzo hayo,” anasema Janet.
Hata wadau wa sekta ya kilimo nao wana kilio hicho hicho. Mkurugenzi wa idara ya rasilimali watu ya kampuni za Bakhresa (BGC), Maryam Bayumi anasema unga ndio biashara yao mama lakini haina watalaamu wa kutosha nchini.
“Tunatumia teknolojia ya kisasa sana kusaga unga hivyo kuhitaji wataalamu wa fani hii ambao hawapatikani nchini,” anasema Maryam.
Kampuni hiyo, anasema inashirikiana na vyuo vya nje kufanikisha mafunzo ya watumishi wake ili kuendesha na kuimaia mitambo ya kisasa iliyopo.
Kujiajiri
Tofauti na mtizamo wa wahitimu wengi, Elia Mkongwa anaamini kwenye uwezo alionao ambao umeongezewa amakali na vyuo alivyosoma.
Baada ya kutengeneza mashine kadhaa ikiwamo ya kupandia mbegu za mazao tofauti hasa nafaka, Mkongwa anapanga kutengeneza gari kwa ajili ya maharusi litakalokuwa kama ndege.
Mashine hiyo ya kupandia ina uwezo wa kupanda eka tano ndani ya nusu hivyo kuokoa muda ambao ungetumi wa na watu kadhaa kuifanya kazi hiyo.
Licha ya hiyo, mbunifu huyo ametengeneza mashine ya kutotolesha vifaranga 200 inayotumia nishati ya umemejua. Kazi hizi, licha ya kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii inayomzunguka, zilimfanya anyakue tuzo ya mbunifu bora mwaka 2015 jijini Nairobi iliyotolewa na Youth Talent Centre.
“Nina mawazo mengi ya kuyafanyia kazi. Kadri navyopata nafasi natekeleza moja baada ya jingine,” anasema mhitimu huyo wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Veta.
Mbunifu huyo anaamini vijana wengi wana ujuzi ila hawapewi nafasi ya kuonyesh auwezo wao kwenye taasisi na kampuni zilizopo ambazo hueneza taarifa za kukosa wataalamu wanaohitajika miongoni mwa wahitimu wanaoomba kazi.
Wadau
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Emmanuel Mjema anasema ingawa hawezi kupinga maoni ya wadau wanaolalamika kuhusu ukosefu wa ujuzi miongoni mwa wahitimu ila anaona kuna chumvi inaongezwa.
“Haiowezekani kumlinganisha mhitimu na mfanyakazi mwenye uzoefu wa miaka 10 kwa mfano. Hata hivyo, uandaaji wa mitalaa ya chuo kikuu huwashirikisha wadau muhimu wakiwamo waajiri ili kukidhi mahitaji ya soko,” anasema.
Kupata suluhu ya kudumu, profesa huyo anawaasa waajiri kuutumia ushauri wa wasomi kupata waajiriwa wenye utalaamu unaohitajikakufanikisha biashara zao.