Wahamiaji 14 kutoka Ethiopia wakamatwa Kilimanjaro

Afisa uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishana msaidizi mwandamizi wa uhamiaji, Agustino Malembo.
Muktasari:
- Wahamiaji hao wamekatwa wilayani Moshi wakiwa wamejificha kwenye makorongo, katika Kilima cha Kifimbo, Kijiji cha Kilototoni wilayani humo.
Moshi. Wahamiaji 14, raia wa Ethiopia, wamekamatwa na Jeshi la Uhamiaji mkoani Kilimanjaro wakituhumiwa kuingia nchini kinyume cha sheria.
Wahamiaji hao walikamatwa Septemba 11, 2024, saa 3:30 asubuhi wakiwa wamejificha katika kilima cha Kifimbo kilichopo Kijiji cha Kilototoni, Wilaya ya Moshi, baada ya jeshi hilo kupata taarifa za uwepo wao.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Septemba 12, 2024, mjini Moshi, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Agustino Malembo amesema raia hao walikamatwa wakiwa wamejificha kwenye makorongo yaliyopo katika kijiji hicho.
“Tuliwakamata wakiwa wamejificha kwenye makorongo katika kilima cha Kifimbo. Inaonyesha kuna watu walikuwa wanawasafirisha, walipofika kwenye eneo hilo wakawaficha hapo, na inaonekana wanajificha huko mara kwa mara, maana tumekuta vitu mbalimbali kama malapa na mikate,” amesema.
Hata hivyo, Malembo alibainisha kuwa kwa sasa wanaendelea kuwahoji wahamiaji hao, na baada ya hapo taratibu nyingine za kisheria zitaendelea, ikiwemo kuwapeleka mahakamani.
Aidha, ameeleza kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi, hususani viongozi wa ngazi ya chini, ili watoe ushirikiano pindi wanapowaona wahamiaji haramu wanaoingia nchini bila kufuata utaratibu watoe taarifa ili hatua zichukuliwe.
“Elimu kuhusu ‘Mjue Jirani Yako’ inaendelea kutolewa na maofisa uhamiaji kwa wananchi, hususani maeneo ya mipakani, ili wawafahamu wageni wanaoingia na kufanikisha jitihada za kudhibiti wahamiaji kuingia nchini bila kufuata utaratibu,” ameongeza Malembo.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, mkazi wa Moshi, Daniel John amesema elimu ya kina inapaswa kutolewa kwa wananchi, hususani wa mipakani, ili kudhibiti wahamiaji haramu kabla hawajaingia nchini.
“Wahamiaji haramu hawa wanapita maeneo ya mipakani ambako kuna watu, watu hawa wanapaswa kuelimishwa madhara ya kukaribisha watu wasiowafahamu, ili wote wawe na uelewa na kushiriki kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu kuingia nchini,” amesema.