Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muwasa yakamilisha mradi wa majitaka wa Sh33.3 bilioni, wananchi wapinga bei

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza katika kikao cha wadau kujadili bei ya huduma za majitaka mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Kata zinazotarajiwa kunufaika na mradi huo wa majitaka kwa awamu ya kwanza ni Kitaji, Mwigobero, Mwisenge, Iringo na Mukendo huku wananchi wa Musoma wakiiomba Ewura kupunguza bei zilizopendekezwa za huduma hiyo wakidai ni kubwa kwa watumiaji wa kawaida.

Musoma. Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) imekamilisha utekelezaji wa mradi wa majitaka wa zaidi ya Sh33.3 bilioni uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu, huku wananchi wakitaka bei zilizopendekezwa za huduma hiyo zipunguzwe.

Mradi huo wa awamu ya kwanza utahudumia kata za Kitaji, Mwigobero, Mwisenge, Iringo na Mukendo katika Manispaa ya Musoma, huku awamu ya pili inayotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh23 bilioni ikitarajiwa kuanza muda wowote.

Akizungumza leo Ijumaa, Mei 29, 2026 katika kikao cha kujadili maombi ya bei za muda za huduma hiyo kilichoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Mkurugenzi Mtendaji wa Muwasa, Nicas Mugisha amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa kituo cha kutibu majitaka na vituo vinne vya kusukuma majitaka.

Amesema kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo 56 katika shule za msingi 20, vyoo vitatu kwenye masoko na vyoo viwili katika maeneo ya wazi ili kuboresha usafi wa mazingira.

“Kazi hizi zimefanyika kuhakikisha mradi unafanya kazi kwa ufanisi na wananchi wanapata huduma bora ya usafi wa mazingira,” amesema Mugisha.

Amesema kwa kuwa mradi huo unahitaji gharama za uendeshaji, Muwasa imewasilisha maombi ya kupanga bei kwa Ewura ili kuhakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu.

Kwa mujibu wa Mugisha, mamlaka hiyo inapendekeza gharama za huduma ya majitaka kwa watumiaji wa majumbani kuwa kati ya Sh832 hadi Sh1,064 kwa ujazo, taasisi Sh1,112, biashara kati ya Sh1,200 hadi Sh1,304 na viwanda Sh1,224.

Amesema tayari mradi umeanza kufanya kazi kwa majaribio na iwapo Ewura itaidhinisha mapendekezo hayo, Muwasa itaweza kuendesha mradi kwa ufanisi na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Musoma wamepinga viwango hivyo wakidai ni vikubwa kwa wananchi wa kawaida.

Mkazi wa Musoma, Kuboja Bwire amesema gharama hizo zinaweza kuwafanya wananchi wengi kushindwa kuunganishiwa huduma hiyo muhimu.

“Sh832 hadi Sh1,064 kwa ujazo ni kubwa sana kwa mwananchi wa kawaida. Angalau bei iwe kati ya Sh300 hadi Sh800 ili watu wengi waweze kumudu,” amesema.

Naye Charles Biswaro amesema upangaji wa bei unapaswa kuzingatia hali ya uchumi wa wananchi.

“Hii ni huduma muhimu, si biashara. Watu wengine wanashindwa hata kulipia huduma ya maji safi, hivyo bei hizi zinaweza kuwa mzigo mkubwa,” amesema.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nyirabu Musira amesema bado kuna hatua mbalimbali za kupitia kabla ya mamlaka hiyo kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu maombi hayo.

Amewataka wananchi kuendelea kutoa maoni yao hadi Juni 18, 2026, akisema Ewura itazingatia hali ya kiuchumi, maoni ya wananchi na umuhimu wa huduma hiyo kabla ya kufanya uamuzi.

“Kabla ya kupitisha bei za huduma, tunazingatia uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji wa wadau na uendelevu wa huduma. Pia wadau wana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 21 kwa Baraza la Taifa la Ushindani iwapo hawataridhika,” amesema.

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewataka viongozi wa Serikali na taasisi zake kusimamia kikamilifu suala la usafi wa mazingira ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko.

Amesema Mkoa wa Mara unapaswa kurejea kuwa kinara wa usafi wa mazingira nchini kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Mji wa Musoma ulikuwa kinara wa usafi nchini lakini hali hiyo imepungua. Viongozi simamieni usafi wa mazingira ili mji huu urejee katika hadhi yake,” amesema.

Mtambi pia amewataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka hovyo akisema uchafuzi wa mazingira unachangia milipuko ya magonjwa na mafuriko kutokana na kuziba kwa mitaro.