Wagombea waangushwa na wapiga kura waliowaamini

Muktasari:

  • Wakati kampeni za wagombea wa urais nchini Kenya zikikusanya idadi kubwa ya wananchi kila kona ya nchi hiyo yenye wapiga kura milioni 22.1, hali imekuwa tofauti kwa idadi ya wapiga kura wachache kujitokeza siku ya kupiga kura.


Nairobi. Wakati kampeni za wagombea wa urais nchini Kenya zikikusanya idadi kubwa ya wananchi kila kona ya nchi hiyo yenye wapiga kura milioni 22.1, hali imekuwa tofauti kwa idadi ya wapiga kura wachache kujitokeza siku ya kupiga kura.

Mpaka kufikia saa 9 alasiri jana, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo (IEBC), Wafula Chebukati alisema kuwa idadi ya wapiga kura waliojitokeza mpaka jana jioni kupiga kura kwa kutambuliwa na mfumo wa kielektroniki wa Kiems ni asilimia 65.4% (milioni 14.1) ya wapiga kura wote.

Hali hii ni tofauti na mategemeo ya watu wengi ambao walidhania uchaguzi wa mwaka huu uliojaa tambo, vijembe na kejeli hasa kwa wagombea mahasimu wawili, mmoja akipeperusha bendera ya Azimio la Umoja, Raila Odinga na mwingine akigombea kupitia tiketi ya Kenya Kwanza, William Ruto.

Eneo ambalo linatajwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura la Mlima Kenya, limeonekana kuwa na muitikio mdogo wa wapiga kura huku wengi wakihusisha hali hiyo na ukabila, kiasili eneo hili linakaliwa na watu wa kabila la Kikuyu ambao kwa uchaguzi wa mwaka huu kabila hilo halikutoa mgombea wa nafasi ya urais.

“Mlima Kenya kwa mtazamo wangu jamii ya Wakikuyu watakaa pembeni kwa zaidi ya misimu miwili mpaka wapate mtu mwenye ushawishi, hii ni ishara nzuri kwenye kuziacha siasa za ukabila na kuonyesha kwamba uchaguzi wa Kenya hauamuliwi na kabila moja,” alisema Joy ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa akiwa kwenye mahojiano na runinga ya NTV.

Muamko huo unatajwa kuwa ni mdogo zaidi kuwahi kutokea kwenye chaguzi za hivi karibuni, hususani ule wa mwaka 2013 na wa mwaka 2017.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2013 uliofanyika Machi 4 mwitikio wa wapiga kura ulikuwa asilimia 85.9, huku ukihusisha vinara wawili wa siasa nchini humo, mmoja akipeperusha bendera ya Jubilee, Uhuru Kenyatta ambaye alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 50.51 akifuatiwa na aliyekuwa mpinzani wake wa wakati huo na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga akiwakilisha muungano wa CORD.

Mchuano wa mwaka 2013 ulikuwa mkali, hali hiyo ilichagizwa na Rais aliyekuwepo madarakani kwa wakati huo, Mwai Kibaki kumaliza muda wake wa kuongoza kikatiba wa mihula miwili hivyo Wakenya kuwa na ari ya kumpata Rais mpya.

Miaka mitano nyuma, yaani 2017, uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ulifanyika Agosti 8, huku ukiwahusisha mahasimu walewale wa mwaka 2013, huku ikiwa ni mara ya sita kwa waziri mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Raila Odinga kuwania nafasi hiyo ya urais, hata hivyo mwamko ulikuwa mkubwa na asilimia 76.6 ya waliojiandikisha kupiga kura walitimiza haki yao hiyo ya msingi.