Waislamu wahimizwa kuzidisha wema mwezi mtukufu wa Ramadhan

Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah akisalimiana na wageni waalikwa wakati wa hafla ya Iftar iliyofanyikaa jana Machi 28, 2024 jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Sheikh wa Wilaya ya Temeke Zailai Mkoyogole amesema hayo katika Iftar iliyoandaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania

Dar es Salaam. Sheikh wa Wilaya ya Temeke Zailai Mkoyogole amewataka waislamu kuzidisha wema katika mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kuwa, wanadamu ni wakosaji mbele ya Mwenyezi Mungu.

Sheikh Mkoyogole amesema hayo jana Alhamisi Machi 28, 2024 katika Iftar iliyoandaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania na kuongozwa na Mkurugenzi mkuu wake Fatma Abdallah.

Sheikh Mkoyogole akizungumza katika hafla hiyo kwa kumwakilisha Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Walid Omar, amesema: “Binadamu anamkosea Mwenyezi Mungu kwa vitu vingi, hivyo sasa ameleta mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kutubu kwa yale yote ambayo ameyafanya, kinachotakiwa katika mwezi huu ni kufanya yale yaliyomema na kurejea  kwake."

Sheikh Mkoyogole amesema Mwenyezi Mungu anapenda kuombwa, hivyo ametoa mwito kwa watu wote kurejea kwa Muumba kuomba msamaha.

Wadau mbalimbali wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania wakichukua futari iliyoandaliwa na kampuni hiyo jana Machi 28, 2024 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa Iftar hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Puma, Dk Selemani Majige amesema ni vema kila Mtanzania kwa nafasi yake kuendelea kuliombea Taifa sambamba na kumuunga mkono Rais  Samia Suluhu Hassan.

"Tunafahamu kwa sasa tunaendelea na Mfungo wa Ramadhan pamoja na Kwaresma, hivyo wakati tukiendelea na mfungo ni vema tukaliombea Taifa letu lakini wakati huohuo kudumisha umoja, amani na mshikamano," amesema Dk Majige.

Pia, amesisitiza kuendelea kudumisha amani nchini  kwa kuwa, kunafanya uchumi kuendelea kuimarika  na biashara ziendelee vizuri.

"Kulinda amani ni jambo kubwa kwa kuwa kama hakuna amani basi hata biashara haziwezi kufanyika vizuri. Hivyo, kupitia mwezi mtukufu wa Ramadhan ni vema kuendelea kumuomba Mungu na kuendelea kumuombea Rais Samia ili aendelee kutuongoza na kudumisha amani katika Taifa letu."

Pia, amewaomba Watanzania kuendelea kutumia mafuta  ya Puma Energy Tanzania pamoja na bidhaa zake zote huku akifafanua mafuta ya kampuni hiyo yana ubora na viwango vya hali ya juu.

"Tunawaomba muendelee kutumia mafuta ya Puma  ili tuongeze faida na tukiongeza faida, Serikali inapata gawio na inapotoa gawio zinapatikana fedha ambazo zinakwenda kuhudumia jamii katika maeneo mbalimbali," amesema Dk Majige.

Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah  amewashukuru wadau  waliojitokeza  katika futari hiyo huku akiwaomba Watanzania kuwaunga mkono kwa kununua bidhaa za mafuta ya kampuni hiyo.

Amesema wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali hasa katika kutekeleza matumizi ya nishati safi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la  kuendelea kutunza mazingira.

"Puma  Energy Tanzania tunatambua mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na hasa kwenye suala la nishati safi,  hivyo tutaendelea kusaidia kwa lengo la kuhakikisha  mazingira yanalindwa na matumizi ya nishati  safi kwa Watanzania yanakuwa kipaumbele."