Wadau wataja vikwazo vitano mapambano dhidi ya ukatili

Mkurugenzi wa Shirika Kivulini, Yassin Ally akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na wadau wa kupinga vitendo hivyo. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Wadau wa kupinga ukatili jijini Mwanza wametaja tabia ya kulindana, ukosefu wa usiri kwa watoa taarifa, ukosefu wa elimu, ukosefu wa rasilimali fedha na vifaa vya usafiri kuwa ni vikwazo katika kukabiliana na kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia katika jamii. 

Mwanza. Wadau wa kupinga ukatili jijini Mwanza wametaja tabia ya kulindana, ukosefu wa usiri kwa watoa taarifa, ukosefu wa elimu, ukosefu wa rasilimali fedha na vifaa vya usafiri kuwa ni vikwazo katika kukabiliana na kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia katika jamii. 

Wakizungumza leo Ijumaa Disemba Mosi, 2023 wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na mashirika ya kupambana na ukatili katika jamii, wameiomba jamii kushirikiana kufichua vitendo hivyo na kutoa ushirikiano kwenye kesi za namna hiyo. 

"Kama tukiwekeza rasilimali zetu na nguvu zetu katika kupinga ukatili naamini tutakomesha kabisa na katika kuwekeza huko tuendelee kutoa elimu kwa jamii yetu inayotuzunguka lakini pia kutoa msaada katika rasilimali fedha kwa ajili ya kuwezesha usafiri wa kukuwezesha kufika katika sehemu unayoenda kutoa elimu au kupinga ukatili," amesema Yulitha Revocatus, Ofisa Miradi kutoka Shirika la Wadada Solutions 

Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally amesema ni jukumu na wajibu wa kila raia kuunganisha nguvu kwa pamoja katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia huku wazazi  na walezi wakihakikisha wanawalea vizuri watoto wao. 

"Tusipo wekeza katika kuzuia ukatili wa kijinsia na wa watoto uzalishaji wa waharifu unaenda kwa kasi kuliko nguvu ya jamii na taasisi za vyombo vya ulinzi na usalama na hamna namna ambayo tunaweza kukabiliana navyo na utaona wajibu wa jeshi la polisi ni kuzuia uharifu kabla haujatokea kwahiyo nitaomba tuwekeze katika hilo," amesema Yassin 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu ya siku 16 za kupinga ukatili inayosema 'Wekeza kuzuia ukatili wa kijinisia'. 

Ametoa wito kwa mashirika, taasisi, makampuni na watu binafsi wenye uwezo kuwekeza katika  kuwasaidia wadau wa kupinga ukatili kufanya hivyo ili kupunguza au kukomesha kabisa vitendo hivyo. 

"Na sisi Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Mwanza tumekwisha wekeza na tunaendelea kuwekeza na tunataka taasisi na mashirika yote yanayohusika na kuzuia ukatili kuwekeza kwa nguvu kubwa kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha tunawafikia waathirika wote wa ukatili na kuwasaidia.

“Lakini pia tunaomba watu wengine binafsi wenye uwezo wajitokeze katika kusaidia mashirika haya ambayo yamesaidia kwa kiasi kukubwa kuwaokoa watoto kama hawa," amesema Kamanda Mutafungwa 

Uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili nchini na hata duniani kote huzinduliwa Novemba 25 hadi Disemba 10 kila mwaka huku ukiambatana na shughuli mbalimbali za kupinga vitendo hivyo.