Wahitimu kidato cha sita waitwa JKT

Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Hassan Mabena

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza tangu mafunzo kwa mujibu wa sheria kwa wahitimu wa kidato cha sita yarejeshwe, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewaita wahitimu wote wa kidato cha sita wa mwaka 2023 kujiunga na mafunzo hayo.

Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewataka vijana wote waliomaliza kidato cha sita mwaka 2023,  kuripoti katika makambi ya jeshi hilo kwa ajili ya mafunzo ya kwa mujibu wa sheria kuanzia Juni Mosi hadi 11 mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Mei 25, 2023 na Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena akitoa taarifa iliyotolewa kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi hilo, Meja Jenerali Rajabu Mabele.

“Wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho wanatakiwa kuripoti katika kambi Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina  miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo,”amesema.

Aidha, limewataka vijana hao kuja na bukta ya rangi ya Dark blue yenye kiuno iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini isiyo na zipu.

Vingine ni t-shirt ya rangi ya kijani, raba za michezo zenye rangi ya kijani au blue, shuka mbili za kulala zenye rangi ya bluu bahari, soksi ndefu za rangi nyeusi na nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi.

Vingine track suit ya rangi ya kijani au bluu, nyaraka zote zinazohitajika katika usajili wa kujiunga na elimu ya juu, zikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya kuhitimu kidato cha nne.

Brigedia Jenerali Mabena, amesema vijana hao wanahitajiika kwenda na nauli za kwenda na kurudi nyumbani.

Amesema orodha ya majina na makambi waliyopangiwa na maeneo yaliyopo yanapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni WWW.jkt.go.tz.

Amesema utaratibu kupata kambi walizopangiwa umerahisishwa ambapo kijana ataandika majina yake matatu aliyotumia kwenye mtihani na kupata jina la kambi alilopangiwa na eneo lilopo.