Waelezeni ukweli watoto kuhusu ukatili-wito

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Msingi miembe saba mjini Kibaha wakifuatulia mafundisho ya madhara ya ukatili kwa watoto yanayorushwa shuleni hapo kwa njia ya sinema (haipo pichani). Picha Julieth Ngarabali.

Muktasari:

  • Yaelezwa watoto wakielimishwa thamani ya miili yao, wakipewa upendo na haki ya kujieleza, kuwajenga kujiamini  na hata kueleza ukatili watakaofanyiwa.

Kibaha. Ikiwa wazazi na walezi wa watoto  wa umri  chini ya miaka nane wakijenga utamaduni wa kuwa karibu na watoto hao na kuwapa upendo na  haki ya kujieleza, kunaelezwa ni moja ya njia rahisi na rafiki  kwao kusema yanayowakabili ikiwemo vitendo vya unyanyasaji na ukatili.

Pia wanafamilia ni vema  kuwaelewesha  watoto  hao  thamani ya miili  yao na umuhimu wa kuulinda  usichezewe na mtu yeyote ndani ya familia na nje wawapo shuleni.

Hayo yamesemwa na wazazi mjini Kibaha leo Jumatatu Desemba 4, 2023 wakizungumza na Mwananchi Digital  kuhusu matukio ya ukatili yanayojirudia mara kwa mara kutendewa watoto huku adhabu zikitangazwa kutolewa kwa wahusika, lakini bado inaripotiwa  baadhi  ya wazazi, walezi na ndugu wanawatendea  ukatili ikiwemo kuwachoma moto sehemu za miili.

Wametolea mfano tukio la hivi karibuni  lililotokea eneo la Boko Kibaha ambapo

Asnah Mohamed (62) mkazi wa eneo hilo alidaiwa kumchoma moto mjukuu wake mwenye umri wa miaka mitano  anayesoma darasa la kwanza  kwa tuhuma ya kuiba  Sh2,000.

Mtoto huyo alikuwa akiishi na bibi yake huyo baada ya mama yake mzazi kuolewa na mwanaume mwingine, tayari ameshapata matibabu hospitali ya Tumbi na pia  mtuhumiwa ameshafikishwa mahakamani

"Matarajio yetu sasa hii  miradi ya usalama wa watoto (Uwawa) ulioanza Pwani kwa lengo la kuimarisha usalama wa watoto na Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto (PJT- MMMAM ),  unaolenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto wa miaka 0-8,  ilete tija katika matukio haya pia," amesema Amina Sefu.

 Wameshauri utekelezaji wa miradi hii ushuke  ngazi za chini vijijini kabisa walipo wazee  na rika za kati wasio na elimu  na wasiojua  kiuhalisia kuwa  ukatili siyo kumbaka au kumlawii tu hata kumpiga kipigo hatarishi au kumtia  jeraha  pia ni kosa.

"Makuzi ya mtoto yanaenda na matamanio ya kujifunza kila kitu. Lazima tuwe karibu kufatilia makuzi licha ya ubize tulionao  tutenge muda maana mtoto akishaingia kwenye tabia hatarishi kumrudisha ni ngumu, vivyo hivyo akifanyiwa ukatili  hatuwezi kuufuta kwenye ubongo wake,"amesema Bahati Kusubila.

Huruma Ibrahim mkazi wa Picha Ndege  amesema jamii inatakiwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto kwa kumuondolea vikwazo wasifokewe wasijengewe uoga ili ajiamini na kutoa taarifa kwa wakati  ya wanaowafanyia ukatili hivyo kupata ushahidi usio na shaka kwa wakati  bila gharama kubwa ya muda ama fedha.

Kwa mujibu wa takwimu za matukio ya ukatili Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2022,  matukio ya ukatili kwa watoto yalikuwa ni 12,163 kati ya hayo  yaliyofanyika kwa wavulana ni 2,201 na wasichana 9,962 ikilinganishwa na matukio 11, 499 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 5.8.

Ofisa ustawi wa jamii Kibaha Mjini, Mary Michael ametaja chanzo  ni wazazi kutelekeza watoto na kukosa malezi mema na kujiingiza kwenye vikundi hatarishi na kuomba ushirikiano kwa ngazi za jamii, Serikali, madawati ya jinsia na wadau ili kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo  kubakwa na kulawitiwa.

Meneja kanda ya Mashariki wa Taasisi ya Christian Social Services Commission (CSSC) inayojihusisha na usalama na haki kwa watoto , Makoye Wangeleja amesema vita ya unyanyasaji na ukatili kwa watoto siyo lelemama, watu wanaowafanyia vitendo hivyo ni ambao huwezi kuwafikiri na inabidi kujipanga  kukabili vitendo hivyo.

Katibu Tawala mkoani  Pwani, Rashid Mchatta amesema mkoa tayari umeshajipanga kuwalinda watoto na kuwachukulia hatua za kisheria  watakabainika kuhusika na matukio ya ukatili kwa watoto na tayari upo mradi wa usalama kwa watoto  na PJT –MMMAM.