Waganga wakuu wapewa maelekezo usimamizi sampuli za vipimo vya VVU
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, Jafar Haniu amewataka waganga wakuu kusimamia usafirishaji sampuli za maabara na kuimarisha afua za maambukizi ya VVU
Mbeya. Waganga wakuu wa hospitali za mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi na Rukwa wameagizwa kusimamia utunzaji na usafirishaji wa sampuli za maabara na kuimarisha afua za maambukizi ya VVU katika vituo vya kutolea huduma.
Hatua hiyo iende sambamba na kufanya ziara ya kukagua vituo vya afya zahanati zilizofanyiwa ukarabati kupitia ufadhili wa PEPFAR kama zinalingana na thamani ya fedha, na kuchukua hatua kwa watakao bainika kufanya ubadhirifu.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe , Jafar Haniu ametoa maelekezo hayo leo Alhamisi Juni 6,2024 alipokuwa akipokea vifaa vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya Sh132.9 milioni kwa ajili ya Hospitali za Mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi na Rukwa.
Vifaa hivyo vimetolewa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (PEPFAR) kupitia WRAIR na HJFMRI kwa lengo la kutekeleza afua za mapambano dhidi ya Ukimwi.
"Waganga wakuu kasimamieni hospitali zote zinazonufaika kupitia HJFMRI kwa kutekeleza afua za VVU ikiwamo ajira kwa watumishi wa kada za afya kwa lengo kutekeleza mapambano dhidi ya Ukimwi sambamba na ukaguzi wa vituo ya afya na zahanati "amesema Haniu.
Haniu amesema Serikali itaendelea kutekeleza afua za Ukimwi katika kuimarisha huduma za maabara katika hospitali, vituo vya afya na zahanati kwa kushirikiana na wadau.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa HJFMRI Tanzania ,Dk Sally Chalamila amesema lengo la kutoa vifaa na mashine za maabara ni kuwezesha watoa huduma kufanya tafiti za sampuli na kupata tiba za wagonjwa.
Amesema maabara hizo zitaboresha upatikanaji wa huduma katika mikoa hiyo kwa lengo ni kufikisha huduma kwa jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkazi wa WRAIR ,Mark Breda amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU.
"Vifaa hivyo vina thamani ya Sh132.9 milioni vimetolewa kwa mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi sambamba na mashine ya uchunguzi saratani ya mlango wa shingo ya kizazi yenye thamani ya Sh30 milioni,"amesema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk Jonathan Ludemo amesema vifaa hivyo vya maabara vitawezesha tija kwa Watanzania na kupata huduma stahiki.
"Kwa niaba ya wenzangu mikoa ya nyanda za juu kusini tumeona jinsi gani wadau wanaboresha upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa sampuli za magonjwa mbalimbali katika kufikisha huduma kwa jamii, "amesema.