Wafanyabiashara 15 watelekeza vibanda soko Tarakea
Muktasari:
Vibanda hivyo vya halmashauri vimeachwa na wafanyabaishara hao kutokana na kuzagaa ovyo kwa uchafu unaotokana na dampo ambalo lipo mbele ya vibanda hivyo zaidi ya 15.
Rombo. Wafanyabiashara waliokodi vibanda vya Halmashauri zaidi ya 15 katika soko la Tarakea Wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro wamevikimbia vibanda hivyo vya biashara kwa madai ya kuzagaa uchafu unaotokana na dampo lililopo mbele ya vibanda hivyo.
Wamesema uwepo wa dampo hilo mbele ya vibanda umewakosesha wateja kutokana na uchafu uliolundikana kwa muda mrefu hali inayotishia usalama wa afya za watu.
Hata hivyo Mwananchi digital ilifika sokoni hapo na kushuhudia vibanda hivyo vikiwa vimefungwa na uwepo wa taka zilizokuwa zimezagaa mbele ya vibanda hivyo vya biashara na pembezoni mwa soko hilo.
Soko la Tarakea ni soko maarufu Wilayani Rombo na lipo mpakani mwa Kenya na Tanzania ambapo ni moja ya vyanzo vya mapato katika halmashauri hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi digital wafanyabaishara hao wamesema suala la dampo hilo limeshindwa kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu na kwamba taka zilizopo kwenye dampo hilo zimekuwa zikikaa kwa zaidi ya miezi miwili.
Charles Tesha, ambaye ni mfanyabiashara katika soko hilo amesema amelazimika kuondoka kwenye kibanda alichokodi kwenye halmashauri hiyo kutokana na changamoto ya uchafu unaotokana na dampo hilo ambalo lipo mbele ya vibanda hivyo.
"Nilikuwa na biashara yangu hapa lakini kutokana na hali ya uchafu uliopo katika soko hili imebidi nifunge biashara nitafute sehemu nyingine, hebu angalia huu uchafu ulivyotapakaa hapa, kwa namna hii huwezi pata mteja na pia ni hatari kwa afya za watu, hii imekuwa ni kero ya muda mrefu, Serikali iangalie jambo hili kwa umakini wake maana tunalipa kodi kwenye hivi vibanda na ushuru nao unalipwa".
Naye Getruda Kavishe amesema dampo hilo limekuwa ni kero kwa wafanyabaishara na jamii inayozunguka eneo hilo la soko kutokana na kutapakaa ovyo kwa uchafu ambapo amesema kipindi cha mvua eneo hilo linakuwa ni zaidi ya choo.
"Ukiangalia hili soko ni soko ambalo lipo mpakani mwa Tanzania na Kenya na linaingizia Serikali mapato kwanini wameshindwa kutafuta sehemu ya kuhamishia hili dampo ambapo haitaleta adha kwa wafanyabaishara cheki vibanda vyote hivi vimefungwa kutokana na uchafu kukusanywa mbele ya hivi vibanda ni mteja gani ambaye anaweza kuja na kuingia hapa".
Mwenyekiti wa kijiji cha Mbomai lilipo soko, Andrea Sarita amesema kero hiyo ni ya muda mrefu na kwa mara kadhaa wamekuwa wakizungumza kwenye vikao vyao vya kijiji na kata bila mafanikio.
"Soko hili ni chafu kwa muda mrefu na hata mtaani pia ni kuchafu sana, kijiji hiki kilibuni mradi wa uzoaji taka kwenye haya maeneo na mji wa Tarakea na wananchi walikuwa wanachangia fedha za taka Sh1000 baada ya mradi huu kufa hakuna kilichoendelea na badala yake halmashauri inachokifanya inakusanya fedha kwa wananchi Sh3000 na taka haziondolewi zaidi ya miezi miwili, hali ambayo imegeuka kuwa ni kero kubwa kwa wananchi pamoja na wafanyabiashara".
Alipotafutwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Godwin Chacha alisema yupo kwenye vikao Dodoma ambapo baadaye alipotafutwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Hamis Maiga alisema tayari wameshakaa kwenye vikao na kukubaliana kuondoa taka hizo kesho Jumatatu Oktoba 3, 2022.