’Chungeni watoto wakati wa likizo’

New Content Item (2)

Wananchi wa kata ya Sanya  juu Wilayani siha mkoani Kilimanjaro, wakimsikiliza Afande Daniel Nyolobi ikiwa ni uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili.

Muktasari:

  • Ni wito unaowataka wazazi na walezi kuwa makini dhidi ya vitendo vya ukatili a udhalilishaji kwa watoto.

Siha. Zikiwa zimebaki siku chache wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari waanze likizo, wazazi na walezi wametakiwa kuweka mpango mkakati wa kufahamu ratiba za watoto wao wakiwa nyumbani ili kuwalinda na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Rai hiyo imetolewa leo Alhamisi November 30, 2023 na Ofisa Maendeleo ya Jamii, Marc Masue wilayani hapa wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili ambapo kiwilaya umefanyika katika majengo ya soko la Sanya juu.

Masue amesema katika kipindi hiki shule zinakwenda kufungwa  na watoto watarudi nyumbani, usalama wao unakuwa mdogo tofauti na wanapokuwa shuleni kutokana na uhuru wanaoupata wakiwa nyumbani.

"Nawaomba kipindi hicho cha likizo tuweke utaratibu mzuri kunusuru watoto na kizazi chetu wabaki salama kama wanapokuwa shuleni ili kufikia malengo yao,"amesema Masue

Kwa upande wake, Idrisa Mndeme, mjumbe wa kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (Smaujata) wilayani Siha, amewataka wanaume kuacha matendo hayo ya kikatili kwa sababu ni chukizo kwa Mungu.

"Ni kweli watu tunaacha shughuli za kimaendelea na kuelekeza nguvu nyingi kupambana na vitendo hivyo ambavyo watu wana uwezo wa kuacha, acheni haya mambo haya,"amesema Idrisa.

 Aidha amewataka kinamama wafanyabiashara masokoni kuwa na ratiba za kukutana na watoto na kuzungumza nao.

Amesema ratiba hizo zitaweza kuwakutanisha na watoto kwa ajili ya kuzungumza nao mambo mbalimbali ya maendeleao ikiwamo changamoto zao hasa kwa kipindi hiki cha matendo ya ukatili kwa watoto yakiongezeka

“Nawaomba wazazi wenzangu tupange muda wa kuongea na watoto, hali ni mbaya leo unasikia mtoto amebakwa ,amelawitiwa tulinde kizazi mwishowe tusipokuwa makini tutakuwa na kizazi ambacho hakina mwelekeo. Hizo hela tunazotafuta zitakuwa hazina manufaa,”amesema.