Wahamiaji 38 wakamatwa Tanzania warudishwa makwao

Muktasari:

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro imewakamata raia 38 wa mataifa mbalimbali wakiwemo 19 wa Kenya kwa kosa la kuingia Tanzania kinyume cha sheria.

Moshi. Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro imewakamata raia 38 wa mataifa mbalimbali wakiwemo 19 wa Kenya kwa kosa la kuingia Tanzania kinyume cha sheria.

 Mkuu wa Idara ya uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, kamishna msaidizi wa uhamiaji Edward Mwenda ameeleza hayo leo Alhamisi Juni 17, 2021 wakati akizungumza na Mwananchi Digital.

Amebainisha kuwa raia hao wamekamatwa katika operesheni ya kukabiliana na wahamiaji mkoani humo iliyoanza Juni Mosi, 2021.

Ameeleza kuwa raia wa Kenya wamekamatwa katika maeneo ya Holili, Himo na maeneo mengine ya mpakani wilayani Rombo kwa kosa la kuingia nchini isivyo halali lakini walipewa elimu ikiwa ni pamoja na kutakiwa kufuata sheria zilizopo na kupewa amri ya kuondoka nchini.

Amesema wengine 19 ni kutoka mataifa mbalimbali waliokamatwa kwa kosa la kuishi na kufanya kazi nchini  bila ya kuwa na vibali.

"Wapo ambao vibali vilikuwa vimeisha na wengine walikuwa wakifanya kazi tofauti na vibali walivyoomba, walipewa adhabu ya kutozwa ada ya hati maalumu na kuweza kukusanya Dola 11,400 za Marekani," amesema.