Wafanyakazi Tanesco mbaroni kwa kuunganishia wateja 21 umeme kinyemela

Muktasari:

  • Watu 17, wakiwemo wafanyakazi wa Tanesco Kilimanjaro, wamematwa kwa kutoza wananchi Sh400,000 kila mmoja kuwaunganishia umeme kinyemela. Kiongozi wa mtandao wa 'vishoka' naye akamatwa. 

Moshi. Watu 17 wakiwamo wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), mkoani Kilimanjaro wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kujipatia zaidi ya Sh8 milioni kwa kuwaunganishia umeme watu 21 kinyemela.

Wananchi hao wakazi wa Kibosho, wilayani Moshi wanadaiwa kuunganishiwa umeme kwa nyakati tofauti, kila mmoja akitozwa Sh400, 000 kwa huduma hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kukamatwa kwa watu hao.

Amesema miongoni mwa wanaoshikiliwa yupo kinara ambaye ni kiongozi wa mtandao wa ‘vishoka' mkoani Kilimanjaro.

"Tumemshakamata kiongozi mkubwa wa hicho kikosi, ambaye amekuwa akishirikiana na mtandao mkubwa uliopo ndani ya watumishi wa Tanesco, wote hawa tumewakamata, tuko kwenye hatua nzuri," amesema Kamanda Maigwa

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori amesema watu hao wamekuwa wakiihujumu Serikali, wakiikosesha mapato kwa manufaa bianfsi.

Amesema mpaka sasa watu 21 katika maeneo ya Kibosho wamefungiwa umeme kinyume cha utaratibu na fedha haziingi serikalini.

"Jambo hili tumeligundua katika Kata ya Kibosho, hawa watu walikuwa wanaenda kuwaunganishia wananchi umeme kwa utaratibu ambao haufahamiki ndani ya shirika, hii ni kuihujumu Serikali na kuikosesha mapato," amesema.

Mkuu huyo wa wilaya amesema, "jambo hili ni la hatari hata kwenye usalama wa wananchi kwa sababu watu waliokuwa wakifanya hujuma hii hawakuwa wakifanya kwa kufuata utaratibu wa kisheria na wa kitaalamu.”

Amelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua ambazo wameendelea kuchukua kushughulikia suala hilo kwa weledi.

Alipotafutwa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kilimanajro, Grace Ntungi, amesema hawezi kuzungumzia kwa kuwa ni liko kwenye upelelezi.

"Hizi taarifa zipo chini ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi, taratibu za uchunguzi zitakapokamilika tutatoa pia taarifa ili tusije kuvuruga utaratibu," amesema.