Waishukuru Serikali kwa kuruhusiwa kuhamia Engaruka
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Aldarpoi, wilayani Ngorongoro akiwa ametoka kuvuna kuni karibu na eneo wanaloishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Muktasari:
- Wananchi ambao ni wa jamii ya kifugaji ya Kimasai wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, katika Kijiji cha Aldarpoi mkoani Arusha wameishukuru Serikali kwa kuwaruhusu kuhama kwa hiari katika hifadhi hiyo na kwenda eneo la Engaruka wilayani Monduli.
Ngorongoro. Wananchi ambao ni wa jamii ya kifugaji ya kimasai wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, katika Kijiji cha Aldarpoi mkoani Arusha wameishukuru Serikali kwa kuwaruhusu kuhama kwa hiari katika hifadhi hiyo na kwenda eneo la Engaruka wilayani Monduli.
Wananchi hao wamesema baada ya serikali kukamilisha mchakato wa malipo ya fidia muda wowote kuanzia sasa wataanza kuondoka ndani ya hifadhi hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kwa kuwa Serikali imeona ni vyema kupisha eneo hilo la hifadhi ni wakati sasa wa serikali kumpa nafasi kila mwananchi kuchagua eneo lake analotaka kwenda kwa ajili ya usalama wa mifugo yake.
Caroline Lucas, mkazi wa Kijiji cha Aldarpoi kilichopo kata ya Enduleni, tarafa ya Ngorongoro amesema shughuli ya kuhama kwa hiari kupisha uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni la kuungwa mkono na jamii ya wafugaji.
“Tunashukuru kwa msaada huu tuliopewa na serikali kuondoka kwa hiari katika eneo hili la hifadhi na kwenda Engaruka, kwa kutupa fursa ya kuchagua eneo tunakotaka kwenda tunamshukuru sana na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema katika kutekeleza majukumu yake," aliongeza Caroline .
Norimoipoi Segulan, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio chao cha kutaka kwenda eneo la Engaruka mkoani humo na kuwataka wananchi wengine ambao hawajajiandikisha kwa ajili ya kuondoka katika maeneo hayo wafanya hivyo mapema.
"Ambao hawajajiandikisha nawashauri wajiandikishe kuondoka ili kuepukana na migogoro na hifadhi ili wanyama nao wapate fursa ya kuishi huku kwani tunaishi sehemu ya hifadhi ya wanyama," alisema Norimoipoi.
Kwa upande wake mmoja wa wazee wa mila wa jamii hiyo ya kimasai, Thomas Oleyapa, mkazii wa Kijiji cha Aldarpoi A amesema endapo serikali itampa kila mmoja nafasi ya kuchagua eneo analotaka kwenda itakuwa ni rahisi kwao kuondoka kwa hiari yao wenyewe.
"Nimeamua kuhama hapa kubadilisha mazingira kutoka eneo la Ngorongoro kama ilivyotangazwa na serikali lakini sio kwa ubaya japokuwa nilitaka mwenyewe nihame ili kubadilisha mazingira na hali ya hewa.
"Wale watu wanaoomba kwenda sehemu nyingine waruhusiwe sio mpaka iwe ni lazima kwenda Msomera, mtu aseme eneo analotaka kwenda kwa ajili ya mifugo yake apewe ruhusa aende na itakuwa ni rahisi na ikifanywa hivyo tutamshukuru sana Rais kama itafanywa hivyo," amesema.
Tayari kaya zaidi ya 500 zimehama kwa hiyari kuelekea kjiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga na Serikali imetangaza kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa nyumba nyingine 5,000 katika maeneo ya Msomera, Kilindi na Kitwai.