Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahitimu Shule ya Msingi Oysterbay Wakabidhi mtambo wa kusafisha maji

Muktasari:

  • Wahitimu hao, kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya, Thomas Apson, walitembelea shule hiyo Desemba 2024 na kufanya tathmini ya mahitaji ya haraka.

Dar es Salaam. Wanafunzi waliohitimu  darasa la saba katika Shule ya Msingi Oysterbay 1985, wameikabidhi shuleni hapo mtambo wa kisasa wa kusafisha maji kwa teknolojia ya Reverse Osmosis (RO) wenye thamani ya Sh13 milioni.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mtambo huo jana Jumamosi Juni 6, 2026, Mwenyekiti wa kundi la wahitimu hao, Francis Haule amesema mradi huo ulitokana na ziara waliyoifanya shuleni hapo Januari mwaka jana na kubaini changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo yenye historia ndefu.

Amesema wahitimu hao walitembelea shule hapo Desemba 2024 na kufanya tathmini ya mahitaji ya haraka, ikiwemo ukarabati wa ukumbi wa shule, paa na dari, maboresho ya mazingira ya kusomea, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kufundishia kama smart boards na televisheni janja kwa madarasa ya awali, msingi wa chini na msingi wa juu.

Aidha, shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa vyoo takribani 20 na inahitaji maboresho katika ofisi ya mwalimu mkuu.

Haule amesema baada ya kubaini changamoto hizo, waliamua kuchangishana fedha ambazo wameanza na utatuzi wa tatizo la maji kutokana na umuhimu wake kwa afya na ustawi wa wanafunzi.

“Leo hii wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wanaweza kupata maji safi ya kunywa moja kwa moja kutoka kwenye bomba. Kundi letu lina wanachama 76, lakini 30 walichangia moja kwa moja utekelezaji wa mradi huu,” amesema Haule.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na baadhi ya walimu waliowafundisha wahitimu hao walipoanza darasa la kwanza mwaka 1979.

Ofisa Elimu, Vifaa na Takwimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Moshi Abdallah amewapongeza wanafunzi hao wa zamani kwa uzalendo na kujitolea.

“Hali hii ni mfano wa kuigwa. Tunawahamasisha wahitimu wa shule nyingine kujitokeza kusaidia kutatua changamoto zinazokabili shule walizosoma,” amesema Abdallah.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Igidius Mjunangoma amesema mradi huo utanufaisha wanafunzi 1,507 pamoja na walimu na wafanyakazi wasaidizi.

“Jukumu letu sasa ni kuhakikisha mtambo huu unatunzwa vizuri ili uendelee kunufaisha jamii nzima ya shule yetu kwa miaka mingi ijayo,” amesema Mjunangoma.

Naye Mhandisi Twisa Emmanuel, mmoja wa wataalamu waliohusika kuusimika mtambo huo amesema una uwezo wa kuzalisha hadi lita 500 za maji safi kwa saa.

Amesema sampuli zilizochunguzwa katika Taasisi ya Maji ya Wizara ya Maji zimeshawathibitishia kuwa maji hayo ni salama kwa matumizi ya binadamu.

“Huu ni mfumo wa kisasa unaoboresha ubora wa maji kwa kuondoa chumvi na uchafu unaoweza kuhatarisha afya ya watumiaji,” amesema Emmanuel.